SIMBA jana usiku ilifanya makubwa huko Tunisia ikiipasua CS Sfaxien kwa bao 1-0 la kiungo Jean Charles Ahoua, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids akianza mapema kuisoma Bravos do Maquis ya Angola watakayovaana nayo wikiendi hii, akilenga kufuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika akiwa ugenini Angola huku akiwa na mechi moja mkononi. Andaeni suti.
Simba na Bravos zitavaana Jumapili hii kwenye Uwanja wa Taifa wa Novemba 11, uliopo Talatona, jirani kabisa na jiji la Luanda ikiwa ni mchezo wa marudiano na wa raundi ya tano wa Kundi A.
Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Novemba 27, 2024 Simba ilishinda Kwa Mkapa kwa bao 1-0 la penalti iliyopigwa na kiungo mshambuliaji, Jean Charles Ahoua, kitu ambacho kocha Fadlu anaamini mchezo huo wa marudiano hautakuwa rahisi hasa kutokana na rekodi za Bravos ikiwa nyumbani.
Timu hiyo katika mechi nne za CAF za nyumbani zikiwamo mbili za raundi ya awali na mbili za makundi, haijapoteza hata moja, ikishinda tatu zote kwa mabao matatu na moja tu ilishinda kwa bao 1-0, kitu ambacho inaelezwa Fadlu amelazimika kuanza kuisoma upya timu hiyo kabla ya kuifuata wikiendi hii.
Katika mechi ya raundi ya kwanza dhidi ya Coastal Union, timu hiyo ya Angola ilishinda 3-0 kisha ikalazimisha suluhu ugenini na kufuzu raundi ya pili ilipokutana na FC Lupopo ya DR Congo na kushinda 1-0 nyumbani, kisha ikaenda kupata ushindi wa 2-1 ugenini na kutinga makundi.
Kwa hatua hiyo ya makundi, Bravos ilizinyuka CS Constantine ya Algeria na Sfaxien kila moja mabao 3-2 na sasa inajiandaa kuikaribisha Simba baada ya jana usiku kuwa ugenini kurudiana na Waalgeria kisha itasaliwa mechi ya mwisho dhidi ya vibonde Sfaxien inayoburuza mkia kundini.
Taarifa kutoka ndani ya kambi ya Simba, zinasema Fadlu hata wakati akiendelea na maandalizi ya mchezo wa jana dhidi ya Sfaxien alikuwa akipekua pia faili la Bravos kwa lengo la kuanza kuisoma mapema kabla ya kuifuata Angola, hasa kwa rekodi ilizonazo za kutopoteza mechi yoyote ya CAF nyumbani.
“Fadlu hataki kuchelewa kabisa kwa mchezo ujao, kwani alikuwa akiwaelekeza wasaidizi wake, hasa video analysts wa timu hiyo kutaka kujua Bravos inachezaje ikiwa nyumbani, kwani ameshtushwa na matokeo iliyonayo msimu huu katika Kombe la Shirikisho na hata kwa Ligi Kuu ya Angola,” kilisema chanzo hicho.
Katika Ligi ya Girabola, Bravos imecheza mechi saba nyumbani na kupoteza moja tu, ikitoka sare nne na kushinda mbili, lakini ikiwa na udhaifu wa kuruhusu mabao kama ilivyo hata katika mechi za CAF japo haijapoteza, kwani yenyewe imefunga saba na kufungwa sita ikiwa nyumbani.
Pia ni mechi mbili tu za raundi ya awali za CAF msimu huu, ndio haikuruhusu bao nyumbani dhidi ya Coastal na FC Lupopo, ila kwa makundi imeruhusu katika mechi zote mbili za awali mbela ya Constantine na Sfaxien, kuonyesha inafungika kirahisi kwani ilishinda 3-2 kila moja ikiwa na maana imeruhusu manne.
Taarifa za kwamba Bravos inaruhusu mabao ikiwa nyumbani hata kama inashinda, ndio iliyomsukuma Fadlu kuanza kuisoma ili kuizuia isifunge na pia kutafuta dawa ya kutumia udhaifu walionao kuinyamazisha Jumapili, baada ya kuifunga kwa tabu zilipokutana Kwa Mkapa.
“Naamini baada ya mchezo wa leo (jana) usiku, ataanza kazi ya kuisoma kwa kina kabla ya kuwapa madini nyota wa timu hiyo ili Angola mambo yawe mepesi kabla hata hatujamalizana na Constantine katika mchezo wa mwisho wa kundi hilo,” chanzo hicho kilifafanua.
Mapema Fadlu, raia wa Afrika Kusini, alikaririwa akitamba anataka kufanya vizuri katika mechi zote zilizosalia kundini ili kuivusha timu kwenda robo fainali, licha ya kundi hilo kuonekana kuwa gumu zaidi hadi sasa kutokana na timu kutotofautiana pointi nyingi ukiiondoa Sfaxien ambayo haina pointi baada ya kipigo cha jana nyumbani kutoka kwa Simba yenye pointi tisa sasa.