KIKOSI cha Singida Black Stars kimerejea mazoezini na leo kinatarajia kwenda Arusha kwa ajili ya kuweka kambi ya mwezi mmoja kujiweka fiti na michuano iliyopo mbele ikiwemo Ligi Kuu Bara inayotarajiwa kuendelea Machi Mosi, mwaka huu.
Wakati huohuo mshambuliaji Jonathan Sowah aliyesajiliwa na timu hiyo dirisha dogo msimu huu, anatarajiwa kuungana nayo kwa ajili ya maandalizi ya kumalizia msimu.
Leo Jumatatu, Singida Black Stars ilianza mazoezi chini ya kocha mkuu Hamdi Miloud ambaye ameomba kuingia kambini mapema ili kuijenga kutokana na kufika ikiwa katikati ya msimu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza alisema: “Ni kweli ni mapema sana kuingia kambini kutokana na ligi kusimama kwa muda mrefu, lakini kocha ameomba iwe hivyo ili kujenga kikosi chake muda huu ambao timu nyingine zimepumzika.
“Kutokana na hilo, tayari timu imeanza mazoezi na kesho (leo Jumanne) inaanza safari ya kwenda Arusha kwa ajili ya kambi.
“Mbali na timu kuingia kambini pia kutakuwa na ugeni wa mshambuliaji wetu Sowah kujiunga na timu tukiwa Arusha tayari kuanza kuitumikia timu sambamba na Hernest Malonga ambaye alikuwa Coastal Union kwa mkopo hivi sasa amerejea kikosini, atakuwa sehemu ya wachezaji watakaosafiri.”
Alisema Miloud licha ya kutaka kuwahi kuingia kambini ili kumfahamu mchezaji mmoja mmoja aina ya uchezaji wake na kutengeneza kikosi cha kwanza, ameomba mechi tatu hadi nne za kirafiki jambo wanaloshughulikia.
Singida Black Stars ipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.