JUKWAA LA TATU LA WAKUU WA TAASISI ZA SMT/SMZ LAFUNGULIWA ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amesema Kongamano la Jukwaa la Wakuu wa Taasisi za SMT na SMZ lina lengo la kuwakutanisha Wakuu wa Taasisi za hizo katika kujenga mashirikiano ya kiutendaji katika kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi katika sekta wanazozisimamia.

Ameyasema hayo wakati wa Ufunguzi wa Jukwaa la tatu (3) la wakuu wa Taasisi za (SMT na SMZ) lililofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za kutimia miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Amesema kuwa jukwaa la Wakuu wa Taasisi limeweka vipaumbele muhimu katika kutekeleza shughuli mbali mbali ikiwemo kuimarisha ushirikiano kwa ajili ya kuongeza tija, ufanisi, fursa, ujuzi, maarifa mahususi, kuimarisha ulezi (Mentorship) pamoja na ushauri nasihi miongoni mwa viongozi wa umma na taasisi mbali mbali.


Mhe Hemed amesema niwazi kuwa kwa kuzingatia malengo hayo, Jukwaa la Wakuu wa Taasisi litaendeleza jitihada za Serikali ya awamu ya Sita (6) ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na awamu ya nane (8) ya Zanzibar ikiwa ni kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kutimiza malengo ya Taasisi wanazozisimamia na kuchochea utoaji wa huduma na ukuaji wa uchumi nchini.

Aidha Makamu wa pili wa Rais ametoa rai kwa Viongozi wa Taasisi za Umma na Watanzania kwa ujumla, kulitumia Jukwaa hilo vizuri katika kujifunza, kubadilishana uzoefu na kutatua changamoto zilizopo katika utoaji wa huduma kwenye maeneo yao kwa kuzingatia suala zima la utawala bora na matumizi sahihi ya rasilimali za umma ambapo utekelezaji wa mikakati mbalimbali itakayotokana na Jukwaa hilo itachangia kuleta mafaniko mazuri zaidi katika kipindi kufupi kijacho.

Sambamba na hayo amewataka Wakuu wa Taasisi nchini kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Viongozi waakuu wa Nchi ikiwa ni pamoja na kutekeleza kwa vitendo Falsafa ya R nne (4R) ambazo zimejikita katika masuala ya Maridhiano (Reconciliation), Ustahimilivu (Resilience), Mabadiliko (Reforms) na kujenga upya Taifa (Rebuiliding) ili kujenga amani na utulivu wa kudumu nchini na kuleta maendeleo endelevu kwa uchumi wa nchi yetu.

Nae Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe. Omar Said Shaaban amesema lengo la kufanyika Jukwaa la Tatu (3) la wakuu wa Taasisi za SMT na SMZ ni kutoa fursa kwa wakuu wa Taasisi kuweza kujadili maono na maelekezo ya Viongozi wakuu wa nchi katika kuwaletea wanachi maendeleo.

Waziri Shaaban amesema Jukwaa hilo ni kiungo muhimu na msaada mkubwa katika kuhakikisha usimamiaji na upangaji wa mikakati mbali mbali ya kimaendeleo pamoja na kuzitatua changamoto mbali mbali ili kuboresha huduma katika jamii ikiwa ni miongoni mwa fikra na falsafa za waasisi wa mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Ameihakikishia Serikali kuwa Jukwa la Wakuu wa Taasisi litaendela kutoa ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja kwa pande zote mbili za Muungano kwa ustawi bora wa Taifa na jamii kwa ujumla ili kufika Zanzibar ya Maendeleo.

Mapema mwenyekiti wa TANTRED Tanzania Bi. Latifa Mohamed Khamis amesema kuwa malengo makuu ya jukwaa hilo ni kutoa fursa kwa wajumbe kujifunza mambo mbali mbali yatakayo wajengea uzoefu wenye kufika malengo ya taasisi zao na Taifa kwa ujumla.

Amesema kuwa jukwaa hilo limekuwa na mtazamo wa kukuza uhusiano uliopo baina ya viongozi wa taasisi za SMT na SMZ wenye lengo la kurahisisha utendaji kwazi wenye kuleta maendeleo na faida kwa wananchi wa pande zote mbili za muungano, pamoja na kuyafanya Mashirika kuwa Imara katika kutekeleza majukumu yao ya kuliletea Taifa Maendeleo

Makami wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Wakuu wa Taasisi mbali mbali za SMT na SMZ wakati wa Ufunguzi wa Jukwaa la tatu (3) la Wakuu wa Taasisi za (SMT na SMZ) lililofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege jijini Zanzibar ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za kutimia miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar


Related Posts