CHUO cha Furahika Education College kilicho chini ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kimewaasa wakuu wa vyuo vyote nchini kuwa na Walimu wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Hayo ameyasema Mkuu wa chuo cha Furahika Education College Dkt. David Msuya wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Januari, 06, 2025. Amesema ili kuzingatia utawala bora na haki ya kusoma ya kila mtanzania miundombinu ya mahali pa kutoa elimu yanatakiwa yafikike kwa kila mmoja.
“Msiweke madarasa yenye ngazi kwaajili ya watu wenye ulemavu hasa ya wale wanaotambaa au wanaotembea kwa njia ya baiskeli, wanashindwa kuingia darasani kwa sababu ya madarsa mengi yamekuwa na ngazi” Amesema Dkt. Msuya
Amesema serikali na taasisi nyingine zinapoandaa miradi ya elimu kuzingatia kujenga miundombinu itakayowawezesha walemavu kuitumia.
Amesema kuwa vyuo viwe na walimu wa lugha za alama ili kuwatendea haki watu wenye ulemavu kwenye vyuo na kuwafanya walemavu wote kupata elimu sawa na wanafunzi wengine ambao hawana ulemavu.
“Niipongeze wizara ya elimu imejitahidi sana kwani inayowalimu wengi wanaofundisha lugha za alama, 2025 Vyuo tubadilike tutafute walimu, wawepo kila idara ili tutimize ndoto za serikali za awamu ya sita kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani, nia yake ni njema sana lakini taasisi hizi za elimu tunatakiwa tujiongeze sisi wenyewe kuona kwamba tunawainua watu wenye mahitaji maalumu.” Amesema
Amesema kuwa Chuo Chake wamefanikiwa kupata walimu wa watu wenye ulemavu wawili, pia amewaomba vyuo vingine walifanye jambo hili ili watanzania wenye ulemavu wawe na haki sawa kama walivyo wengine kwa kupata elimu na ujuzi.
Pia amesema kuanzi Aprili, 2025 katika chuo hicho wanatarajia kuanzisha fani ya ushonaji viatu pamoja na kazi ya uhudumu kwenye magari kwani kunawatu wanausafiri wa mabasi lakini hakuna wahudumu.
Pia amesisitiza kuwa soko la ajira lisichague aina ya watu, wenye ulemavu na wasio na ulemavu kwaajili ya kufanya kazi, waajili watu wote.
“Ulemavu unaweza kumkuta mtu yeyote kwahiyo soko la ajira lisichague ili kila mmoja anufaike na mirafi mbalimbali inayoanzishwa na serikali.” Amesema Dkt. Msuya.
“Ili kupunguza ukatili na tutende haki pande zote mbili tutende haki kwa walemavu wa mikono, wa miguu, macho na wasio sikia…. Wanahaki ya kupata mafunzo ya veta ili watimize malengo yao na tujiongeze kubadilishane ujuzi kutoka vyuo tofauti tofauti.” Amesema Dkt. Msuya
Licha ya hayo Dkt. Msuya pia amewakaribisha Watoto wote waliopo mtaani, waliofeli darasa la Saba na kidato cha nne kuanzia mwaka 2022 mpaka sasa kujiunga na chuo hicho kwani mpaka sasa kinanafasi 400 za kujiunga.
Na fomu za usajili zinapatikana katika tovuti ya chuo hicho ya www.furahika.co.tz.
Wanafunzi wote kutoka mikoa yote ya Tanzania bara na visiwani wanakaribishwa kujiunga na chuo hicho kwani elimu inayotolewa ni bure na haina gharama yeyote na baada ya kuhitimu katika chuo hicho watatafutiwa kazi kwani chuo hicho kinamikakati ya kufuatilia wahitimu.