Tarime. Serikali inatarajia kutoa mafunzo kwa walimu zaidi ya 9,000 wa masomo ya sayansi, hisabati na Tekonolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa shule za sekondari nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha elimu.
Idadi hiyo inatarajiwa kufikiwa Machi mwaka huu, ikiwa ni awamu ya kwanza ya mpango huo kabla ya awamu nyingine, ili kuhakikisha walimu wote wa masomo hayo wanapata mafunzo hayo.
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatatu, Januari 6, 2025, mjini Tarime na Mkurugenzi wa Walimu wa Sekondari kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Haruna Mageni, wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa walimu wa mikoa ya Mara na Simiyu.
Dk Mageni amesema mafunzo hayo yatazingatia lugha ya kufundishia, ili kuwawezesha walimu kuwasilisha mada zao kwa ufasaha na kueleweka kwa urahisi na wanafunzi.
“Changamoto mojawapo katika ufundishaji wa masomo haya ni lugha. Baadhi ya walimu hujaribu kutafsiri maneno ya kisayansi bila usahihi, hali inayosababisha kupotosha maana. Mafunzo haya yanalenga kuwajengea uwezo wa lugha ya kufundishia sayansi, hisabati na Tehama,” amesema Dk Mageni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia Elimu ya Sekondari kutoka Tamisemi, Hadija Mcheka amesema mafunzo hayo yanalenga kuboresha mbinu za ufundishaji na kusaidia kuongeza idadi ya wataalamu wa sayansi, hisabati na Tehama nchini.
“Bado kuna upungufu mkubwa wa wataalamu katika maeneo haya na mafunzo haya ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha tunazalisha wataalamu wa kutosha kwa maendeleo ya nchi yetu,” amesema Hadija.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia Elimu, Dk Wilson Mahera amesema Serikali imejizatiti kuboresha elimu, hasa masomo ya sayansi, hisabati na Tehama kama njia ya kufanikisha maendeleo endelevu.
“Ili nchi iendelee, lazima tuwekeze kwenye sayansi, teknolojia na ubunifu, huku tukizingatia msingi imara wa hisabati. Mafunzo haya ni sehemu ya kuhakikisha walimu wanapata stadi bora za kufundisha,” amesema Dk Mahera.
Aidha, ameagiza kufanyike utafiti ili kupima matokeo ya mafunzo hayo kwa wanafunzi na kubaini kama yana tija iliyokusudiwa.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia na tayari shule mpya 180 za sekondari zimejengwa, zikiwamo 26 maalumu za wasichana katika kila mkoa.
“Kupitia mradi wa SEQUIP, tunatarajia kutoa mafunzo endelevu kwa walimu zaidi ya 40,000 kwa masomo yote, lengo likiwa ni kuhakikisha walimu wanakuwa mahiri na wanafunzi wanapata elimu bora,” amesema Dk Mahera.
Naye Dk Emmanuel Sulungu kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), mmoja wa wakufunzi, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea walimu uwezo wa kutumia mbinu shirikishi na vifaa vinavyopatikana katika mazingira yao.
“Tunalenga mafunzo kwa vitendo zaidi ili walimu wahamie kwenye mbinu za ufundishaji shirikishi, badala ya kuendelea kutumia nadharia pekee,” amesema Dk Sulungu.
Mmoja wa walimu washiriki, Eliud Myovela amesema mafunzo hayo yana mchango mkubwa katika kuboresha utendaji wao wa kazi na anaamini ufaulu wa wanafunzi utaongezeka.
“Changamoto zipo, ikiwemo idadi kubwa ya wanafunzi darasani, lakini kupitia Tehama na mbinu mpya tunazofundishwa, naamini tutapunguza changamoto hizo,” amesema mwalimu Myovela.