Dar es Salaam. Matukio ya watu kudaiwa kutekwa yameendelea kuripotiwa nchini, baada ya jana kudaiwa kutekwa kwa mkazi wa Dar es Salaam, Dastan Mutajura eneo la Buza -Sigara.
Taarifa za kutekwa kwa Mutajura zilisambaa mtandaoni, zilidai lilitokea wakati akienda kazini akitokea nyumbani kwake eneo la Kitunda.
Kutokana na taarifa hiyo, asubuhi ya leo Jumapili, Januari 5, 2025 taarifa ya kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro ilieleza kuwa wanafuatilia kupotea kwa mtu huyo.
Mwananchi limefika eneo lilipotokea tukio hilo na kuzungumza na mashuhuda walioeleza watu wasiojulikana wakiwa na bunduki walitekeleza utekaji uliowaacha wananchi na hofu, saa nne asubuhi ya Januari 4, 2025.
Mjumbe wa eneo hilo la Kwa Mchina, Selina Geay amesema tukio la kutekwa Mutajura halikuchukua dakika tano hadi kuondoka naye, kwani lilikuwa la haraka.
“Nilikuwa nafanya usafi katika eneo langu hapa, tukaona gari nyeusi ilikuwa na mwendo wa kasi, lakini ilisimama ghafla baada ya kuvuka dimbwi la maji. Tukamuona mwanaume anashuka kwenye hiyo gari, huku nyuma yake kukiwa na gari nyingine,” amesema Selina.
Amesema baada ya mwanaume huyo kushuka “Mutajura” alianza kupiga kelele akihitaji msaada na kudai anatekwa na watu asiowajua, jambo lililowashangaza watu waliokuwepo eneo hilo.
“Wakati anapiga kelele hizo tukaona watu wengine wameshuka na bunduki na kumfuata yule baba na kumpiga mdomoni na hakuendelea kupiga kelele. Watu waliokuwa jirani na tukio katika kijiwe cha bodaboda walitaka kukimbia, lakini walitishiwa na kubaki eneo hilo,” amesema.
Selina amesema bila kuchelewa walimkamata Mutajura na kumuweka kwenye gari walilokuja nalo, kisha kuondoka kwa mwendo wa haraka, huku gari nyeusi ikiwa limebaki eneo lilipotokea tukio hilo.
Amesema baada ya watu hao kuondoka, alipiga simu kituo cha polisi Buza kwa ajili ya kuwapa taarifa kwa tukio hilo na kuachwa kwa gari ambayo imepelekwa polisi na kutolewa taarifa.
Wakiwa katika maulizo na Jeshi la Polisi, amesema alijitokeza mwanamke akitokea njia ya Kitunda yalipokuwa yametokea magari hayo na kujitambulisha kuwa ni mke wa aliyetekwa (Matujura).
“Yule mwanamke alipofika alijitambulisha kwa polisi kuwa gari lililopo katika tukio ni la mumewe, hivyo alihitaji kujua yuko wapi lakini walimwambia waende kituoni kwa ajili ya maelezo zaidi,” amesema.
Baada ya kuvutwa kwa gari hilo kupelekwa katika kituo cha polisi Buza, mkewe naye alifuata nyuma akiwa kwenye bodaboda ambayo alikwenda nayo eneo la tukio.
Amesema leo mkewe amefika tena eneo la tukio kuuliza mashuhuda namna mumewe alivyotekwa na walichokishuhudia hadi walivyoondoka naye.
“Leo mkewe amekuja tena maana jana hakutaka kuongea na mtu zaidi ya polisi, naona ili kupata usahihi wa taarifa amerudi ili kujua ilikuaje na kama walimdhuru wakati wanamchukua na sisi tumemueleza kile tulichokiona,” amesema shuhuda mwingine ambaye hakutaka jina lake liandikwe.
Amesema kilichotokea jana madereva wa bodaboda katika kijiwe lilipotoea tukio wameingiwa na uoga, baada ya kuona bunduki na kupewa amri za kutokwenda sehemu yoyote na kutofanya kitu chochote kwenye simu zao.
“Tulikuwa kama mateka jana, hakuna kutingishika hadi leo watu kukaa kijiweni wanaogopa wakiamini kuwa linaweza kutokea tukio lingine kama lile, ndiyo maana leo hakuna watu wameingia uoga wa kukaa hapa na kila wakati wanakuja watu kuulizia tukio lilivyotokea,” amesema.
Kuhusu Dastan kuishi eneo la Sigara, amesema si mkazi wa eneo hilo, hivyo anahisi atakuwa ni mkazi wa Kitunda, kwani watu wanaoshinda katika kijiwe alipotekewa wanasema gari lililoachwa si mara ya kwanza kupita eneo lao.
Matukio ya watu kudaiwa kutekwa yakizidi kuibua hofu na sintohafamu kwenye jamii, licha ya juhudi za kutafuta mwarobaini wa kadhia hiyo zikiendelea.
Hadi mwishoni mwa mwaka 2024, matukio ya kupotea ama kutekwa yaliripotiwa ikiwemo lile la Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana chama cha ACT Wazalendo, Abdul Nondo, jaribio la kutekwa kwa mfanyabiashara, Deogratius Tarimo, utekaji wa Ali Kibao yaliibua taharuki.