Dar es Salaam. Kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa gramu 41.49 inayowakabili wanandoa, imepangwa kuanza kusikilizwa Januari 20, 2025.
Wanandoa hao, Shabani Adamu na mkewe Husna Issa pamoja na mtoto wao wa kiume, Mussa Shabani, wanakabiliwa na kesi ya kusafirisha heroini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Kesi hiyo imeitwa leo Jumatatu, Januari 6, 2025, kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ya kuanza usikilizwaji baada ya washtakiwa hao kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo mwezi uliopita.
Hata hivyo, Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Godfrey Mhini, yupo likizo, hivyo kesi imeahirishwa kwa hakimu mwingine, Beda Nyaki.
“Hakimu anayesikiliza kesi yenu yupo likizo, hivyo naiahirisha hadi Januari 20, 2025. Washtakiwa mtaendelea kubaki rumande kwa kuwa shtaka linalowakabili halina dhamana,” amesema Hakimu Nyaki.
Desemba 23, 2024, washtakiwa hao waliieleza mahakama hiyo kuwa wanakusudia kumuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) wakiomba kukiri makosa yao na kupunguziwa adhabu.
Washtakiwa hao, kupitia wakili wao Nehemia Nkonko, walitoa taarifa hiyo siku hiyo, muda mfupi baada ya kesi yao ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa.
Nkonko baada ya kutoa taarifa hiyo, Serikali ilisema bado haijapata barua hiyo, na wakiipata wataifanyia kazi.
Desemba 11, 2024, washtakiwa hao walisomewa hoja za awali mahakamani hapo.
Mahakama hiyo ilielezwa namna washtakiwa hao walivyodakwa na kiasi hicho cha dawa nyumbani kwao Manzese.
Washtakiwa hao walisomewa maelezo yao na Wakili wa Serikali, Anna Thomas, ambapo alidai washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Julai 11, 2024, eneo la Kilimani, Manzese.
Aliendelea kudai kuwa, washtakiwa Shabani na Husna ni wanandoa na Musa ni mtoto wao.
Alidai kuwa, Julai 11, 2024, Koplo Jackson alipata taarifa kwamba eneo la Manzese Kilimani kuna watu wanajihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya.
Baada ya kupata taarifa hizo, Koplo Jackson akiwa na wenzake waliweka mtego wakitaka kuuziwa dawa hizo.
Koplo Jackson na timu yake walikwenda eneo hilo wakiwa na mjumbe ambapo waliwakamata washtakiwa na kisha kufanya upekuzi katika nyumba ya washtakiwa hao.
“Katika upekuzi huo, walikamata vitu mbalimbali, ikiwemo mfuko wa nailoni angavu wenye unga wa chengachenga, mifuko miwili ya nailoni yenye unga mweupe unaosadikika kuwa ni dawa za kulevya, kitambulisho cha NIDA cha Adamu, simu tatu, fedha taslimu Sh130,000, kisu, kijiko cha chakula na jiko la gesi,” alidai Wakili Thomas wakati akisomea hoja za awali.
Aliendelea kudai kuwa, baada ya upekuzi, hati ya kukamata mali ilijazwa na washtakiwa Adamu, Husna, askari na mjumbe, na walitisaini nyaraka hiyo isipokuwa Musa.
Hata hivyo, unga huo ulichunguzwa katika Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kubainika kuwa ni dawa za kulevya aina ya Heroini zenye uzito wa gramu 41.49.
Washtakiwa walipohojiwa polisi walikiri kutenda kosa hilo.