Vijana wanne kati ya 29 ‘waliotekwa’ Kenya wapatikana

Nairobi. Tovuti ya Daily Nation imeripoti kuwa vijana wanne kati ya 29 walioripotiwa kutekwa na watu wasiojulikana nchini Kenya, wamepatikana wakiwa hai huku familia zao zikithibitisha.

Vijana hao wanaotajwa kuwa wakosoaji wa Serikali ya awamu ya tano ya nchi hiyo, walianza kutoweka mwishoni mwa mwaka 2024, jambo lililosababisha baadhi ya Wakenya kuandaa maandamano kuitaka Serikali iwarudishe.

Vijana hao waliopatikana leo Jumatatu, Januari 6, 2025 ni pamoja na Billy Munyiri Mwangi (24), Peter Muteti (22), Bernard Kavuli na Ronny Kiplagat.

Kabla ya kupatikana kwa vijana hao, leo raia wa Kenya walipanga kufanya maandamano katika njia zote za jijini Nairobi, kuishinikiza Serikali kuwaachia huru vijana hao.

Billy Munyiri Mwangi, mwanafunzi wa chuo kikuu amepatikana leo asubuhi katika Kaunti ya Embu, huku Ronny Kiplangat akipatikana katika Kaunti Machakos.

Kwa upande wake, kijana Peter Muteti, aliyetekwa nyara na watu wasiojulikana huko Uthiru Desemba 21, 2024, amepatikana leo katikati ya Jiji la Nairobi.

Naye, Bernard Kavuli, mbunifu wa maudhui mtandaoni, familia yake imethibitisha kuwa amepatika katika eneo la Kitale.

Kwa upande mwingine, Kiplangat aliyetoweka baada ya kuhudhuria ibada Desemba 25, 2024, amepatikana leo, huku akisema kuwa alitupwa Kaunti ya Machakos.

Related Posts