Unguja. Wakati sekta ya ujenzi ikitajwa kuwa miongoni mwa zinazochangia kwa kiasi kikubwa kuharibu mazingira, wahandisi wameshauriwa kujifunza matumizi ya teknolojia ya chuma ambayo ni rahisi na rafiki kwa mazingira.
Pia, wataalamu hao wametakiwa kuzingatia maeneo ya urithi wa dunia wanapoendesha shughuli zao ili yaendelee kuwa katika sura ileile.
Hayo yalibainika jana, wakati wa mkutano wa kuwaendeleza wataalamu wa usanifu, uhandisi na wakadiriaji majenzi Tanzania uliofanyika kwenye viwanja vya maonyesho Nyamanzi, Unguja.
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban alisema ipo haja sekta hizo zikabadilika kuendana na teknolojia za ujenzi za kisasa, ili kunusuru rasilimali za ardhi kutokana na sekta hiyo kuhusisha uchimbaji na ukataji wa miti na misitu.
“Sekta ambayo inahatarisha zaidi rasilimali za ardhi ikihusisha uchimbaji mchanga ni sekta ya ujenzi, sasa tukijifunza teknolojia mbalimbali, mfano ya chuma itatupa fursa ya kuwa na majengo ambayo ni rafiki kwa mazingira, hususan kuepusha ukataji wa miti. Kwa hiyo jambo hili tulipe mkazo mkubwa,” alisema.
Kuhusu maeneo ya urithi, Waziri Shaaban alisema kuna changamoto kubwa makandarasi au wasanifu majengo wanapopewa kazi kuzingatia namna ambavyo maeneo au miji inatakiwa kubaki kama ilivyo bila kuharibiwa.
“Ni muhimu sana taaluma hizi zikaangalia masuala ya uhifadhi, tunalo tatizo, hasa kwenye maeneo ya urithi, hususan eneo la Mji Mkongwe, makandarasi au wasanifu majengo wanapopewa kazi wakati hawana taaluma vipi miji ya urithi inatakiwa iwe,” alisema.
Alisema Serikali zote mbili zinazingatia maeneo ya urithi ili kuendelea kunufaika kidunia, hususan katika sekta ya utalii, kwani maeneo hayo yanapata wageni wengi wanaoenda kuyatembelea na kujifunza tamaduni.
Pia wajiendeleze kusoma kutokana na taaluma kubadilika na kuwapo na vitu vipya kila siku.
Mbunifu majengo, Danie Matondo alisema kuna changamoto ya vifaa wakati wa ukarabati, hususan katika maeneo ya Mji Mkongwe, kwani vifaa vyake ni gharama kubwa, hivyo Serikali iangalie namna ya kuwasaidia.
“Wasione majengo kama hayana maana, yametunza historia ya Taifa letu na yanavutia utalii na kuongeza uchumi katika sekta ya utalii, kwa hiyo tumekubaliana watumie ujuzi, uadilifu na uzalendo, hususan kuhifadhi majengo,” alisema.
Alisema kuna baadhi ya maeneo ya kihistoaria hayajatambuliwa, hivyo Serikali ichukue hatua kuyatangaza yahifadhiwe, yakiwamo Bagamoyo na Tabora.
Mbunifu majengo na upangaji wa miji, Zakia Nyombi alisema uhifadhi ni muhimu, utajiri wa nchi umejidhihirisha katika uhifadhi, kwa hiyo kuhakikisha katika upangaji wa miji na ubunifu wa majengo vinakwenda kuzingatia ubora na majengo yadumu muda mrefu.
Mhandisi wa Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM), Sania Muhamed alisema hawana taaluma nzuri kuhusu maeneo ya urithi wa dunia na ni muhimu kuipata.
“Nachukua taaluma hii, maana sisi KMKM ni watu ambao tunapokea miradi ya Mji Mkongwe, tuliwahi kupata zabuni lakini hatukufuata njia zinazotakiwa kufanyika,” alisema.