Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), Hashim Rungwe amewashauri wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya Chadema, kuepuka kupigana madongo badala yake waeleze nini watakachokifanya ili wajumbe wawachague.
Chadema inatarajia kufanya uchaguzi mkuu ifikapo Januari 21, 2025, ambapo wajumbe watachagua viongozi wa kitaifa, ukitanguliwa na chaguzi za mabaraza ya chama hicho.
Kauli ya Rungwe imekuja wakati kukiwa na mtifuano kati ya wapambe wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wa Makamu wake, Tundu Lissu wanaogombea uenyekiti. Pia wapo wagombea wengine wa wili wa nafasi hiyo, Odero Charles Odero na Romanus Mapunda.
Akizungumza katika mahojiano na mtandao wa Global leo Jumamosi Januari 4, 2025, Rungwe amewaonya wagombea wanaozungumza mambo yasiyohusu uchaguzi huo.
“Wasiwe wanazungumzazungumza mambo mengi ambayo sio ya uchaguzi, mambo binafsi hayaleti uchaguzi, mambo mengine ni criminal (jinai) hayana msingi kuzungumza kwa sababu mmeshazungumza kwenye vikao vya chama.
Hata kwenye mpira watu wanazungumza mambo yao ya ndani, sasa ukitoka nje na kwenda kutangaza, nafikiri si sawa sawa,” amesema Rungwe.
Mwanasiasa huyo mkongwe nchini amesema vyama vyote ni kawaida kukaa na kuzungumza mambo yao ya ndani na yakizungumzwa hubaki ndani.
Rungwe amekosoa madai ya kuwepo tuhuma za rushwa katika chama hicho yaliyotolewa na Lissu, akisema Tanzania nzima ina rushwa.
Amesema makamu huyo mwenyekiti wa Chadema aliwataja watu wengi kuhusika na rushwa, akisema mambo hayo kama yana ukweli polisi wangewakamata na fedha hizo.
“Kuzungumza tu kila mtu anaweza kuzungumza. Naweza kuongea wewe umeniletea rushwa lakini vyombo vya maamuzi si vipo, basi viende kumshika, twende kwenye (principal) kanuni za mazungumzo.
“Huyu anazungumza nini na huyu anazungumza nini, mara huyu kanunua gari, kwani kuna mtu nchi hii kazuiwa kununua gari?” amehoji.
Amesema kama yapo matumizi mabaya ya fedha ndani ya chama, Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) hufanya ukaguzi na kubaini dosari na ndio wakati wa kuhoji kasoro zitakazobainika.
Tuhuma za kuwepo rushwa kwenye uchaguzi wa chama hicho, zilitolewa na Lissu Mei 2, 2024 akihutubia mkutano wa hadhara mjini Iringa na alirudia tuhuma hizo katika maeneo mengine nchini.
Kuhusu mapendekezo Mbowe asigombee tena uenyekiti baada ya kuingoza Chadema kwa miaka 20, Rungwe amesema msingi unaopaswa kufuatwa ni katiba ya chama.
“Kama katiba ya chama iko wazi, Mbowe anaweza kuona anaweza kuendelea tu, unaweza kumshauri lakini atakuwa na haki ya kuendelea hadi aridhike na wanaogombea wana haki; wanachama wapigakura ndiyo wataamua,” amesema.
Uchaguzi wa Chadema umevutia mijadala mbalimbali ndani na nje ya chama hicho kikuu cha upinzani.