Hesabu moja Kombe la Mapinduzi leo

Ushindi ndio lengo la kila timu leo wakati Zanzibar Heroes itakapocheza na Burkina Faso katika Uwanja wa Gombani, Pemba ikiwa ni muendelezo wa Kombe la Mapinduzi 2025 kuanzia saa 1:00 usiku.

Baada ya kuibuka na ushindi katika mechi ya kwanza dhidi ya Kilimanjaro Stars, Zanzibar Heroes ikipata ushindi leo, itakuwa imejihakikishia kutinga hatua ya fainali ya mashindano hayo kwani itafikisha pointi sita ambazo zitaifanya imalize katika nafasi mbili za juu.

Burkina Faso ambayo mechi ya kwanza ilitoka sare na Kenya, ikipata ushindi leo, itafikisha pointi nne na hivyo itahitaji angalau matokeo ya sare kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Kilimanjaro Stars, iweze kutinga fainali.

Zanzibar Heroes inaingia katika mechi ya leo ikimtegemea zaidi Feisal Salum ‘Fei Toto’ huku Burkina Faso ikimtegemea Aboubacar Traore, wachezaji wote wakiwa ndio waliozifungia timu zao kwenye mechi za kwanza.

Kocha wa Burkina Faso, Issa Balbone alisema timu yake ipo tayari kwa mechi dhidi ya Zanzibar Heroes.

“Hatujaanza vibaya kwani tulitoka sare katika mechi ya kwanza. Timu yangu iko fiti kwa ajili ya hii mechi,” alisema Balbone.

Kocha wa Zanzibar Heroes, Ally Mngazija alisema wanaingia kwa tahadhari kubwa dhidi ya Burkina Faso.

“Tuzungumze kweli, Burkina Faso ni timu nzuri ambayo imekuwa ikibadilika badilika. Tumeiona na tumeshajua jinsi ya kukabiliana nayo ili tupate ushindi,” alisema Mngazija.

Related Posts