Morogoro. Kituo cha mabasi Msamvu mkoani Morogoro kuna ongezeko kubwa la abiria, wakiwamo wanafunzi wanaorejea shuleni baada ya likizo kumalizika.
Pia nauli zimepaa, hali inayotajwa kuchangiwa na uchache wa magari.
Mwananchi Digital imefika kituoni hapo leo Jumatatu, Januari 6, 2025 na kuzungumza na baadhi ya abiria akiwamo Magdalena Olomi, anayesema kumekuwa na tabia ya wasafirishaji kupandisha nauli kiholela, hasa nyakati za sikukuu na kipindi cha shule kufunguliwa.
“Unakuta nauli ya kutoka Morogoro kwenda Dar es Salaam ni Sh13,000 kwa magari ya kawaida, lakini kipindi hiki wanapandisha mpaka Sh20,000,” amelalamika Olomi.
Amesema kutokana na uwingi wa abiria katika kipindi hiki, madereva na utingo wa mabasi hujichukulia uamuzi wa kupandisha nauli bila kufuata utaratibu.
“Mbaya zaidi, tunabebwa kwenye mabasi yaliyojaa kupita kiasi na hizi ajali zinazotokea zinatufanya tusafiri tukiwa na hofu. Naomba mamlaka husika ziwe macho zaidi katika kipindi hiki,” amesema msafiri huyo.
Kwa upande wake, Halidi Omary, dereva wa mmoja wa mabasi yanayofanya safari kati ya Morogoro na Arusha, amesema kupanda kwa nauli kunatoka na wingi wa abiria, baadhi ya madereva na makondakta hutumia fursa hiyo kujitengenezea kipato.
“Pia wapo wachache (madereva, makondakta) wanaopandisha bei ya nauli wakidai wanafidia gharama za mafuta, lakini wengine ni ushindani tu katika sekta yetu hasa kipindi hiki cha mwanzoni wa mwaka,” amesema Omary.
Akijibu changamoto hizo, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Andrew Mlacha amesema licha ya ongezeko la abiria katika stendi ya Msamvu, maofisa wa mamlaka hiyo wameendelea kusimamia shughuli za usafirishaji na kuhakikisha abiria wanalipa nauli iliyopangwa na mamlaka.
Pia amewataka abiria kutoingia kwenye mabasi kabla ya kukata tiketi, huku akisisitiza matumizi ya tiketi za kielektroniki kama suluhisho la kudhibiti upandishwaji wa nauli kiholela.