Arusha. Mahakama ya Rufani imempunguzia adhabu Amedeus Kavishe kutoka malipo ya faini ya Sh1.077 bilioni au kifungo cha miaka 20 jela aliyohukumiwa baada ya kutiwa hatiani kwa kukutwa na nyara za Serikali na risasi kinyume cha sheria hadi faini ya Sh27.6 milioni.
Mahakama hiyo iliyoketi Moshi imempunguzia adhabu baada ya kumuondolea hatia katika mashtaka mengine aliyotiwa hatiani awali, isipokuwa moja ambalo alihukumiwa adhabu ya faini ya Sh27.6 milioni au kifungo cha miaka 20 jela.
Katika rufaa hiyo, mahakama imewaachia huru Fremini Mrema, Evance Shirima na Simon Tairo waliokuwa wamehukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela au faini ya Sh34 milioni kila mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kukutwa na nyara za Serikali, yakiwamo meno ya tembo yenye thamani ya Dola 60,000 za Marekani.
Rufaa namba 516/2020 na namba 725/2023 zilizounganishwa kwa kusikilizwa pamoja zilitokana na kesi ya uhujumu uchumi iliyosikilizwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Masjala Ndogo ya Moshi.
Wanne hao na Aristidius Massawe, walihukumiwa na Mahakama Kuu Oktoba 21, 2024 katika makosa sita chini ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori, Sheria ya Udhibiti wa Uhalifu wa Kiuchumi na Kupangwa, Sura ya 200 (EOCCA).
Hukumu katika rufaa ilitolewa Januari 3, 2025 na jopo la majaji Augustine Mwarija, Rehema Kerefu na Lucia Kairo na nakala kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Warufani katika Mahakama Kuu walishtakia wakidaiwa Julai 21, 2019 katika Kijiji cha Ikwini wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro, walikutwa na meno manane ya tembo yenye thamani ya Dola 60,000 za Marekani (Sh138.1 milioni) bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Pia wanadaiwa Julai, 2019 walikutwa wakinunua nyara za Serikali, (meno ya tembo) bila kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Amedeus alishtakiwa kwa makosa mengine manne akidaiwa kukutwa na nyara ya Serikali, ikidaiwa Julai, 2019 eneo la Munga, wilayani Rombo alikutwa na meno ya tembo 19 yenye thamani ya Dola 4,500 (Sh103.51 milioni).
Pia alidaiwa kupatikana na silaha kinyume cha sheria ikielezwa alipatikana na bunduki aina ya Rifle 458 iliyokuwa na risasi nane, pia alikutwa na maganda manne ya risasi kutoka kwenye bunduki hiyo pasipo kuwa na leseni.
Baada ya kupitia hoja za mawakili na sababu za rufaa za warufani wa kwanza hadi watatu, majaji walikubali sababu mbili kwamba kielelezo cha pili (meno manane ya tembo) kilikubaliwa kuwa sehemu ya ushahidi kinyume cha kanuni, kwani hakikuorodheshwa wakati shauri linasikilizwa.
Wakili wa warufani alidai kielelezo hicho kilikubaliwa kimakosa, hivyo kinapaswa kufutwa na kikifutwa ushahidi uliobaki hauwezi kuendeleza hukumu dhidi ya warufani.
Hoja ya pili ni kuwa shitaka la pili lilikuwa na dosari pamoja na kukosekana kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), na kuwa kosa la kujihusisha na nyara za Serikali lipo chini ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori, ambacho hakikutajwa katika shitaka.
Majaji katika hukumu ya rufaa walikubali sababu hizo mbili.
“Kwa makosa yote mawili, kielelezo hakikuorodheshwa wakati wa shauri hivyo hazikufikishwa kwa warufani kama sehemu ya msingi ya ushahidi ambao mwendesha mashtaka alikusudia kutegemea katika kesi hiyo, hivyo tunafuta kielelezo kutoka kwenye kumbukumbu.
“Tunaifuta siyo tu kwa warufani watatu bali kwa mrufani wa nne pia kuhusiana na makosa hayo mawili. Ufutaji huo unatosha kuondoa rufaa dhidi ya mrufani wa kwanza hadi wa tatu, hivyo tunafuta hukumu zao, kuweka kando adhabu zote mbili za faini na kifungo,” imeeleza hukumu ya majaji.
Kuhusu mrufani wa nne, Mahakama imesema wakili wa Jamhuri alianza kwa kukiri kwa vile ridhaa ya DPP ilitolewa kwa shtaka la kwanza na la pili pekee, mashitaka mengine ambayo mrufani wa nne alishitakiwa nayo yalikosa ridhaa, hivyo mwenendo wa kesi ulifanywa kuwa batili.
Alidai shtaka la kwanza, mrufani wa nne alihukumiwa baada ya kukiri.
Majaji katika hukumu walisema kukosekana kwa ridhaa ya DPP katika mashitaka yote isipokuwa shtaka la kwanza na la pili kulisababisha dosari, hivyo hukumu ya mrufani kwa makosa hayo haikuthibitishwa ipasavyo.
“Kutokana na hali hiyo, tunafuta hukumu yake katika shtaka la pili, la tatu, la nne, la tano na la sita na kufuta adhabu ya faini na kifungo alichopewa kwa makosa hayo,” imeeleza hukumu.
Kuhusu sababu zake za kukata rufaa kupinga kutiwa hatiani kwa kukiri kosa, kumbukumbu ya Julai 12, 2020 inaonyesha baada ya kusomewa shtaka alikiri makosa.
Mahakama imesema kumbukumbu za rufaa ukurasa wa 38-56 inaonyesha Julai 14, 2020 aliposomewa mara ya pili alikiri hatia na ukurasa wa 71 alinukuliwa akikiri.
“Ndiyo nimesikia ukweli, sina pingamizi, nakiri kukutwa na meno ya tembo 8, meno ya tembo 8, risasi 19, risasi 4, bunduki aina ya riffle 458. Nakiri hati ya kukamatwa kwa upande wa meno 8, vipande 19 vya meno ya tembo, risasi 8, baruti 4, riffle 458. Ninakubali cheti cha uthamini wa meno nane na vipande 19 vya meno ya tembo.”
“Kwa kuzingatia hayo hapo juu, tuna uhakika kwamba, Jaji alimpa mrufani aliyetajwa fursa ya kuelewa aina ya makosa anayoshtakiwa ikiwa ni pamoja na kosa katika shtaka la kwanza na katika matukio yote mawili mrufani wa nne alikiri hatia bila shaka,” imeeleza mahakama.
Mahakama imesema hawezi kusikilizwa sasa akilalamika kwamba ombi lake lilikuwa la usawa au kwamba lilikuwa na utata.
Hivyo mahakama ilitupilia mbali sababu za kwanza, nne, tano na sita za kukata rufaa kwa kukosa sifa.
Katika mahakama ya chini, mrufani wa nne aliyekuwa mshtakiwa wa kwanza, alikiri makosa yanayomkabili akatiwa hatiani na kuhukumiwa kulipa faini ya Sh27.63 milioni au kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kwanza.
Kosa la tatu alihukumiwa kulipa faini zaidi ya Sh1.045 bilioni au kifungo cha miaka 20 jela huku kosa la nne na tano akihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au faini ya Sh15 milioni, ambapo adhabu za kifungo zilipaswa kutekelezwa kwa wakati mmoja.
Warufani wa kwanza hadi wa tatu walikana mashtaka. Upande wa mashtaka uliita mashahidi 10 kuthibitisha kesi.
Mahakama Kuu iliridhika kwamba upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi dhidi ya Aristidius na kuamuru aachiwe huru.
Warufani watatu walitiwa hatiani na kuhukumiwa kila mmoja kulipa faini ya Sh34.5 milioni au kifungo cha miaka 20 jela.
Hawakuridhika wakakata rufaa iliyopewa namba 516/2020 ikiwa na sababu saba za rufaa, Amedeus alikata rufaa pake yake namba 725/2023 akiwa na sababu saba za rufaa. Mahakama ilizisikiliza kwa pamoja.