Zambia. Jeshi la Polisi nchini Zambia linawasaka watuhumiwa walioachiliwa huru na askari polisi aliyedaiwa kulewa ili washerehekee mapokezi ya mwaka mpya 2025.
Desemba 31, 2024, ofisa huyo aitwaye, Titus Phiri aliwaachia watuhumiwa hao hatua iliyozua gumzo kwenye mitandao ya kijamii.
Msako unaendelea huku wengi wakikabiliwa na mashtaka ya uhalifu ikiwa ni pamoja na kushambulia, wizi na ujambazi.
Kitendo cha kuwaruhusu kubaki huru kunaweza kusababisha hatari kubwa kwa usalama wa umma kama alivyosema Msemaji wa Polisi, Rae Hamoonga akinukuliwa na shirika la AFP mapema Ijumaa.
Hata hivyo, Phiri alikamatwa kwa kosa la kulewa akiwa kazini na kuwaachia huru watuhumiwa hao 13 na yeye mwenyewe kukimbia.
Hamoonga amesema siku hiyo, katika Kituo cha Polisi cha Cheelo jijini Lusaka, Phiri aliyekuwa amelewa, alichukua kwa nguvu funguo za vyumba husika kutoka kwa askari mwingine.
Kisha, ofisa huyo aliwafungulia watuhumiwa huku akiwaambia “mpo huru kwenda kuupokea mwaka mpya.”
Imeandaliwa na Sute Kamwelwe kwa msaada wa mashirika.