Ukraine yaishambulia Russia kwa makombora ya ATACMS, yaahidi kujibu mapigo

Moscow. Russia imesema itajibu mapigo kufuatia mashambulizi ya makombora nane ya vikosi vya Ukraine. Ukraine ilipewa na Marekani makombora hayo aina ya ATACMS.

Kwa mujibu wa The Guardian, shambulizi la Ukraine nchini Russia lilifanyika jana Jumamosi Januari 4, 2025 ambapo makombora hayo yalilenga kupiga umbali wa kilometa 300 ndani ya Russia kutoka nchini Ukraine.

Wizara ya Ulinzi ya Russia imeripoti kuwa makombora yote nane, yakiambatana na droni zaidi ya 72, hayakupenya baada ya kudhibitiwa na mifumo ya kujilinda ya anga la Russia.

Wizara hiyo iliongeza kuwa: “Vitendo vya Kyiv ikisaidiwa na mataifa ya magharibi yatalipizwa vikali na Russia.” 

Wizara hiyo imesema droni nyingi za Ukraine zilidhibitiwa eneo la Mkoa wa Leningrad ulioko Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo na droni moja ilidunguliwa mkoani Kursk, ambako Ukraine ilifanya mashambulizi ya kushtukiza .

Rais wa Marekani anayeondoka madarakani, Joe Biden aliridhia Ukraine kutumia makombora ya ATACMS kuishambulia Russia Novemba 2024, akisema uamuzi huo unalenga kuiadhibu Russia iliyokubali kushirikiana na Korea Kaskazini.

Hata hivyo, Rais Vladimirj Putin wa Russia amekuwa akitishia kulipiza kisasi kwa mashambulizi yoyote ya Ukraine ambayo yatatekelezwa kwa kutumia makombora ya ATACMS. Putin alisema atajibu mapigo  kwa kutumia makombora ya Oreshnik.

Desemba 2024, Putin alionya kuwa shambulizi lolote la ATACMS kutoka Ukraine litakalifanyika ndani ya ardhi ya Russia, litamlazimu kuelekeza mapigo jijini Kiev. 

Kwa mara ya kwanza Russia ilitumia kombora la Oreshnik Novemba 21, 2024, makombora hayo yaliekezwa mkoani Dnipro nchini Ukraine.

Televisheni ya Taifa ya Russia (TASS) imeripoti kuwa mashambulizi ya Droni kutoka Ukraine, yameilazimu mamlaka nchini Russia kuweka kuzio la muda katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa St. Petersburg.

Gavana wa Leningrad, Aleksandr Drozdenko, alitoa taarifa kwa umma akisema: “Usiku na asubuhi ya kuamkia Januari 4, 2025, kulikuwa na mashambulizi ya droni kwa wingi katika anga la Russia eneo la Leningrad.”

Ofisa Usalama kutoka Ukraine, Andrii Kovalenko alichapisha kwenye mtandao wa Telegram kuwa mashambulizi hayo yalilenga eneo la Bahari mkoani Leningrad kuliko na miundombinu ya kiuchumi na kijeshi ya Russia.

Wakati huohuo, The Guardian imeripoti kuwa vikosi vya Russia vimekiteka Kijiji cha Nadiya kilichopo Mkoa wa Luhansk nchini Ukraine.

Huko Donetsk, Bandari ya Pokrovsk tayari iko chini ya usimamizi wa vikosi vya Russia huku uvamizi wa Russia ukiendelea pande zote Kusini na Mashariki mwa taifa hilo.

Ukraine pia inaamini kwamba kuingia kwa Donald Trump Ikulu ya Marekani Januari 20, 2025 huenda kukakomesha misaada ya kijeshi nchini humo, jambo ambalo linahatarisha ushindi wa Ukraine dhidi ya hasimu wao Russia.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika

Related Posts