Kibaha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linawashikilia watu 173 kwa tuhuma mbalimbali za uhalifu ikiwemo usafirishaji wa nyara za Serikali, dawa za kulevya, wizi wa pikipiki na simu.
Watuhumiwa hao pia wanakabiliwa na tuhuma za kujihusisha na biashara haramu ya pombe ya gongo, wizi wa mifugo, pamoja na kukutwa na mafuta ya transfoma yanayodaiwa kupatikana kwa njia zisizo halali.
Hayo yamebainika kupitia taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, alipozungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Januari 5, 2025.
Kamanda Morcase amesema jeshi lhilo linaendelea na uchunguzi wa watuhumiwa hao na hatua za kisheria zitachukuliwa mara tu uchunguzi utakapokamilika.
“Wahalifu hao wamekamatwa katika msako uliofanyika mwishoni mwa Desemba 2024, tulifanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kudhibiti uhalifu na kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao,” amesema Kamanda Morcase.
Kamanda huyo ametaja baadhi ya mali zilizokamatwa pamoja na watuhumiwa hao ni pikipiki 35, simu za mkononi 13, madawati 15 yaliyoibwa kutoka Shule ya Msingi Kibadagwe katika Halmashauri ya Chalinze, na lita 900 za mafuta ya kupikia.
Vilevile, amesema walikamata mafuta ya transfoma lita 80, nyaya za kopa kilo 3,687 na nondo 35 za kujengea.
Katika hatua nyingine, Kamanda Morcase amezungumzia kukamatwa kwa madereva 24 wa magari ya IT kwa kushindwa kufuata sheria za kutosafirishaji abiria.
“Hawa madereva wa magari ya IT hawaruhusiwi kupakia abiria kisheria, lakini wamekuwa wakikiuka sheria hii kwa madhumuni ya kujiongezea kipato. Hatufumbi macho juu ya vitendo hivi kwa sababu ni hatari kwa usalama wa wananchi,” amesisitiza Kamanda Morcase.
Amesema kuwa jeshi hilo linaendelea kuchukua hatua za kudhibiti uhalifu na kuhakikisha sheria inatekelezwa ipasavyo mkoani Pwani.