SIMBA imefanya unyama mwingi sana baada ya usiku wa leo kupata ushindi wa kwanza wa kihistoria katika ardhi ya Waarabu kwa kuichapa CS Sfaxien ya Tunisia kwa bao 1-0.
Bao hilo pekee la dakika ya 34 lililowekwa kimiani na Jean Charles Ahoua, liliiwezesha pia Simba kupata ushindi wa kwanza ugenini katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa msimu huu.
Simba ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi, jijini Tunis na kuifanya ifikishe pointi tisa kutokana na mechi nne ilizocheza hadi sasa katika Kundi A na kujiweka pazuri kuinasa tiketi ya kutinga robo fainali, kwani sasa inahitaji pointi tatu tu katika mechi mbili ilizonazo. Mechi hizo ni dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola itakayopigwa wikiendi hii ugenini na CS Constantine ya Algeria itakayopigwa Januari 19 jijini Dar es Salaam.
Ikicheza kwenye uwanja usio na mashabiki kutokana na wenyeji kuadhibiwa na CAF kwa kile ilichokifanya kwenye mchezo wa kwanza nyumbani dhidi ya Constantine, Simba ilitawala kwa dakika 90 ikiupiga mpira wingi, japo ilishindwa kutumia nafasi ilizotengeneza.
Licha ya wenyeji kucheza kwa nidhamu na kutumia mashambulizi ya kushtukiza, lakini ukuta mgumu wa Simba uliokuwa chini ya mabeki wa kati, Abdulrazack Hamza na Fondoh Che Malone na kipa Moussa Camara, iliufanya mchezo kuwa mtamu.
Hata hivyo, ilikuwa ni Simba iliyopata bao pekee lililofungwa kiufundi na Ahoua katika dakika ya 34 akipokea pasi tamu ya Leonel Ateba na kufumua shuti mbele ya beki wa Sfaxien na kumtungua kipa Aymen Dahmen.
Hilo lilikuwa ni bao la pili kwa Ahoua katika michuano hiyo baada ya awali kufunga dhidi ya Bravos katika ushindi wa 1-0 jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Ellie Mpanzu alianzishwa katika mchezo huo kwa mara ya kwanza katika michuano ya CAF na alitumika kwa dakika 77 kabla ya kutolewa kumpisha Debora Mavambo.
Kwa muda aliotumika uwanjani, Mpanzu aliisumbua ngome ya Sfaxien ambayo imepoteza mechi ya nne mfululizo za makundi na kubaki mkiani ikiwa haina pointi.
Alitengeneza nafasi za mabao katika kipindi cha kwanza zilizopotezwa na Ateba, Kibu Denis na Ahoua, huku lingine alikikosa mwenyewe kwa kuokolewa na beki wa wenyeji.
Mara ya mwisho wa Simba kutakata katika ardhi ya Waarabu ilikuwa 2003 ilipoing’oa kwa penalti waliokuwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa msimu huo, Zamalek yua Misri.
Katika mchezo wa jana Simba ilicheza soka tamu na kasi, ikiwa haina presha kubwa kama ingekuwa na nyomi la mashabiki wa Sfaxien.
Kibu, Mpanzu, Ateba na mabeki wa pembeni, Shomary Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ waliinyima amani ngome ya Sfaxien ambayo ilinusurika kupigiwa penalti kabla ya mapumziko baada ya beki wa timu hiyo kuonekana kuunawa mpira akiwa ndani ya lango la timu hiyo, lakini mwamuzi Daoudi Gueye kutoka Senegal alimeza filimbi licha ya wachezaji wa Simba kulalamika.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids aliendelea kuonyesha ni kocha aina gani kutokana na kuingia uwanjani na mbinu kali akiwatumia viungo wakabaji wawili Fabrice Ngoma, na Yusuf Kagoma, huku mbele akiwa na viungo washambuliaji wenye kasi, Mpanzu, Kibu na Ahoua ambao walicheza kwa nidhamu, licha ya umakini mdogo katika umaliziaji, kabla ya kumtoa Kibu na Mpanzu na kuwaingiza Debora Mavambo na beki Chamou Karaboue kisha kumtoa Ateba na kumuingiza Steven Mukwala dakika ya 90 na kuituliza timu.
Mbinu ya kuanza na wachezaji hao ilionekana kuibeba Simba, huku kipa Camara akiendelea kuonyesha ubora wake kikosini kwa kuokoa michomo michache ya Sfaxien hasa kipindi cha pili.
SFAXIEN: Dahmen, Traore/Winley, Baccar, Harabi, Ayouni, Conte, Becha/Ben Ali, Sekkouhi, Hassen/Haboubi, Cristo/Hmidi na Zaidi/Habbassi
SIMBA: Camara, Kapombe, Tshabalala, Hamza, Che Malone, Kagoma, Kibu/Karaboue, Ngoma, Ateba/Mukwala, Ahoua na Mpanzu/Debora.