Walichokisema Mbowe, Lwaitama ukomo wa madaraka Chadema

Dar es Salaam. Mjadala ulioibuliwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu kuhusu ukomo wa madaraka umezidi kupamba moto ndani na nje ya chama hicho, kila upande ukizungumzia suala hilo kwa namna tofauti.

Suala hilo mara hii limemwibua Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema na mshindani mkuu wa Lissu kwenye kinyang’anyiro cha uenyekiti wa chama hicho, pamoja na mwanazuoni wa siku nyingi, Dk Azaveli Lwaitama, ambaye pia ni mdhamini wa bodi ya chama hicho.

Akizungumza katika mahojiano na Crown Media jana Januari 3, 2025 jijini Dar es Salaam, Mbowe amesema ukomo si kipimo cha demokrasia, bali demokrasia ni haki ya kuchagua na kuchaguliwa.

“Sasa inawezekana humtaki Mbowe, mko 10 msiomtaka Mbowe, wako wengine 100 wanaomtaka, hao 100 haki yao mnaipeleka wapi? Ndiyo sababu kwenye mfumo wa demokrasia kuna uchaguzi unafanyika kila baada ya miaka mitano, ule ni ukomo wa madaraka,” amesema.

Hoja ya ukomo wa madaraka ambayo kwa miaka mingi ilikuwa inazungumzwa nje ya Chadema, iliibuliwa upya na Lissu alipotangaza kugombea uenyekiti wa Desemba 12, 2024 jijini.

Lissu alisema pamoja na kwamba ukomo uliondolewa kwenye katiba ya chama hicho mwaka 2006 kwa kuwa kilikuwa kichanga, kwa sasa unapaswa kurejeshwa kwa kuwa kimekomaa.

Alipendekeza kuwe na ukomo kwa nafasi zote na kwa wabunge wa viti maalumu wa Chadema ili kuwana nafasi wanawake wengine, baada ya waliotangulia kupata uzoefu kwa miaka mitano.

Mbowe na Lissu wote wanakubaliana kwamba katiba ya chama hicho haijaweka ukomo wa madaraka kwenye nafasi zote.

Hata hivyo, Mbowe amesema katiba hiyo ya Chadema imetoa utaratibu wa wanachama kupeleka mapendekezo endapo wanataka suala hilo liwekewe ukomo, huku akisema kwa miaka yote si Lissu aliyewahi kuwa mwanasheria wa chama, wala mwanachama mwingine yeyote aliyewasilisha pendekezo hilo.

Mbowe alipoulizwa ikiwa chama hicho kitashika madaraka, pia wataondoa ukomo wa madaraka kwenye nafasi za kisiasa ukiwemo urais, amesema serikalini ni mambo tofauti na pia suala hilo ni la kikatiba.

“Unapokuwa serikalini ni tofauti na chama cha siasa cha upinzani ambacho ni mkusanyiko wa wanachama wanaojitolea binafsi kwa njia mbalimbali. Tukiingia serikalini kuna katiba ya nchi ambayo ni ya watu wote,” amesema.

Pia amesema katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, kila chama kinajiamulia mambo yake, ikiwemo aina ya ukomo wa madaraka.

“Wewe unaweza kuondoka leo ukaenda kuanzisha chama chako, kiite jina lolote, ukaamua kwamba mtakuwa na ukomo wa madaraka, hayo ni maamuzi yako, kila chama kinasimama kinavyotaka.

“Sisi katika chama chetu hakuna ukomo wa madaraka, ACT (Wazalendo) wana term limit (ukomo wa madaraka) usitulazimishe tuwe kama ACT ndio useme ni demokrasia,” amesema. 

Mbowe amehoji sababu ya hoja hiyo kuibuliwa na Lissu wakati huu wakati alikuwemo ndani ya kamati kuu kwa miaka 20 na aliwahi kuwa mwanasheria mkuu wa chama.

“Katika nafasi ya kamati kuu amekaa miaka 20 amekuwa makamu mwenyekiti kwa miaka mitano, hajawahi kuleta pendekezo lolote.

“Ukiangalia hili ni toleo la katiba ni la 2019 (anaonyesha), Chadema imeanza mwaka 1992, kwa hiyo anajua na yeye ni mwanasheria siyo mtoto mdogo ambaye hana akili. Lakini mtu ukiamua kuchafua hali ya hewa anaichafua tu bila kujua athari yake ni nini,” amesema.

Pia Mbowe amesisitiza, ndani ya chama hicho hakuna aliyekatazwa kugombea nafasi yoyote.

“Anaposema mwenyekiti amekataa kuwa na term limit wakati yeye anatamani mwenyekiti aondoke, kuna maelfu wananiambia mwenyekiti don’t (usiondoke). Sasa hiyo ndiyo demokrasia.

“Wengine wanasema yeye kama anataka agombee, sawa, sijakataa asigombee, yeye amekuja kugombea hajanyimwa kugombea. Hata mtu yeyote akitaka kugombea agombee, mwisho wa kuchukua fomu ni Januari 5. Sasa hizo kelele za mwenyekiti hataki kuachia, inatoka wapi?” amehoji.

Akizungumza suala la ukomo wa madaraka katika mahojiano na mtandao wa Sauti Kubwa Januari 3, 2025, Dk Lwaitama amesema ukomo ni nyenzo inayotumiwa kutafutia kura kwa wajumbe.

Huku akirejea historia ya baadhi ya viongozi duniani, Profesa Lwaitama amesema wengi waliendelea kuwa viongozi kwa muda mrefu.

“Nilimwona Maalim Seif (Sharif Hamad) aliendelea kuwa kiongozi, nilimwona Abdoulaye Wade (Senegal) aliendelea kuwa kiongozi, niliona Dk Kiiza Besigye (Forum for Democratic Change (FDC- Uganda), niliona Mwalimu Julius Nyerere aliendelea kuchaguliwa (CCM).

“Kwani walikuwa wanajichagua? Mbona kama wanashambuliwa wakati hakuna kikomo kwenye katiba yao, kuna tatizo gani? Wajumbe ndio wataamua vilevile,” amesema mtalaamu huyo wa falsafa.

Ametoa pia mifano ya viongozi wakiwamo Mao Tse Tung (China), Fidel Castrol (Cuba) akisema waliendelea kuwa viongozi wa vyama vyao.

“Hiyo dhana inatajwa sana na watu wa CCM ambao wao mwenyekiti wao aliendelea mpaka miaka 30 na kitu, alipoamua mwenyewe na alikuwa amejipanga kuondoka,” amesema.

Profesa Lwaitama aliyesema kuwa hatapiga kura, amesema wajumbe ndio wataangalia uzito wa hoja na kuamua kupitia sanduku la kura.

“Wanaweza kumchagua mtu mwingine kabisa, wakasema kwa kigezo hicho basi watamchagua Odero, watasema kwanza wewe Lissu ulikuwa makamu mwenyekiti.

“Wanaweza kutumia uzoefu na matokeo, yaani huyu Mbowe alianza wana mbunge mmoja mpaka wakafika wabunge 70. Wakasema hata wewe Lissu uliingizwa na huyu huyu, kwamba huyu ni mzoefu na anavutia wengine kwamba hata na wewe ukiondoka anaweza kuleta mtu mwingine,” amesema. 

Kama ni kigezo cha kuwa na mtu mpya, Profesa Lwaitama amesema wajumbe wanaweza kuwachagua wagombea wapya ambao ni Odero Charles Odero au Romanus Mapunda.

Mbowe alipoulizwa kama hawaoni athari kwa viongizi wa juu kuwania nafasi hiyo, amekiri walikutana na kubaini kuwepo athari kwa chama hicho siku za usoni, kabla ya kuamua kugombea wote nafasi hiyo,

“Tumelijadili, kama kila mmoja aliona anafaa kugombea, hatunyimani nafasi. Ila kushtuana kwamba hili unaliona limekaa sawa? Mwenzako akikwambia ameliona sawa au siyo sawa, huo ni mtazamo. Tuliona athari, naomba nikiri,” amesema.

Lissu ambaye awali alitangaza kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti na alikuwa ametangaza nia, alibadilisha gia na kutangaza kugombea uenyekiti.

Mbowe alipoulizwa kuhusu mivutano inayoendelea ndani ya chama, amesema viongozi wanapaswa kuwa wanyeyekevu na kuonya tabia ya wao kujiona mashujaa. 

“Sasa kuna watu katika siasa wanashindwa kuvumilia na kuishi na umashuhuri. Kwa hiyo umashuhuri ukimpanda anafikiri kwamba bila yeye ndiyo hakuna taasisi, siyo kweli.

“Unaweza kujipa personal glorification (kujitukuza) kwamba you are so important (wewe ni wa muhimu), unasahau kwamba wewe ni deputy (naibu) wa mtu na katika chama chetu hakuna mwenyekiti mwenza. Kuna mwenyekiti na kuna makamu mwenyekiti,” amesema.

Akizungumzia mvutano huo, Mbowe amesema japo ni bahati mbaya, lakini ni lazima utokee.

“Kiongozi anapoamua kukengeuka na kuipuuza katiba ya chama inakuwa ni bahati mbaya sana. Lakini kama Chadema, acha tupite tunakopita na hatuna sababu hata moja ya kuogopa uchaguzi,” amesema.

Alipoulizwa kama kutoogopa uchaguzi kwake kunatokana na kuwarubuni wajumbe katika chama hicho, amekanusha.

“Si kweli, kwa nini niwe na nguvu ndani ya chama, ni kwa sababu pengine mnajua mchango wangu ndani ya chama chetu?

“Na niseme tu bila kujificha, ni mtu mwendawazimu tu asiyeweza kujua mchango wangu ndani ya Chadema, ni mtu mwendawazimu anayeweza kupuuza mchango wangu kuifikisha Chadema ilipo, ni mtu mwendawazimu anaweza kutilia shaka kujitoa kwangu katika ujenzi wa demokrasia Tanzania,” amesema.

Akieleza jinsi anavyokabiliana na migogoro ndani ya chama hicho, Mbowe amesema hajawahi kuwa na masilahi binafsi.

“Mimi siongozwi na mihemko, nina uwezo wa kusikiliza sana. Wanaoleta tuhuma dhidi yangu hazijawahi kuniondoa kwenye focus (lengo) ninayoiamini na dhamira yangu katika kuyasimamia mageuzi katika nchi yangu.

“Naweza kukubali maumivu, lakini hakuna kiasi cha maumivu kinachoweza kunipotezea udhibiti na nikaingia kwenye malumbano majukwaani,” amesema.

Mbowe amesema ana historia ya kuibua vipaji vya siasa, akiwamo Lissu.

“Tafuta kiongozi yeyote wa Chadema aliyepo na aliyetoka ambaye atakwambia kwamba Mbowe hakuhusika katika kumleta kwenye siasa ndani za Chadema, akiwemo makamu wangu ambaye mnamzungumza sana, Tundu Lissu. 

“Mimi nimemleta kwenye chama kwa kumshawishi…tukamjenga, siyo kwamba tulimwingiza tukamwacha. Tulimjenga na akakisaidia chama. Sasa kunishambulia, hilo swali angelijibu mwenyewe, kwa sababu hakuna shutuma anayoitoa hadharani ambayo ni ya kweli. Tumemtaka kama ana lawama na mwenyekiti na una ushahidi lete kwenye vikao vya chama tuzungumze,” amesema.

Related Posts