Same. Changamoto ya usafiri na usafirishaji katika Tarafa za Mamba Myamba na Gonja wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro, inaelekea kuwa historia baada ya Serikali kuanza ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 36 kutoka Ndungu hadi Mkomazi.
Wakati mkandarasi akikabidhiwa jukumu la ujenzi wa barabara hiyo, pia Serikali imekamilisha mchakato wa kumpata mkandarasi atakayejenga takribani kilomita 50 kutoka Same hadi Ndungu.
Ujenzi wa njia ya Ndungu hadi Mkomazi ni sehemu ya barabara ya kilomita 100 inayoanzia Same-Kisiwani hadi Mkomazi, ikiunganisha mikoa ya Tanga na Kilimanjaro. Mchakato huo utakwenda sambamba na kuifungua Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.
Tarafa za Mamba Myamba na Gonja zinasifika kwa kilimo cha tangawizi na mpunga, hata hivyo wakulima wamekuwa wakipata changamoto za usafiri kutokana na ubovu wa barabara, hasa nyakati za mvua.
Akizungumza leo Jumamosi, Januari 4, 2025, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amewapa matumaini wananchi akisema wamepata Kampuni ya Ujenzi na Mawasiliano ya China (CCC) itakayotekeleza mradi huo kwa miezi 18.
Waziri Ulega amesema lengo la ujenzi wa barabara hiyo ni kuondoa kero kwa kuboresha mtandao wa njia hiyo sambamba na ujenzi wa madaraja ili kuongeza ufanisi kwenye sekta ya usafirishaji na usafiri.
“Matumaini yangu ujenzi wa barabara hii utaondoa kero ya usafiri na usafirishaji. Ikikamilika, pia itashusha gharama za usafiri kwa wananchi,” amesema Ulega.
Waziri Ulega ameitaka Tanroads kuwasimamia kwa ukaribu wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali, ukiwemo wa barabara ya Same-Kisiwani hadi Mkomazi, utakaogharimu Sh59 bilioni.
“Meneja wa mradi na meneja wa Tanroads Kilimanjaro wote kina mama, naamini mtaweza. Mkicheka naye nitakula sahani moja nanyi endapo nikibaini hamjasimamia vizuri. Ninawaamini, nendeni mkasimamie,” amesema Ulega.
Kabla ya kumkabidhi mkandarasi huyo, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mohamed Besta amesema zabuni ya sehemu ya tatu kutoka Same hadi Mahole yenye kilomita 56.8 kwa kiwango cha lami, mkandarasi ameshapatikana na wakati wowote mkataba utasainiwa ili kumaliza kilomita 100 za barabara hiyo.
Besta amesema barabara hiyo ni mojawapo ya mtandao muhimu katika mikoa ya Kilimanjaro, hasa Tarafa za Gonja, Ndungu na Bendera ambazo ni maarufu kwa uzalishaji wa tangawizi na mpunga, hivyo ni kiungo cha usafirishaji wa mazao hayo.
“Serikali imeshatoa Sh5.87 bilioni kama malipo ya awali kwa mkandarasi ambaye yupo katika maandalizi ya kuanza kazi. Nitoe wito wa CCC kufanya kazi kwa viwango ili ikamilike kwa wakati ambapo itakuza pia utalii kwenye Hifadhi ya Mkomazi,” amesema Besta.
Awali, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela amesema wananchi wa Same Mashariki wamefurahia mradi huo kwa kuwa kilikuwa ni kilio cha muda mrefu.