Daraja lililovunjika Same kujengwa usiku na mchana

Same. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amewataka wataalamu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wanaojenga Daraja la Mpirani wilayani Same kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha linakamilika ndani ya siku tatu.

Daraja hilo lililopo Kijiji cha Mpirani, Kata ya Maore, lilivunjika Januari 2, 2025 baada ya nguzo kuathiriwa na maji ya mvua.

Kuvunjika kwa daraja hilo kumekata mawasiliano katika barabara kuu ya Same-Mkomazi, Same mkoani Kilimanjaro.

Ulega ametoa agizo hilo leo Januari 4, alipotembelea eneo hilo na kueleza hadi Jumatano Januari 8, likiwa halijakamilika atarudi kuweka kambi hapo.

Amesema kipimo cha kwanza kwa wataalamu na wahandisi wa mikoa yote nchini ni utayari wao wakati wa dharura.

Ulega amewataka wataalamu kujenga daraja hilo kwa umakini na kwa tahadhari wakitambua kuwa bado mvua ni nyingi mbeleni.

“Niwapongeze Tanroads makao makuu na hapa mkoani kwa kuweka kambi hapa na kuchukua hatua za haraka. Katibu mkuu na mtendaji mkuu, kipimo chetu cha kwanza ni ule utayari wao wakati wa dharura, sisi tutampima mtu umahiri wake na uwezo wake kwa namna anavyochukua hatua za haraka wakati wa dharura, hicho ndicho kipimo chetu cha kwanza,” amesema na kuongeza:

“Mmesema mtafanya kazi usiku na mchana iwe kweli usiku na mchana, mfunge taa hapa pawe panafanyika kazi. Nimeona taa zilizopo hazitoshi, mnaweza mkaazima hata za wakandarasi mfanye kazi usiku na mchana.

“Kama mtazidisha Jumatano, mkuu wa mkoa akaniambia zimezidi, nitakuja kuungana nanyi hapa, mimi na mkuu wa mkoa tutakuja kuweka kambi hapa.”

Amesema anaamini Jumatano atapata taarifa magari yanapita na shughuli zinaendelea katika eneo hili.

“Ongezeni timu ya vibarua, hapa Mpirani wapo vijana wengi wanaotaka kushiriki, wapeni kazi. Jengeni kitu kwa uhakika na tahadhari mvua nyingi zinakuja, tusifanye makosa baada ya siku mbili matatizo yanajirudia, Watanzania hawatatuelewa,” amesema.

Akitoa taarifa, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Kilimanjaro, Motta Kyando amesema wametengeneza kivuko cha dharura cha watembea kwa miguu na magari madogo.

Amesema kazi ya utengenezaji wa daraja hilo ili kurudisha mawasiliano inafanywa na wataalamu wabobezi wa madaraja kutoka makao makuu na mkoani Kilimanjaro, akiahidi Jumatano kazi itakuwa imekamilika.

“Tunategemea kazi hii itatumia siku tatu, Jumatano tunategemea kufungua eneo hili ili magari yaweze kupita, kwani wataalamu wanafanya kazi usiku na mchana,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema kuvunjika kwa daraja hilo kumesababisha adha kubwa kwa wananchi.

Related Posts