Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amemvaa mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo akidai haudhurii vikao vinavyojadili maendeleo ya mkoa huo, badala yake anasubiria viongozi wa kitaifa ili kueleza changamoto.
Tukio hilo limetokea leo Jumatatu, Januari 6, 2025 eneo la Ilboru katika ziara ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega aliyekuwa akikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Mianzini- Olemringaringa- Sambasha- Tumbolo yenye urefu wa kilomita 18, inayojengwa kwa Sh 23 bilioni.
Katika shughuli hiyo, mbali na Ulega pia walikuwepo watendaji mbalimbali wa Serikali na wananchi.
Awali, Gambo amesema amefika eneo hilo kwa sababu ni barabara inayohusu jimbo hilo, akianza kwa kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna Serikali inavyotekeleza miradi ya barabara za ndani zinazotekelezwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijini (Tarura).
“Serikali inafanya kazi kubwa ya kujenga barabara za lami ndani ya jiji la Arusha, ikiwemo ya Mianzini – Ngaramtoni inayotekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads). Tunakupongeza kwa kuanza na barabara hii.
“Tukuombe isiwe yale maombi ya mbunge mwenzangu ya kulipa fidia tu na kuongeza kipande kingine, lakini barabara hii utusaidie tupate na taa. Ombi jingine ni barabara ya kona ya Kiseria kule Mushono itakayounganisha na Bypass ili kupunguza foleni kuelekea kwenye mashindano ya Afcon 2027,” amesema.
Kwa mujibu wa Gambo aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa huo, katika barabara hiyo Tanroads wamejenga kilomita moja na mwaka huu wa fedha hawajaitengea bajeti, licha ya kupelekewa maombi maalumu na kuahidiwa kwamba itatekelezwa.
“Ombi langu lingine ni barabara ya Arusha Kibaya hadi Kongwa ambayo Jiji la Arusha tungepata kilomita 27, lakini toka mwaka 2022 hatujamuona mkandarasi. Ningependa utumie fursa hii utueleze zile kilomita 27 kwa ajili ya Afcon Serikali ina mpango gani wa kuziweka vizuri?” amehoji Gambo.
Baada ya Gambo kueleza hayo, mshehereshaji alimpatia Makonda kipaza sauti ili kuzungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Ulega, ambapo amesema kulikuwa na vikao vingi vyenye ajenda ya barabara na cha mwisho cha bodi ya barabara kiliazimia kumuomba Ulega kufika mkoani Arusha.
“Nimefurahi kumsikia Gambo ambaye kwa sasa kutamka jina la Makonda anapata tabu sana, lakini mimi ndiye mkuu wake wa mkoa. Hata hapa amekuwa na kigugumizi, mwanzoni alikuwa anasema ananenepa kwa sababu ya Makonda, sasa kulitamka limekuwa gumu kwa sababu napiga spana mtu yeyote yule ili mambo yaende.
“Nimsaidie waziri (Ulega) hoja alizozisema hapa, Gambo kwenye vikao hashiriki na huu ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu kumsubiri kiongozi kwenye public (umma) ili umvizie upachike mambo,” amesema Makonda.
Makonda amesema mtu akienda kwenye vikao atapata majibu na kwamba huwezi kuwa kiongozi, kisha unasubiri kiongozi mkubwa anayekwenda mahali fulani na wewe unakwenda na kumpachikia neno,” amesema na kuongeza;
“Hebu fikiria kama mtani wangu (Ulega) hapa angekuwa hajajua vizuri si angeanza kunong’onezana na watendaji wake kwamba ilikuwaje. Viongozi hawa ni watu wenye heshima, njoo kwenye vikao na jenga hoja.
“Tumeshapewa msimamo wa Serikali barabara ile inakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami na Waziri wa Ujenzi (Ulega) amesema. Sasa Gambo anataka kuja kusemea huku. Uwe unahudhuria vikao, mimi sipendi mtu hahudhurii vikao halafu anasubiri kwenye public (umma) anaanza kumchomekea kiongozi maneno.”
“Ooh tupe leo kauli? Kauli ni kwamba nenda kwenye vikao,” amesema Makonda huku akishangiliwa na wananchi wa Ilboru wilayani Arumeru.
Makonda ametolea mfano wa suala jingine lililozungumziwa na Gambo kuwa ni changamoto la taa za barabarani ambalo Waziri Ulega ameshalitolea ufafanuzi kwenye kikao cha ndani kilichofanyika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa mapema leo Jumatatu, Januari 6, 2025.
“Msitafute umaarufu wa kijinga wa kutaka huruma ya umma hapa, wakati wewe ni kiongozi na mimi bahati mbaya nimenyooka. Tunataka tuweke heshima ya viongozi wetu, ukihudhuria kwenye kikao unajenga hoja, mnatoka wote na sauti moja.
“Gambo ungehudhuria kwenye vikao, haya yote usingeuliza hadharani ili uonekane unatetea wananchi, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inatetea kila mwananchi na viongozi waliopo serikalini ni jukumu lao,” amesema.
Makonda amesema mbunge wa Arumeru Magharibi, Noah Lembris ameomba fedha na kushukuru, akisema ndani ya Arusha akiwepo viongozi wanapaswa kuzungumza jambo ambalo limeshapatiwa mwelekeo kwenye vikao vya ndani.
Awakutanisha mawaziri Ulega, Dk Mwigulu
Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na Ulega walikutana mkoani Arusha mapema leo kuhudhuria kikao cha bodi ya barabara mkoani humo na kuahidi kutekeleza kikamilifu maombi ya Makonda ya kuzijenga na kukarabati barabara jijini humo, ili kuchagiza uchumi na kukuza sekta ya utalii.
Akiwakaribisha mawaziri hao walioambatana watendaji wao, Makonda ameeleza kuhusu ubovu wa barabara za Arusha akiwaomba kuharakisha ujenzi na maboresho yake kutokana na umuhimu wa barabara hizo katika kukuza uchumi.
Katika maelezo yake, Dk Mwigulu ameahidi Serikali kuharakisha utoaji wa fedha za ujenzi na kuziweka baadhi ya barabara kwenye bajeti ijayo, huku Ulega akiagiza kuanza mara moja kwa upembuzi wa baadhi ya barabara pamoja na kufungwa taa zinazotumia nishati jua.