TAAWANU yazindua rasmi zoezi la ugawaji bure wa vitanda elfu 60 kwenye hospitali nchini Tanzania

Taasisi ya Taawanu Islamic Foundation chini ya Mkurugenzi wake wa Kimataifa Hajjat Zahra Dattan (zaradattani on Instagram) imezindua rasmi zoezi la ugawaji wa vitanda kwa hospitali mbalimbali hapa Nchini Tanzania lengo likiwa ni kusaidia wananchi wanaoenda maeneo hayo kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Zoezi hilo limezinduliwa katika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera ambapo limehudhuliwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkurugenzi wa Taawanu Kimataifa Hajath Zahra na Mwenyekiti wa Taawanu Taifa na Afrika kwa ujumla Sheikh Hashimu Kamugunda ambaye ndo amezindua zoezi hilo akimuwakilisha Muft wa Tanzania na amekabidhi baadhi ya vitanda ikiwa ni ishara ya uzinduzi kwa Umoja wa Maendeleo ya Wanawake wa Kiislamu Kagera (UMWAKIKA) ambavyo vitatumika kwenye kituo chao cha Afya kilichopo Kata ya Nyanga ndani ya Manispaa hiyo.

Baada ya kukabidhi vitanda hivyo na kuzindua zoezi hilo rasmi,Viongozi wa Taawanu Hajjat Zahra pamoja na Sheikh Hashimu Kamugunda wamewasihi na kuwataka wale wote watakaopata vifaa hivyo kuhakikisha wanavitunza vizuri ili viweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa ambayo ni pamoja na kuwasaidia wagonjwa sambamba na kupunguza mzigo kwa taasisi ambazo zinatoa huduma ya afya kwa wananchi.

Pia Hajjat Zahra amesema kuwa zoezi hilo litafanyika nchi nzima ambapo wataanza kwa kugawa vitanda elfu sitini na zoezi litakuwa endelevu kadri watakavyojaliwa ili waweze kuwafikia walio wengi huku akitaja gharama kitanda kimoja kuwa ni zaidi ya milioni 8 za Kitanzania.

Related Posts