Taarifa ya vifo vya watoto hao imetolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) ambalo limesema pia kuwa karibu watoto wachanga 7,700 katika eneo la Gaza lililoharibiwa na vita, wanaishi katika makazi duni kutokana na mgogoro unaoendelea kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Hamas.
Shirika la habari la Palestina WAFA liliripoti mwishoni mwa mwezi Desemba kwamba watoto wengine wanne walikufa kutokana na baridi kali. Mamia ya maelfu ya Wapalestina wamepoteza makazi yao kutokana na vita vya zaidi ya miezi 15 huko Gaza. Wale waliohamishwa wanaishi katika mahema ambayo hayawakingi mvua wala baridi.
Ndani ya muda wa saa 24 zilizopita, watu zaidi ya 20 wamearifiwa kuuawa Gaza karibu na mji wa Khan Younis na kwenye kambi za wakimbizi wa ndani za Bureij, Deir al Balah na al Nuseirat. Jeshi la Israel limesema lilishambulia maeneo zaidi ya 100 ya “magaidi” na limekuwa likiwalenga wapiganaji wa kundi la Hamas.
Soma pia: Watu 50 wauawa Gaza kufuatia mashambulizi ya Israel
Taarifa ya jeshi imeendelea kueleza kuwa kabla ya mashambulizi hayo, hatua muhimu zilichukuliwa ili kupunguza madhara kwa raia, na kwamba idara za kijeshi na kijasusi zitaendelea kupambana na makundi ya kigaidi katika Ukanda wa Gaza ili kuwalinda raia wa Israel.
Marekani yaelezea matumaini ya kufikiwa mpango wa usitishwaji mapigano
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ameonyesha matumaini kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza na kuachiliwa kwa mateka yatafikiwa hivi karibuni lakini akasisitiza kuwa huenda ikawa baada ya Rais Joe Biden kuondoka madarakani Januari 20, 2025.
Akiwa ziarani nchini Korea Kusini, Blinken amesema katika wiki mbili zilizosalia, watafanya kazi kila dakika ili kujaribu kuufanikisha mpango huo huku akiitolea wito Hamas.
“Tunaitaka Hamas ichukue maamuzi ya mwisho muhimu ili kukamilisha makubaliano hayo, na kubadilisha kabisa hali ya mateka, kuwaachilia huru. Na pia kwa watu wa Gaza na eneo zima kwa ujumla kuwaletea unafuu, kwa kuwepo fursa ya kweli ya kusonga mbele kwa mustakabali bora na salama zaidi kwa kila mtu anayehusika.”
Tangu kuanza kwa mzozo wa Gaza Oktoba 7 mwaka 2023, Blinken alifanya ziara 12 katika eneo la Mashariki ya Kati ili kujaribu kusuluhisha. Taifa lake Marekani, Misri na Qatar wamekuwa wapatanishi wakuu kwenye mzozo huu ambao umesababisha maafa makubwa.
Vyanzo: (AFP, DPA, AP)