Kituo kikubwa kujaza gesi kwenye magari UDSM kuanza kazi

Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dk James Mataragio amesema kituo cha kujaza gesi asilia kwenye magari eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kitaanza majaribio ya awali Januari 16, 2025.

Amesema kituo hicho chini ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kilipaswa kuanza kazi Desemba 2024, lakini kimechelewa kutokana na meli iliyobeba mitambo ya gesi kuchelewa kufika Tanzania.

Akiwa kwenye ziara ya kukagua maendeleo ya kituo hicho leo Jumatatu, Januari 6, 2025 Dk Mataragio amesema ujenzi umefikia asilimia 80 na kazi inafanyika usiku na mchana.

“Januari 16, tutaanza majaribio na yatafanyika kwa wiki mbili na mwishoni mwa Januari gari la kwanza litaanza kujazwa gesi kwenye kituo hiki, kazi inafanyika hapa kwa saa 24, eneo la karakana ya kubadili mifumo ya gari kutumia gesi nayo imefikia asilimia 90,” amesema.

Dk Mataragio amesema kituo hicho kitatumika kusafirisha gesi asilia kwenda mikoa ya jirani Dodoma na Morogoro pamoja na kutumika kama nishati viwandani.

Kwa upande wake, Meneja Msimamizi wa Mradi wa CNG kutoka TPDC, Aristides Katto amesema kituo hicho kitakapokamilika kitapunguza changamoto za vituo vya kujaza gesi kwenye magari.

“Kitakuwa na uwezo wa kujaza vituo vingine kwa sababu hiki ni kituo mama watu wanakuja kuchukua gesi na kupeleka kwenye vituo vingine.

“Kituo hiki kitasaidia pia kwenye mradi wa gesi majumbani, kwenye viwanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili,” amesema.

Ujenzi wa mradi huo wa kujaza gesi kwenye magari unagharimu Sh14.55 bilioni na kituo kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kushindilia gesi kwenye magari matatu ya kusafirisha gesi kupeleka mahali pengine pamoja na kujaza na uwezo wa kujaza magari 1000 kwa siku.

Kwa mujibu wa TPDC, kiwango cha gesi kinachoweza kushindiliwa kwa siku na mitambo ya kituo hicho ni futi za ujazo milioni tatu kikihudumia magari na viwanda, kikiwemo kiwanda cha dawa Kairuki kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

Kituo hicho kitakuwa na pampu nne za kujaza gesi zenye uwezo wa kuhudumia magari manane kwa wakati mmoja.

Kukamilika kwa kituo hicho kunakuja wakati ambapo baadhi ya vituo vilivyopo nchini vimeelemewa na vyombo vya moto vinavyotumia gesi asilia.

Kituo cha Ubungo baadhi ya madereva wa bajaji walieleza kadhia ya kukwama kurejesha mikopo kwa ajili ya vyombo hivyo kwa kuwa wameshindwa kufanya kazi.

Wanadai kutumia mafuta ni gharama kubwa,  kwani gesi asilia gharama yake ni Sh6,500 kwa kilo nne ambayo hujaza mara mbili tofauti na mafuta ambayo kwa siku  hulipia zaidi ya Sh 30,000 kwa lita moja.

Akielezea manufaa kituo hicho, Mchambuzi wa masuala ya uchumi Oscar Mkude amesema kitapunguza kero ya watu kushinda vituoni kusubiri nishati hiyo.

“Watu wakikaa sana vituoni kusubiri gesi inawakatisha tamaa wale ambao walitamani kuunganisha mfumo wa gesi kwenye vyombo vyao, kwa hiyo kituo kuanza kuifanya kazi ni jambo zuri,” amesema.

Amesema kinachohitajika sasa ni kuongezwa vituo vingi zaidi vya gesi kuondoa changamoto wanazopitia wateja ili kuvutia watu kutumia gesi badala ya mafuta.

“Tukiwa na vituo vingi watu wataagiza sasa magari moja kwa moja inayotumia mifumo ya gesi badala ya mafuta, kwa sababu magari haya unapobadilisha mifumo ufanisi wake uapungua.

“Kwa madereva magari mtandao wanaotumia gesi wanakosa fursa ya kubeba wateja wenye mizigo kwa sababu nyuma ya magari yao yana mitungi mikubwa, hivyo kwenye kazi wanachagua abiria sana,” amesema.

Mkude amesema matumizi ya gesi yakiwa makubwa nchini ni rahisi kudhibiti mfumuko wa bei ambao kwa kiasi kikubwa unachangiwa na bei ya mafuta kupaa mara kwa mara.

Agustino Paulo, dereva bajaji iliyounganishwa na mifumo ya gesi, amesema ni nafuu zaidi kukiwa na vituo vingi vya kujaza gesi asilia kwenye magari, kwani wanalazimika kuacha kazi kusubiri foleni kupata gesi.

“Ukisubiri kwa muda mrefu maana yake utashindwa kufanya kazi, familia inashindwa kupata mahitaji kwa sababu kwa siku hujaingiza unasubiri kuongeza gesi ili ukafanye kazi, pia haitakuwa nafuu kwetu tu hata kwenye magari nao watapata huduma haraka,” amesema.

Ujenzi wa kituo, hali ilivyo

Taarifa ya TPDC inaonyesha ujenzi wa kituo kimoja cha kujaza gesi inagharimu kati ya Sh2.1 bilioni hadi Sh2.7 bilioni kulingana na ukubwa na mahitaji ya eneo wakati kituo cha mafuta ni Sh400 milioni.

Kuhusu kiwango cha gesi kilichopo nchini, Tanzania inakadiriwa kuwa na futi trilioni 230 za ujazo za gesi asilia, ingawa zilizothibitishwa mpaka sasa ni futi trilioni 57.5, hivyo kuiweka kwenye ramani ya dunia ikishika nafasi ya 82.

Gesi hiyo tayari imeanza kuchimbwa katika visiwa vya Songosongo wilayani Kilwa mkoani Pwani na eneo la Msimbati mkoani Mtwara, ikitumika kuzalisha umeme na kuendesha mitambo ya baadhi ya viwanda nchini.

Vituo vilivyopo na magari

Hadi sasa endapo kituo cha kujaza gesi kwenye magari kitakapokamilika kutafanya idadi ya vituo vya gesi nchini kufikia vitano. Vituo vingine ni cha Uwanja wa Ndege, Tazara, Ubungo na TOT Tabata.

Kwa idadi ya magari, taarifa ya mwisho ya mwaka jana ya TPDC ilionyesha magari yanayotumia mfumo wa gesi nchini ni zaidi ya 4,800, lakini uwezo wa vituo vya kujaza gesi ni kuhudumia magari 1,200 hadi 1,500 kwa siku.

Related Posts