Mwanza. Uchaguzi wa ndani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) unazidi kupamba moto baada ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, John Heche kuchukua na kurejesha fomu kuwania nafasi ya umakamu mwenyekiti – bara.
Heche aliyewahi kuwa mbunge wa Tarime Vijijini amesisitiza kuwa anayeweza kusimamia malengo ya kuanzishwa chama hicho kwa sasa ni Tundu Lissu anayewania nafasi ya uenyekiti wa Chadema taifa.
Heche anachukua hatua hiyo zikiwa zimepita siku mbili tangu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje kuchukua na kurejesha fomu ya kugombea umakamu mwenyekiti Chadema bara.
Wenje anamuunga mkono Freeman Mbowe aliyekiongoza chama hicho kwa miaka 20 tangu mwaka 2004 akichukua kijiti kutoka kwa Bob Makani ambaye alianguliwa na Edwin Mtei.
Uchaguzi wa chama hicho unafanyika Januari 21, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam na leo Jumapili, Januari 5, 2025 saa 10:00 jioni dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu litafungwa.
Akizungumza mbele ya wanachama, wajumbe wa Chadema na waandishi wa habari jijini Mwanza leo Jumapili, Heche amesema chama hicho kinahitaji watu waadilifu ili watimize malengo ya kuanzishwa kwake.
“Leo tuna watu wachache kwenye chama ambao wamepotoka wameshindwa kutambua kwa nini chama hiki kilianzishwa.”
“Na leo nasema rasmi kwamba Mwenyekiti, Freeman Mbowe kwa heshima tutakwenda kwenye uchaguzi, tutakushinda uchaguzi, namuunga mkono Tundu Lissu na nimeamua kuchukua fomu baada ya kutafakari,” amesema Heche.
Heche ameyataja malengo ya kuanzishwa chama hicho kuwa ni kushinda uchaguzi, kuiondoa CCM madarakani na kutumia rasilimali za nchi kwa mabadiliko ya watu.
“Nimekaa kimya muda mrefu, kutafakari mwenendo wa nchi na sababu ya kuundwa kwa chama hiki ndio maana nimeamua kugombea nafasi hiyo.
“Hii taasisi ni tegemeo kwa Watanzania…mimi John Heche nina uzoefu, nina uwezo, nina nguvu, nina maarifa ya kuwa makamu mwenyekiti wa hiki chama wa taifa…tuunde sekretarieti mpya ya chama chetu, tuunde na tuhuishe majimbo, tusimamie usajili wa chama na twende kwenye slogani inayosema ‘no reform no election,” na tutakavyosema hivyo hatutosema kwa maneno tu tutasema kwa vitendo na Watanzania watatuunga mkono.”
“Kwa sababu tukiruhusu katika nchi hii viongozi wasitokane na kura za watu viongozi hawatowaheshimu watu …silaha pekee inayomsababisha mbunge akae jimboni apigane kwa ajili yako ni kama kura yako inaweza kumuweka na kumuondoa madarakani,” amesema Heche
Heche amesema anampenda sana Mbowe na ndiyo amemjenga kisiasa lakini muda wa kukaa pembeni umefika na kutazama vijana wake wakifanya kazi.
“Mimi ninamuheshimu mwenyekiti na ninampenda…kwangu ni baba wa siasa ambaye amenifikisha hapa. Siwezi kusema baya kuhusu Mbowe. Nimekuwa nasema vikaoni na namshukuru kwa alipokifikisha hapa chama chetu. Leo nasema tutakwenda kwenye uchaguzi na tutakushinda,” amesema Heche huku akishangiliwa.
Akiendelea kumzungumzia Mbowe, Heche amesema, “kama kuna mtu alikuja hapa anajua nitamshambulia mtu siwezi kufanya hivyo. Bado mwenyekiti wetu (Freeman Mbowe) atabaki kuwa mjumbe wa kamati kuu. Tumefika hapa tulipo kwa sababu yake. Kujenga mtandao wa chama kama hiki ni kazi kubwa. Ndio maana mimi namuheshimu sana Freeman.”
Amesema anaamini Lissu na yeye akishinda chama hicho kitatimiza malengo ya kushika dola na kubadilisha maisha ya watu akisisitiza wanahitaji mabadiliko ndani ya chama kwa kuwa siyo jambo baya na Mbowe atabaki kuwa mjumbe wa kamati kuu.
“Muheshimiwa (Mbowe) muachie mtu mwingine akuonyeshe tunaenda wapi. Hii ni taasisi ambayo inashindana na Serikali kila siku. Hatuwezi kuaford kuua taasisi hii (Chadema) hii taasisi ni tegemeo kwa Watanzania. Hata wana CCM hawataki Chadema ife,” amesema.
Amesema kwa sasa chama hicho mtu akikemea rushwa anaitwa mropokaji lakini akishinda yeye na Lissu wataweka hadharani wala na wapokeaji rushwa kwa majina yao bila aibu, kama ambavyo wanawataja wala rushwa wengine nje ya Chadema.
“Chadema kilijijenga kwa kushambulia mafisadi. Ukila rushwa ndani ya chama tutakusema na tutakutaja jina kuwa wewe ni mla rushwa. Lissu ni mkweli na mwadilifu,” amesema.
Heche aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha) amesema, “tunaweza kutofautiana mimi na yeye (Lissu) vitu vidogovidogo, ni wakati gani wa kusema lakini Lissu ni mwadilifu, mkweli na msafi na huyo ndiyo anastahili kuwa kiongozi wetu kwa sasa.”
Heche amesisitiza ataibuka kidedea kwenye uchaguzi huo na hata kama akishindwa hatohama Chadema na kuwa endapo atashinda atafanya kazi na yeyote atakayeshinda kati ya Mbowe na Lissu.
Katika maelezo yake, Heche amesema Lissu atapata, “ushindi wa kimbunga” kwani dalili zote zinajionyesha.
Aidha, ametumia fursa hiyo kuonya makundi mbalimbali ya vijana kuacha kuwashambulia viongozi wao: “Naomba vijana wa chama wanaotukana viongozi wetu waache. Wanamshambulia na kumtukana Freeman Mbowe waache, mtu anakaa anamtukana Tundu Lissu hebu tuache.”
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho mkoani Shinyanga, Erasti Kazinja amesema endapo Mbowe atashinda kwa haki watamuunga mkono na kumrekebisha pale wanapoona aliteleza, lakini kwa wakati huu wa siasa kuelekea uchaguzi mkuu wanamuhitaji Lissu na Heche kwa kuwa sio waoga.
Kwa upande wake, Michael Makenzi, Mwenyekiti Chadema Butiama amesema anamuunga mkono John Heche kwa sababu ya misimamo yake na uadilifu wake, huku Neema Steven, Mwenyekiti Chadema Jimbo la Geita Vijijini amesema wajumbe wanatakiwa kupeleka dereva atakayeongoza jahazi kufikia nchi ya ahadi.