GET Program ambayo inapitia ukata itawapa mkono wa kwaheri nyota tisa ambao itashindwa kuendelea nao katika dirisha hili dogo la uhamisho kutokana na changamoto ya kifedha.
Wachezaji hao ni Koku Kipanga, Diana Mnally, Zubeda Mgunda waliotimkia Yanga Princess, Janeth Nyagali, Anandez Lazaro, Zainabu Ally, Nasma Manduta, Lucy Mrema na Elizabeth Nashon.
Chanzo kiliiambia Mwanaspoti kuwa timu hiyo inapitia changamoto ya ukata ikiwamo kushindwa kuwalipa mishahara wachezaji na kumudu mahitaji ya timu.
Aliongeza kuwa sababu ya kuwapa mkono wa kwaheri wachezaji ni baadhi yao kuomba kuvunjiwa mikataba na kutafuta changamoto sehemu nyingine na wengine ambao wamepata ofa timu kubwa.
“Michezo minne hatujacheza tunapitia kipindi kigumu, hakuna fedha za kujiendesha ndio maana tukaona wachezaji walioomba kuondoka haina haja ya kubaki nao tuwatoe na wengine tuliowauza tupate chochote ingawa bado,” kilisema chanzo hicho.
Ukiachana na wachezaji hao, aliyekuwa straika wa timu hiyo, Zainabu Mohamed ‘Dudu’ naye wiki iliyopita alijiunga na Mashujaa Queens kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba.