Dar es Salaam. Wakati kikao cha siku tatu cha Kamati Kuu ya Chadema kikianza leo Mei 11, 2024, baadhi ya wagombea wa uchaguzi wa kanda nne za chama hicho wameeleza hofu ya ushindani mkali uliopo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu.
Jumla ya watia 135 nia wa nafasi mbalimbali kutoka Kanda za Serengeti (Mara, Simiyu na Shinyanga), Magharibi (Kigoma, Tabora, Katavi), Nyasa (Songwe, Iringa Njombe, Mbeya na Rukwa) na Victoria inazoundwa na mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita walianza kuwasili jana kwa ajili ya usaili na mchujo.
Nafasi zinazowaniwa ni za mwenyekiti wa kanda, makamu mwenyekiti, mtunza hazina na watendaji wa mabaraza ya chama hicho –Bavicha, Bazecha na Bawacha.
Baadhi ya wagombea waliozungumza na Mwananchi leo wamesema uchaguzi wa mwaka huu umekuwa na mwitikio mkubwa tofauti na uliofanyika mwaka 2019.
Wameeleza hayo leo Mei 11 katika ofisi za Chadema za Mtaa wa Ufipa, Kinondoni walipokwenda kujisajili katika daftari maalumu kabla ya kuitwa kwenye kamati kuu kwa usaili na mchujo kesho.
Meya wa zamani wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe amesema, “najiona natosha ndiyo maana sikujiuliza mara mbili kuchukua fomu, tunahitaji kuwa na viongozi imara wenye dira na maono ngazi ya kanda ili kuijenga Chadema.
“Tunataka Chadema ipate ushindi katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa 2025,” amesema Kimbe anayewania umakamu uenyekiti wa Kanda ya Nyasa.
Mgombea mwingine pia wa umakamu mwenyekiti Kkanda ya Serengeti, Gango Kidera ambaye amesema mtihani wake umelala kwenye shughuli ya kesho atakapoitwa mbele ya kamati kuu katika usahili.
Kidero amesema ana imani atapenya katika mchakato huo, kisha kuibuka kidedea katika nafasi hiyo ili kukisaidia chama hicho katika chaguzi zijazo za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.
“Matumaini yangu jina langu kesho lipitishwe niingie katika hatua inayofuata,” amesema Kidero.
Jackson Skania, mwingine anayewania umakamu uenyekiti wa Kanda ya Serengeti, pia amesema anajiona ana sifa stahiki za kupenya kesho, japo anaingiwa na ubaridi kutokana na ushindani uliopo.
“Sina wasiwasi na usahili wa kamati kuu, ila kinachonitia uoga ni wapinzani wangu, sijui katika kampeni watatumia silaha gani, maana kila mmoja ana mbinu zake,” amesema.
Akizungumzia uchaguzi huo, Spika wa Bunge la Wananchi (Chadema), Suzan Lyimo amesema baada ya wagombea kupitishwa na Kamati Kuu watapewa nafasi ya kufanya kampeni kwa siku saba.
“Kinachofanyika leo ni kujua idadi yao kwanza na kesho wataanza kufanyiwa usahili ikiwemo kujua kama wamekidhi matakwa ya fomu, kwa kuwa kunakuwa na wadhamini kama wamesaini na ni wanachama halali ambao wamelipia kadi zao,” amesema.
Wakati hayo yakielezwa, kikao cha Kamati Kuu kimeanza saa 5 asubuhi leo, kikifunguliwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe.
Viongozi wengine waliokuwepo ni pamoja na Makamu Mwenyekiti (Bara), Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti (Zanzibar, Said Issa Mohamed, Katibu Mkuu, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu na Benson Kigaila.
Kikao hicho imejikita katika ajenda za kupokea taarifa ya chaguzi katika ngazi mbalimbali za chama, tathmini ya maandamano na usaili na uteuzi wa wagombea wa kanda ndizo zitakazojadiliwa.
Imeandikwa na Bakari Kiango, Tuzo Mapunda na Mintanga Hunda.