KOCHA wa Ceasiaa Queens, Ezekiel Chobanka amesema mipango ya timu kwa sasa ni kuhakikisha inasalia Ligi Kuu ili msimu ujao ijipange.
Timu hiyo iko nafasi ya tisa katika msimamo wa ligi hiyo ya timu 10 ikishinda mechi mbili kwenye michezo saba na kupoteza tano ikikusanya pointi sita.
Chobanka ametambulishwa hivi karibuni kama kocha mkuu wa timu hiyo akisimamia mechi mbili na zote akipoteza dhidi ya Yanga Princess 4-1 na Alliance 3-1.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chobanka alisema timu hiyo msimu huu haitaki makuu kilichobaki ni kusalia Ligi Kuu kisha kujiandaa vizuri kwa msimu ujao ikiwamo kusajili nyota wapya.
“Timu haikuwa na maandalizi mazuri mwanzoni mwa msimu, mtakumbuka pia haikuwa na kocha maalum, pia usajili haukuzingatia maeneo, kuna baadhi ya maeneo nafanya maboresho ili timu irudi kwenye mstari mzuri wa ushindani,” alisema.
“Msimu huu mipango timu ibakie Ligi kuu ili msimu ujao tujipange kwa usajili mzuri na maandalizi ya mapema na kisha turudi kwenye ushindani ila kwa sasa mapumziko ya siku 20 ni kusuka mipango ya ushindi.”
Msimu uliopita timu hiyo ilikuwa kati ya timu shindani kwenye Ligi ikiifunga Yanga Princess nyumbani na ugenini na kuikomalia JKT na Simba Queens kuruhusu mabao mengi. Hata hivyo, baada ya kocha Noah Kanyaga kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi akatimka kikosini hapo pamoja na wachezaji muhimu.