Wasomea masomo ya sanaa kwenye maabara ya sayansi

Morogoro. Kutokana na uhaba wa viti, meza na madarasa, wanafunzi wa sanaa katika Shule ya Sekondari Ifakara wilayani Kilombero, wanalazimika kutumia maabara kusoma masomo yasiyohusiana na sayansi.

Wanafunzi hao ni wale walio katika programu ya kurejea shule baada ya kupata changamoto mbalimbali za kimaisha ikiwamo ujauzito.

Katika kituo hicho kuna  jumla ya wanafunzi 50, kati ya hao 26 wapo  awamu ya kwanza na 24 wapo awamu ya pili.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kuhusu  adha hiyo baadhi ya wanafunzi hao  akiwamo, Whitnes Mahanga, amesema changamoto kubwa ni kutokuwepo kwa darasa kwa ajili yao, viti na meza.

“Hali hii wakati mwingine inatulazimu kuwapisha wanafunzi wanaokwenda asubuhi shule wakati wakiwa na kipindi cha mazoezi kwa vitendo kwa masomo ya sayansi na kwenye madarasa ya kawaida hutumia wakati wanafunzi wa darasa husika hawapo shuleni.

“Hii inatufanya   tuishi kama wakimbizi hapa shuleni licha ya kuwa tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan katusaidia kurudi shule, hivyo kwa changamoto hii tunaomba wadau mbalimbali wajitokeze kutusaidia,” amesema Whitness

Leila Ally, amesema changamoto nyingine inayowakumba katika kupata elimu ni kukaa mbali na shule, hivyo kuchelewa kufika shuleni hasa katika kipindi hiki cha mvua maeneo mengi hujaa maji.

“Ukiacha viti na meza, tunaomba wadau kutusaidia kujenga bweni ili tuwe muda wote katika mazingira ya shule, kwa kuwa kwa umbali tunaotembea huenda tukajikuta tunarudi kwenye vishawishi vilivyotufanya tukatize masomo yetu ikiwemo kupata mimba,” amesema Leila.

Mwalimu wa Kiswahili, Hussein Bakari ameungana na wanafunzi hao na kusema hali hiyo inampa wakati mgumu kuwafundisha kutokana na muingiliano wa vipindi na madarasa mengine.

Mwalimu Bakari ameomba Serikali iwatengee bajeti ya kujenga darasa na kununua vifaa kwa ajili ya wanafunzi hao ili nao wajisikie kama wanafunzi wengine.

Akizungumzia hilo, Mratibu wa kituo kwa masomo ya sekondari  mbadala (SEQAEP) Wilaya ya Ifakara, Avith Mosha  amekiri kuwepo kwa tatizo hilo la uhaba wa viti na meza jambo linalowaathiri hadi wanafunzi wa kawaida shuleni hapo.

Hata hivyo, kwa upande wa madarasa amesema wapo vizuri kwa kuwa mpaka sasa wanayo 20 ambayo kila moja linatakiwa kuwa na  wanafunzi wasiozidi 50 huku shule nzima ikiwa na wanafunzi 1447.

Mosha ameomba wadau kusaidia hilo kwa kuwa tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameshaonyesha nia yake ya kuhakikisha watoto hao wanafikia ndoto zao kwa kukubali awarudi shule.

“Kwa haraka shule hii yote tunahitaji viti na meza visivyopungua 2,000 huku kwa hawa wanafunzi waliorejea shule, mahitaji yao ni viti na meza visivyopungua 100,”amesema Mosha.

Related Posts