Othman: Serikali inalenga kutanua fursa za elimu Zanzibar 

Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud amesema uimarishaji wa miundombinu ya shule ni ishara kuwa, Serikali inalenga kutanua fursa ya elimu na kuhakikisha hakuna kijana anayekosa haki ya kupata elimu.

Othman amesema hayo leo Jumapili, Januari 5, 2025 Maungani Wilaya ya Magharibi B Unguja baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule ya ghorofa tatu ya Maungani kwenye shamrashamra za kuelekea kilele cha miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema hatua hiyo ni jitihada za Serikali za kutatua changamoto ya uhaba wa madarasa katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar na kuleta maendeleo kwa vitendo.

 “Kuimarisha miundombinu hii ya elimu, sio tu kuwajengea misingi imara vijana wa Zanzibar kupata ujuzi na maarifa ya elimu, bali pia ni kujenga kizazi kitakachokuwa na uwezo wa kuchangia vyema maendeleo ya Zanzibar,” amesema. 

Othman amesema hali hiyo pia, itawawezesha vijana kushindana vyema katika mabadiliko ya sasa ya ulimwengu.

Amesema Zanzibar imekuwa ni miongoni mwa nchi  zenye ongezeko kubwa la idadi ya watu huku sensa ya mwaka 2022 inaonesha Zanzibar ina wastani wa ongezeko la watu kwa asilimia 3.7 kwa mwaka.

Kutokana na ongezeko hilo, kunasababisha mahitaji ya elimu kuongezeka mwaka hadi mwaka yakiwamo madarasa.

Amesema ujenzi wa shule kama hizo unatoa taswira kwamba Serikali imeguswa na idadi ya watu na kutatua changaoto hiyo. 

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohammed Mussa amesema ujenzi huo ni jitihada za Serikali kuleta mageuzi ya sekta ya elimu.

Waziri Lela amesema hakuna Taifa lolote linaloweza kuendelea bila ya watu wake kuwa na elimu na ndio maana Serikali imetoa kipaumbele chake kwenye sekta hiyo.

Akitoa taarifa ya kitaalamu juu ya ujenzi huo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Khamis Abdalla Said amesema shule hiyo itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,710 kwa wakati mmoja na kwa wastani wa darasa moja kwa watoto 45. 

Related Posts