Dar es Salaam. Tanzania inatarajiwa kuwaunganishia umeme watu milioni 1.2 kila mwaka kutoka 500,000 wanaounganishiwa sasa.
Kutokana na hilo, katika miaka mitano 2025/30, watu milioni 8.5 wataunganishiwa huduma hiyo nchini.
Ongezeko hilo la watakaounganishiwa umeme, litatokana na kuanza kwa utekelezaji wa Agenda300 inayolenga kufikisha nishati hiyo kwa watu milioni 300 Afrika ifikapo mwaka 2030.
Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), zimetangaza mpango wa kuhakikisha watu milioni 300 wanafikiwa na umeme Afrika ifikapo mwaka 2030.
Katika utekelezaji wa hilo, Januari 27 na 28, 2025, wakuu wa nchi za Afrika watakutana jijini Dar es Salaam kujadili kuhusu Ajenda300.
Hayo yameelezwa leo, Jumapili Januari 5, 2025 na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Innocent Luoga katika semina ya wahariri na waandishi wa habari kuelekea mkutano wa wakuu wa nchi Afrika kuhusu nishati.
Amesema nchi 14 ikiwamo Tanzania, zimechaguliwa kuwa za awali kwa ajili ya utekelezaji wa Ajenda300 na katika mkutano huo, zitasaini mkakati wa utekelezaji.
Mbali na Tanzania, amezitaja nchi nyingine ni Mali, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Ivory Coast, Burkina Faso, Chad, Liberia, Madagascar, Malawi, Mauritania, Msumbiji, Niger, Nigeria na Zambia.
Kwa sababu mkakati huo wa Ajenda300 utakapoanza kutakuwa na uwezo wa kifedha, amesema kiwango cha kuunganishia wananchi umeme kitaongezeka.
“Mpango wa kawaida wa sasa na kwa miundombinu na bajeti iliyopo, Tanzania kwa mwaka tunaunganishia umeme wananchi 500,000. Hili ndilo lengo na tumelitimiza mwaka jana na juzi,” amesema.
Kwa kuwa kutakuwa na fedha za kutosha, amesema wanatarajia kwa miaka mitano wateja milioni 13.5 watakaounganishwa umeme kwa miaka mitano.
Amesisitiza baada ya kusainiwa kwa mkakati, inatarajiwa kufikia mwaka 2030 upatikanaji wa umeme nchini, ufikie asilimia 100.
Akizungumzia katika mkutano huo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema wakuu wa nchi zaidi ya 10 wanatarajiwa kuhudhuria katika mkutano huo.
Amesema Januari 27, watakutana mawaziri hasa wa fedha, kisha Januari 28 watakutana wakuu wa nchi.
Msigwa amesema idadi ya watu wasiofikiwa na umeme Afrika ni milioni 685, hivyo Ajenda300 itapunguza karibu nusu yake.
Msigwa amefafanua hatua ya Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji inatokana na juhudi zilizofanywa na Serikali kutoa huduma ya umeme kwa wananchi.
Amesema uzalishaji wa umeme nchini kwa sasa ni Megawati 1,410 katika mashine sita za Bwawa la Umeme la Julius Nyerere.
Uzalishaji wa jumla, amesema ni megawati 3,169 kutoka vyanzo mbalimbali, huku mahitaji yakiwa takriban megawati 1,800.
Kwa sababu uzalishaji unazidi mahitaji, amesema miundombinu ya kuhakikisha usambazaji wa umeme kwenda mataifa mengine, unaendelea na ndiyo mwelekeo wa Ajenda300.
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda amesema Benki ya Dunia na AfDB ndilo chimbuko la mkutano huo.
Mkutano huo, amesema unatokana na azimio la pamoja la Benki ya Dunia na AfDB katika mkutano wa majira ya kipupwe wa WB uliofanyika Washington DC, Marekani.
Amesema Rais wa Benki ya Dunia na AfDB waliandika barua kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuomba Tanzania iwe mwenyeji.
Amezitaja sababu za Tanzania kuwa mwenyeji ni kuwepo kwa mikakati kabambe ya kuhakikisha upatikanaji umeme kwa wote.
Sababu nyingine, amesema ni kushamiri kwa diplomasia, amani, utulivu, ukarimu na uzoefu wa nchi kuendesha mikutano mikubwa.
Amesema katika mkutano huo watu 1,500 wanatarajiwa kuhudhuria katika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere.
Amesema tayari mialiko imetumwa kwa wakuu wa nchi zote za Afrika na wengine nje ya bara hilo.