Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya darasa la nne na kidato cha pili, likionya vitendo vya udanganyifu na kuahidi kuchukua hatua kwa walimu waliohusika.
Katika matokeo yaliyotangazwa leo Januari 4, 2025 na Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Dk Said Mohamed, wanafunzi 1,320,227 kati ya wanafunzi 1,530,911 waliofanya mtihani wa darasa la nne, sawa na asilimia 86.24 wamefaulu kwa kupata madaraja A, B, C na D ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.9. Kati ya waliofaulu, wasichana ni 699,901 na wavulana ni 620,326. Wanafunzi 1,633,279 walisajiliwa kufanya mtihani huo.
Matokeo hayo ni tofauti na mwaka 2023 ambao wanafunzi waliofaulu walikuwa 1,287,934 sawa na asilimia 83.3.4, hivyo kuwa na ongezeko la ufaulu kwa asilimia 2.90 kwa wanafunzi waliopata fursa ya kuendelea na darasa la tano ukilinganishwa na mwaka 2023.
Kwa kidato cha pili, Dk Mohamed amesema wanafunzi 680,574 kati ya 796,825 wenye matokeo ambayo ni sawa na asilimia 85.41 wamefaulu kuendelea kidato cha tatu ambao wamepata madaraja ya 1,2,3 4.
Amesema matokeo hayo ni tofauti na mwaka 2023 ambao wanafunzi waliofaulu walikuwa 592,741 sawa na asilimia 85 na kufanya ufaulu kuongezeka kwa asilimia 0.10.
Kwa matokeo hayo amesema wanafunzi 680,574 waliofaulu kuendelea na kidato cha tatu, wasichana ni 367,457 na wavulana ni 313,117.
Kwa wanafunzi wa kujitegemea amesema waliofaulu na kupata sifa za kufanya mtihani wa kidato cha nne ni 4,205 sawa na asilimia 55.94, huu ukiwa ni mwaka wa kwanza kwa wanafunzi wa kujitegemea kutahiniwa upimaji huo.
Waliopata ufaulu mzuri wa daraja la kwanza hadi la tatu ni 239,707 sawa na asilimia 30.08.
“Mwaka 2023 wanafunzi waliopata ufaulu wa madaraja 1 hadi la tatu walikuwa 192,633 sawa na asilimia 27.73. Hivyo ubora wa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 2.35 ukilinganisha na mwaka 2023,” amesema.
Katika hatua nyingine, pasipo kutaja idadi, amesema Necta imewazuia kujihusisha na shughuli za baraza hilo walimu waliowezesha watoto watoro kufanyiwa mitihani.
Amesema walimu hao ni wa Shule ya Msingi Bwisya iliyopo wilayani Ukerewe mkoani Mwanza na Shule ya Msingi Kininga iliyopo mkoani Songwe. Shule hizo ni za Serikali.
Amesema watawasilisha hoja kwa kuziandikia mamlaka zao za ajira ili kuwachukulia hatua za kinidhamu za utumishi wa umma.
Dk Mohamed amesema walimu hao kwa nyakati tofauti walishiriki kuwachukua watoto wa darasa la tatu, la tano na la sita kuwafanyia watoto 98 mitihani ambao walikuwa watoro.
“Pamoja na hatua zilizoanza kuchukuliwa na kamati za mitihani za mikoa, baraza litawasilisha hoja kwa mamlaka zao za ajira ili kuchukulia hatua za kinidhamu za kiutumishi wa umma ikiwemo kutenguliwa madaraka ya ukuu wa shule, kufukuzwa kazi serikalini na kufunguliwa mashtaka ya jinai au kuhujumu mitihani,” amesema.
Amesema Serikali imeweka jitihada kubwa kuzuia mianya ya udanganyifu wa mitihani, ambazo zimezaa matunda kwani takwimu za udanganyifu katika mitihani zimepungua mfulululizo kwa miaka ya karibuni.
Ameonya kuwa wakati huu nchi ikiwa katika mikakati ya maboresho ya elimu hawatakuwa tayari kuwavumilia watu wanaopanga kuhujumu elimu, akiahidi hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika.
Ametoa rai kwa wadau, wanafunzi, walimu na wazazi kuzingatia sheria na mwongozo wa uendeshaji wa mitihani ya Taifa.
Katika hatua nyingine Necta limeifungia Shule ya Sekondari Goodwill iliyopo mkoani Arusha kuwa kituo cha mitihani.
Amesema shule hiyo ambayo ni kituo cha mtihani namba S2527 kimefungiwa kutokana na mkuu wa shule na baadhi ya walimu kuthibitika kufanya udanganyifu kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi.
“Kituo hiki kilijaribu kuwarubuni walimu na askari polisi Oktoba 28, 2024 ikashindikana, mkuu wa shule akajaribu tena kuwarubuni wasimamizi wetu Oktoba 29, ikashindikana.
“Hivyo wakaamua kutafuta mbinu mbadala ya kuandaa majibu kwa kuhusisha walimu wa shule hiyo kwa kuwapanga wanafunzi kupata majibu kutoka chooni,” amesema.
Amesema baraza limeandika barua kwa Kamishana wa Elimu ili kituo hicho kifutiwe usajili kwa kukosa sifa.
“Bila shaka mzazi anapompeleka mtoto wake shuleni anatarajia pamoja na kupata elimu pia apate malezi bora na maadili,” amesema.
Amesema bila juhudi walizofanya kudhibiti hali hiyo, ni wazi wangetangaza kufuta matokeo ya watoto wote wa kidato cha pili katika shule hiyo, jambo ambalo lingekuwa hasara kubwa kwa wazazi na watoto.
Mbali na hayo, wanafunzi 105 wa darasa la nne na wanafunzi 46 wa kidato cha pili wamefutiwa matokeo kwa kufanya udanganyifu na kuandika matusi wakati wakifanya mitihani.
Dk Mohamed amesema kwa wanafunzi wa darasa la nne, 100 walifanya udanganyifu na watano waliandika matusi.
Huku kwa wale wa kidato cha pili, 41 walifanya udanganyifu na watano waliandika matusi kwenye mitihani yao.
“Matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa kifungu cha 5(2)(j) cha sheria ya Baraza la Mitihani sura 107 kikisomwa pamoja na kifungu cha 30(2) (b) cha kanuni za mitihani za mwaka 2016,” amesema.
Katika mtihani huo, somo la uraia ufaulu umeshuka kutoka asilimia 48.27 mwaka 2023 hadi asilimia 33.24 mwaka 2024.
Hata hiyo, ufaulu wa somo la Kiswahili ni asilimia 91.74 na Kichina ni asilimia 90.82. Kiarabu na Kifaransa ufaulu ni wa wastani wa kati ya asilimia 51.06 hadi 69.07. Kiingereza ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 68.27 mwaka 2023 hadi asilimia 74.58 mwaka 2024.
Kwa masomo ya ufundi, ambayo yameingia katika mtalaa mpya ufaulu ni juu ya wastani, somo la Building Construction likiwa na ufaulu wa asilimia 84.79 likifuatiwa Electrical Engineering lenye ufaulu wa asilimia 83.66.
Akizungumzia udanganyifu katika mtihani uliobanishwa na Necta, Muhanyi Nkoronko, ambaye ni mtafiti wa elimu amesema yanachangiwa na mambo mbalimbali, ikiwemo ubora wa shule kutafsiriwa kulingana na namna inavyofaulisha wanafunzi wengi, bila ya kuangalia masuala mengine muhimu.
Nkoronko amesema hata wazazi wanapotafuta shule bora kwa ajili ya kuwapeleka watoto wao hujikita kuangalia ufaulu wa shule husika.
“Hivyo, kutokana na sababu za kibiashara baadhi ya walimu ambao siyo waadilifu hujikuta wakifanya mbinu mbalimbali ikiwemo udanganyifu ili kupata matokeo mazuri waweze kuapata udahili wa wanafunzi wengi,” anasema.
Amesema udanganyifu kwa upande wa wanafunzi unasababishwa na mambo mbalimbali, ikiwemo dhana iliyopo kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuwa kufaulu sana ndiyo msingi wa kusogea mbele kimasomo na kimaisha kwa ujumla.
“Hivyo, kwa mwanafunzi hata kama hakufanya maandalizi ya kutosha atafanya kila namna ikiwemo hata kufanya udanganyifu ili aweze kufanya vizuri katika mitihani,” amesema.
Amesema hatua zaidi zinapaswa kuendelea kuchukuliwa dhidi ya vitendo vya udanganyifu kwani vina athari kubwa katika ustawi wa elimu nchini.
“Hii ndiyo sababu mtu anafaulu hadi chuo kikuu lakini uwezo wake ni mdogo na hawezi kumudu masomo, unahitajika utafiti wa kina ikiwezekana hata kubadili mfumo tunaotumia kupima wanafunzi,” amesema.
Amesema licha ya kufutiwa matokeo hatua zaidi za kinidhamu zinapaswa kuchukuliwa kwa wahusika ili kutokomeza matukio hayo.
Mdau wa elimu na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus amesema ili kuondokana na changamoto ya udanganyifu katika mitihani Serikali inapaswa kufanya uchunguzi wa kina kujua ukubwa wa tatizo ili wachukue hatua.
Akizungumzia ufaulu wa masomo mapya anasema ni hatua yenye kuleta matumaini, akitoa wito kwa Serikali kufanya juhudi kuhakikisha inazalisha walimu wa kutosha na vifaa kwa ajili ya kufundishia masomo hayo.
“Hiyo itasaidia kuongezeka zaidi ufaulu katika miaka ijayo,” amesema.
Akizungumzia ufaulu somo la lugha ya Kichina, Mkurugenzi wa Tanzania wa Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Aldin Mutembei amesema ufaulu huo umechangiwa na hamasa ya wanafunzi kusoma lugha hiyo.