Burkina Faso yachomoa bao ‘jiooni’

Bao la dakika ya 90 lilifungwa na Aboubacar Troure wa Bukina Faso lilizima matumaini ya Harambee ya Kenya kushinda mchezo wa kwanza wa Kombe la Mapinduzi 2025 baada ya kutoka sare ya 1-1 katika pambano kali la michuano hiyo kwenye Uwanja wa Gombani, kisiwani hapa.

Mchezo huo ambao ulipigwa juzi usiku na kuhudhuriwa na mashabiki kiasi chake ulikuwa wa ushindani  wa aina yake kwa kila timu kuonyesha ubora na ustadi na mbinu za kuushika mchezo ili kuweza kupata matokeo ya ushindi.

Harambee Stars ilikuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza mnamo dakika ya 45+3 za nyongeza kupitia mshambuliaji, James Kinyanjui baada ya mabeki wa Bukina Faso kufanya makosa yaliyotumiwa vyema na Kenya kujiapatia bao hilo la kuongoza na kufanya hadi mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Timu hizo zilirudi uwanjani kukianza kipindi cha pili kwa kila upande ukijidhatiti kwa kuyafanyia kazi mawaidha waliyopata kutoka kwa walimu wao pamoja na kufanya mabadilo kama ifutavyo.

Bukina Faso waliwatoa nje Abdouley Troure, Lagnene Isouf, Hamed Blakiss Ouattara na kuwaingiza Attou Romain, Ridouanno Maiga, Raouf Memed Dao na Hanaby Hadalou Sagne, huku Kenya ikiwapumzisha  Brian Okoth, Boniface Muchiri, Daniel Sakar na Michael Mutunda na nafasi zao kujazwa na Chripine Erambo, Mohamed Bajabir, Darius Msagah na Ben Stanley Omond.

Mabadiliko hayo yalikuwa na faida kwa Bukina Faso kupitia kiungo Raouf Memed Dao alifanya kazi kubwa ya kupeleka mashambulizi kupitia katikati na hatimae timu hiyo kuonekana wakitengeneza nafasi ya kulifikia lango la Harambee Stars, lakini wakionekana kukosa utulivu kwenye nafasi ya umaliziaji.

Hali hiyo, iliwapa nguvu hadi kufika mnamo dakika 90 timu hiyo ilipata bao la kusawazisha uliowekwa kambani na Aboubacar Traore.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Mohameed Ouattara wa Burkina Faso aliyechaguliwa kuwa Mchezaji mwenye nidhamu, alisema mchezo ulikuwa mgumu kutokana na timu hizo kukamiana kwenye mchezo.

Alisema pamoja na kupata alama hiyo moja kuna kazi kubwa inapaswa kufanywa na makocha wa timu hiyo katika kutoa maelekezo na mbinu zaidi zitakazowafaya wapate ushindi katika mchezo unaofuata.

Burkina Faso itashuka uwanjani tena kesho Jumatatu kuvaana na Zanzibar Heroes iliyoanza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Bara, ambayo yenyewe itacheza Jumanne kwa kuvaana na Harambee Stars ya Kenya.

Related Posts