Ushindi wa Lissu, Mbowe uko hapa

Dar es Salaam. Mizania ya ushindi wa nafasi ya uenyekiti wa Chadema kwa mtazamo wa wataalamu wa siasa, inalingana kati ya Freeman Mbowe na Tundu Lissu, ingawa wanasema kila mmoja ana sifa inayomtofautisha na mwenzake.

Kwa mujibu wa wanazuoni, kuelekea uchaguzi huo, Mbowe anabebwa na ukongwe ndani ya chama na uwezo kiuchumi, huku Lissu akibebwa na aina ya siasa zake zinazotajwa kuupendeza upinzani wa sasa, pia ana timu timamu inayomuunga mkono.

Wahadhiri hao waliobobea katika sayansi ya siasa, wanasema kila sifa ina mchango wake katika kuchochea ushindi wa mgombea, jambo linalowafanya wagombea wote wawe katika mizania sawa, ingawa ipo nafasi ya upepo kubadilika kadri siku zinavyokwenda.

Uchambuzi wa wanazuoni hao, unakuja ikiwa zimebaki siku 14 kwa Chadema kufanyika mkutano mkuu wa uchaguzi Januari 21, mwaka huu, katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam utakaoamua mshindi wa kiti cha mwenyekiti wa chama hicho taifa.

Katika uchaguzi huo, Mbowe anagombea kutetea kiti chake huku Makamu Mwenyekiti Bara, Lissu akigombea kama ingizo jipya katika nafasi ya uenyekiti, iliyoshikiliwa kwa miaka 21 na Mbowe.

Lissu na Mbowe si wagombea pekee katika nafasi hiyo, wamo pia Romanus Mapunda na Charles Odero wanaoutaka uenyekiti wa Chadema, ingawa si wanaotajwa sana katika rasharasha za ushindi.

Katika mazungumzo yao na gazeti hili jana, wasomi hao wanaonyesha dalili ya kuzaliwa kazi mpya ya kuwaunganisha wafuasi wa Chadema baada ya uchaguzi huo, huku wakitaja turufu za ushindi wa Lissu na Mbowe.

Mbowe anatofautishwa na Lissu, kwa historia yake ya kuwa miongoni mwa waanzilishi wa Chadema na hivyo anakijua tangu kuanzishwa kwake, kama inavyoelezwa na mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Faraja Kristomus.

Sambamba na hilo, mwanazuoni huyo anasema Mbowe ana uhusiano mzuri na chama tawala ukilinganisha na Lissu, jambo linalotajwa kuwa turufu nyingine kwake.

Tofauti nyingine ya wawili hao, kwa mujibu wa mwanazuoni huyo ni utulivu wa kuzungumza na uwezo wa kuhimili mashambulizi mambo ambayo anatajwa kuwa nayo Mbowe, huku Lissu akiyakosa.

Dk Kristomas anasema Mbowe pia ni tajiri, anajiweza kiuchumi hategemei siasa kuishi, badala yake Chadema kinamtegemea yeye, tofauti na Lissu ambaye hana sifa hizo.

Hata hivyo, hoja ya Chadema kumtegemea Mbowe, imewahi kufafanuliwa na Lissu, akitaka ujengwe msingi wa chama hicho kuwa na nguvu ya kiuchumi na kisimtegemee mtu mmoja.

Turufu nyingine aliyonayo Mbowe, msomi huyo anasema ni kuungwa mkono na wajumbe wengi zaidi ambao ndiyo wapiga kura, huku Lissu akiungwa mkono na wanachama na wafuasi wa nje ya Chadema.

Ingawa Mbowe anabebwa na turufu hizo, mwanazuoni huyo anasema Lissu ni mwanasiasa mwanaharakati ambaye ndiyo hitaji la kizazi cha sasa cha siasa za upinzani.

Anasema wanasiasa wengi wa upinzani kwa sasa, wangependa kuwa na mtu kama Lissu kwa sababu ana mvuto kwa aina ya siasa za upinzani na anapendwa na vijana wengi.

“Chadema kilipoteza mvuto hivi karibuni baada ya uamuzi wa Mbowe kufanya maridhiano na Serikali. Lissu anaweza kukiokoa chama kutoka kwenye mtanziko huo na mwisho wa siku kikarudi kwenye nafasi yake,” anasema.

Turufu nyingine aliyonayo Lissu, Dk Kristomus anasema ni aina ya timu yake ya kampeni inayomhusisha John Heche (Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema), ambaye ni mwanasiasa mwanaharakati na ana mvuto kwa wanachama wengi.

Muunganiko wa Lissu na Heche, anasema unawavutia wengi na unaweza hata kubadilisha upepo wa kura za uenyekiti siku ya uchaguzi, kuliko ule wa Ezekiah Wenje na Mbowe.

“Heche anaweza kuhimili vishindo na mashambulizi kutoka kwa upande mwingine, hivyo anaweza kuziba mapungufu aliyonayo Lissu lakini Wenje hana uwezo wa kuziba mapungufu ya Mbowe,” anaeleza.

Kwa ujumla, Dk Kristomus anasema ushindani utakuwa mkubwa katika uchaguzi huo, ingawa kitendo cha kuwepo kwa wagombea wengine katika nafasi hiyo kutapunguza kura za mmoja kati ya Lissu au Mbowe.

Anasema itarajiwe kwa siku zilizosalia upepo unaweza kubadilika kutokana na makundi yaliyopo.

“Upande mmoja ukiwa unashambulia na mwingine unajibu kwa hekima na hoja, kuna uwezekano upande huo kuwavutia wapiga kura wengi zaidi kwa kuonekana wana ukomavu wa uongozi,” anasema.

Anasisitiza Mbowe binafsi ana ukomavu wa uongozi, lakini changamoto ni wafuasi alionao, wengi wameonyesha ombwe la ukomavu, pengo linaloweza kutumiwa na wapinzani wake.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Frank Mateng’e anasema wawili hao wamejenga ufuasi ndani ya chama hicho na kila mmoja ana nafasi inayowiana na mwingine katika uchaguzi huo na wote wana kambi zao.

Anasema Lissu anabebwa na hitaji la mabadiliko ya uongozi lililopo kwa baadhi ya wanachama wa Chadema, kutokana na kile wanachodai, Mbowe amehudumu muda mrefu.

“Wanaosema Mbowe amekaa muda mrefu sio kwa sababu hiyo tu, bali wanataka kuona mabadiliko ya aina ya siasa, uhusiano wa chama na dola na uwezo wa chama kusukuma mahitaji yao,” anasema.

Anasema kwa aina ya siasa za Lissu, wanaamini huenda zikazalisha shinikizo litakaloilazimu Serikali kuamua yale wanayoyahitaji.

“Hayo yote ni matumaini lakini hayawezi kuwa hakikisho la kwamba wanachokitarajia kitatokea kama wanavyohitaji, kwamba kauli za Lissu zitafanikisha dola itekeleze mahitaji yao,” anasema.

Kwa mujibu wa Dk Mateng’e, nguvu ya chama haipo kwenye maneno makali ya kiongozi majukwaani, bali ni uwezo wa kuwashawishi wanachama waungane na kiongozi kwa kila anachotaka wafanye.

“Nguvu ya kiongozi haipimwi kwa maneno makali, bali ni namna anavyoungwa mkono kwa vitendo kwenye lolote analolifanya,” anasema.

Kwa upande wa Mbowe, anasema anaonekana ni mwanasiasa mzuri asiye na mihemko ya maneno makali na haamini katika hayo anaposhinikiza kutekelezwa kwa yale anayoyahitaji.

Anamtaja kuwa mwanasiasa anayeamini katika maridhiano, ingawa inamfanya aonekane dhaifu.

Katika hatua nyingine, leo Jumatatu, Lissu amerejea nchini akitokea ughaibuni na akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam amezungumzia masuala mbalimbali yanayoendelea kuhusu uchaguzi huo.

Miongoni ni kikao cha siri kilichofanyikia Msimbazi Center kikimshirikisha yeye (Lissu), Mbowe, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika na kiongozi wa dini ambaye hakumtaja jina. Kikao hicho kilifanyika kwa siku tatu mfululizo.

Msingi wa kikao hicho ni kililenga kuwapatanisha wawili hao ili kila mmoja achague nafasi ya kugombea kati ya uenyekiti na urais kuepusha athari zinazoweza kujitokeza kwa masilahi ya chama.

Kauli hiyo ya Lissu inajibu kile kilichozungumzwa na Mbowe wakati anahojiwa na Crown Media aliyedai uamuzi wa Lissu kugombea nafasi hiyo ulikuwa wa ghafla.

“Kama kila moja aliona kwamba anastahili kugombea hatunyimani nafasi lakini hatukuona athari tuliona athari kwa sababu tulishakubaliana juu ya nafasi za kugombea ila ikawa ghafla sana yeye kutangaza kugombea nafasi ya uenyekiti ngazi ya taifa,” alisema Mbowe.

Hata hivyo, Lissu amesema katika kikao hicho kilichofanyika Msimbazi wapatanishi wakuu walikuwa mapadre.

“Katika siku tatu zote Mwenyekiti alisema hajaamua kugombea nafasi yeyote na Katibu Mkuu, John Mnyika ni shahidi kwa siku tatu tukizungumza pamoja,” amesema.

Lissu amesema Mbowe alikuwa hataki Lissu atie nia lakini wapatanishi walipokuwa wanamuuliza majibu yake alikuwa anadai bado hajaamua.

“Sijawahi kuzungumza naye chochote nje ya hapo katika hizo siku tatu, nilimuambia mwenyekiti baada ya hayo yote muafaka nini, kwangu mimi nikasema suala la kuokoa hiki chama huko tunakoenda si kuzuri niko tayari nigombee uenyekiti wa chama na urais nimuachie Mwenyekiti,” amesema.

Katika hatua nyingine, Lissu amesema Mjumbe wa Kamati Kuu, John Heche ni miongoni mwa viongozi hazina kwa chama hicho.

Lissu amemwagia pongezi hizo Heche, ikiwa siku moja imepita baada ya Heche kutangaza kumuunga mkono alipokuwa anachukua na kurejesha fomu ya kuwania umakamu wenyekiti wa Chadema.

“Heche ni moja wapo ya hazina ya viongozi kwa chama chetu nafikiri sitasema cha ajabu nikisema hivyo, Heche amekuwa mbunge wa chama chetu alishinda uchaguzi na amekuwa kiongozi wa Bavicha, amekuwa mjumbe wa Kamati Kuu,” amesema. 

Amesema amefanya kazi kwa ukaribu kwenye kamati kuu na bungeni na alikuwa kwenye kamati ya maridhiano na kama asingelikuwepo basi umma usingejua mambo mengi yaliyokuwa yanaendelea.

Related Posts