KIKOSI cha Yanga kikiupiga mpira mwingi kwa mtindo wao wa ‘Gusa Achia Twenda Kwao’kimefufua tumaini la kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa pili mfululizo, baada ya kuinyoosha TP Mazembe kwa mabao 3-1 jioni ya leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo uliochagizwa na mabao mawili kutoka kwa mshambuliaji chipukizi, Clement Mzize na jingine la kiungo mshambuliaji nyota, Stephane Aziz KI umetosha kuifanya Yanga ifikishe pointi nne na kutoka mkiani mwa kundi A ikiishusha Mazembe ambayo imesaliwa na pointi mbili kila moja ikicheza mechi nne.
Mazembe iliyoahidiwa mamilioni ya fedha kwa kila bao ambalo ingefunga leo na kuipa timu hiyo ushindi kutoka kwa Rais wa klabu hiyo, Moise Katumbi, ndio iliyokuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 16 tu ya mchezo baada ya Chadrak Boka kufanya madhambi yaliyozaa penalti iliyowekwa kimiani na kipa Badara Faty aliyemtungua Diarra Djigui aliyerejea uwanjani kwa mara ya kwanza kutoka kwenye majeraha.
Bao hilo ni kama liliwaamsha Yanga walioamua kutembeza boli na dakika ya 32 Mzize aliisawazishia kwa shuti kali la mbali akipokea pasi ya Boka aliyeng’ara katika beki ya kushoto.
Mchezo huo ulianza vizuri kwa wenyeji kuonyesha kuhitaji bao la kuongoza lakini wapinzani wao walianza kwa kuwaheshimu wakicheza kwa kujilinda.
Yanga walitumia eneo la kati lililokuwa likiongozwa na Khalid Aucho, Mudathir Yahya akisaidiana na Pacome Zouzoua na Aziz KI kutengeneza mashambulizi na kufanikiwa ndani ya dakika tisa wakipata kona mbili za haraka, lakini hazikuzaa matunda kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Mazembe.
Mazembe iliyoingia uwanjani kwa staili ya kujilinda zaidi na kutengeneza mashambulizi ya kushtukiza, kabla ya kupata penalti hiyo iliyotolewa na mwamuzi Ahmad Imtehaz Herreralall kutoka Mauritius na Faty kufunga bao hilo lililowatia hasira wenyeji wa mchezo, kwani licha ya kutanguliwa haikutaka tamaa na badala yake iliongeza kasi na kupata bao la kusawazisha dakika ya 32 kupitia Mzize.
Mzize alifunga bao hilo kwa shuti kali la mbali akiwa nje ya 18 akimtungua Faty aliyeruka kulidaka bila mafanikio baada ya mfungaji huyo kupokea pasi ya Boka.
Dakika mbili baadae Prince Dube na Stephane Aziz Ki walipoteza nafasi mbili za wazi ambazo zingeipeleka Yanga mapumziko ikiwa mbele, baada ya kuishia kupiga nje na kuwa kona ambazo hazikuzaa matunda.
Kipindi cha pili Yanga ilirudi na kasi zaidi ya Gusa Achia iliyowanyamisha kabisa wageni, baada ya Aziz KI kufunga bao la pili akimalizia pasi ya Khalid Aucho akiwa ndani la lango la Mazembe akimpiga tobo kipa Faty aliyetoka kumkabili.
Bao hilo lilifungwa dakika ya 56 kabla ya Mzize kukamilisha hesabu kwa kufunga bao la tatu dakika ya 60 akipokea pasi ya Dube na kuwa bao la pili kwake katika mchezo huo na hatua ya makundi.
Yanga ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Aziz Ki, Aucho na Pacome Zouzoua nafasi zao zilichukuliwa na Keneddy Musonda, Duke Abuya na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ wote waliingia kipindi cha pili cha mchezo timu yao ikiwa inaongoza mabao 3-1, huku Mazembe nayo ikibadilisha wachezaji wanne ambao hawakuweza kubadilisha matokeo ya mchezo huo.
Matokeo hayo yamerejesha tumaini kwa Yanga la kufuzu robo fainali kwa msimu wa pili mfululizo, ikisaliwa na mechi mbili, ikiwamo moja ya ugenini dhidi ya Al Hilal inayoongoza msimamo wa kundi hilo na ile ya mwisho dhidi ya MC Alger ya Algeria.
Al Hilal ina pointi tisa wakati MC Alger ikiwa na nne sawa na Yanga, lakini timu hizo mbili zimecheza mechi tatu, tofauti na Yanga na Mazembe inayoburuza mkia ikiwa na pointi mbili zilizocheza michezo minne kila moja.