Mtoto wa Museveni atishia kumkata kichwa Bobi Wine

Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni, amesema isingekuwa baba yake angemkata kichwa kiongozi wa upinzani nchini humo, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine.

Jenerali Kainerugaba amechapisha tamko hilo jana Jumapili, Januari 5, 2025 katika ukurasa wake X na kuibua hali ya sintofahamu.

“Kabobi (Bobi Wine) anajua kuwa mtu pekee anayemlinda kutoka kwangu ni baba yangu. Mzee asingekuwepo ningemkata kichwa leo!” ameandika.

Bobi Wine amemjibu kuwa hachukulii kiwepesi tishio la kukatwa kichwa na mkuu huyo wa jeshi, huku akisema hatokubali vitisho vya utawala wa watu waoga.

“Tishio la mtoto wa Museveni (ambaye pia anaongoza Jeshi la Uganda) la kunikata kichwa si jambo ninalolichukulia kirahisi, ikizingatiwa kwamba wengi wameuawa na yeye na baba yake, na kwa kuzingatia majaribio yao kadhaa ya kuniua. Nakataa kutishwa na utawala wa watu waoga. Ulimwengu unatazama,” amemjibu Bobi Wine.

Aidha, Muhoozi ameendelea kumkataza kiongozi huyo wa upinzani kutamka jina lake au familia yake na endapo atafanya hivyo tena atampiga pamoja na walioko nyuma yake.

“Kabobi, nitakupiga na yeyote utakayejificha nyuma yake! Tamka tena jina langu au la familia yangu nitakuvunja meno yako yote hayo ya nyani,” ameandika Jenerali Muhoozi.

Kiongozi huyo wa jeshi mara kwa mara amekuwa akitoa machapisho yenye utata kwenye mitandao ya kijamii, ikiwa ni pamoja na tishio la 2022 la kutaka kuivamia nchi jirani ya Kenya.

Machapisho hayo kuhusu Bobi Wine ambaye alimaliza wa pili nyuma ya Museveni katika uchaguzi wa urais wa 2021, yameendeleza misukosuko ya kiongozi huyo wa upinzani ambaye mara kadhaa amekuwa akikamatwa kutokana na ushawishi wake nchini humo.

Related Posts