Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema Jukwaa la Wakuu wa Taasisi za Serikali za Tanzania Bara na Visiwani (SMT na SMZ) limeweka vipaumbele vya kuimarisha ushirikiano.
Abdulla amesema hayo leo Jumatatu Januari 6 2025, wakati wa ufunguzi wa jukwaa la tatu la SMT na SMZ lililofanyika Unguja ikiwa ni mwendelezo wa shamrashamra za kutimia miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema jukwaa hilo linalenga kuongeza tija, ufanisi, fursa, ujuzi, maarifa na kuimarisha ulezi miongoni mwa viongozi wa umma na taasisi mbalimbali.
“Ni wazi kuwa, kwa kuzingatia malengo hayo, jukwaa la wakuu wa taasisi litaendeleza jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Awamu ya Nane ya Zanzibar ikiwamo kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kutimiza malengo,” amesema Abdulla.
Ametoa rai kwa viongozi wa taasisi za umma na Watanzania, kulitumia jukwaa hilo vizuri katika kujifunza, kubadilishana uzoefu na kutatua changamoto zilizopo katika utoaji wa huduma kwenye maeneo yao.
Pia, amewataka kuzingatia suala zima la utawala bora na matumizi sahihi ya rasilimali za umma ili kuleta mafaniko mazuri katika kipindi kufupi kijacho.
Pia, amewataka wakuu wa taasisi hizo kuunga mkono jitihada zinazofanywa na vongozi wakuu wa nchi ikiwamo kutekeleza kwa vitendo falsafa ya R4.
“R4 zimejikita katika maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na kujenga upya Taifa ili kujenga amani na utulivu wa kudumu nchini na kuleta maendeleo endelevu kwa uchumi wa nchi yetu,” amesema Abdulla.
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban amesema lengo kuu ni kutoa fursa kwa wakuu wa taasisi kujadili maono na maelekezo ya viongozi wakuu wa nchi katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Waziri Shaaban amesema jukwaa hilo ni kiungo muhimu na msaada katika kuhakikisha usimamiaji na upangaji wa mikakati ya maendeleo ili kuboresha huduma katika jamii.
Ameihakikishia Serikali kuwa, jukwaa hilo litaendelea kutoa ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja kwa pande zote mbili za muungano kwa ustawi bora wa Taifa na jamii kwa jumla ili kufika Zanzibar ya maendeleo.
Awali, Mwenyekiti wa jukwaa la taasisi za SMT na SMZ na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa Mohamed Khamis amesema malengo makuu ya jukwaa hilo ni kutoa fursa kwa wajumbe kujifunza mambo yatakayowajengea uzoefu.
Amesema jukwaa hilo limekuwa na mtazamo wa kukuza uhusiano uliopo baina ya viongozi wa taasisi za SMT na SMZ wenye lengo la kurahisisha utendaji kazi na kuleta maendeleo na faida kwa wananchi wa pande zote mbili za muungano.
Pia, amesema jukwaa linafanya ushirikiano huo kuwa imara katika kutekeleza majukumu ya kuliletea Taifa maendeleo.