Dar es Salaam. Marehemu Francis Ogalla aliyekuwa Mkuu wa Majeshi nchini Kenya, atazikwa pasipo mwili wake kuwekwa kwenye jeneza, kaka yake mkubwa Canon Hezekiah ameeleza.
Jenerali Ogalla alifariki dunia Aprili 18, 2024 baada ya helikopta aliyokuwa akisafiria pamoja na maofisa wengine tisa wa Jeshi kuanguka.
Kifo cha kiongozi huyo mkuu wa Jeshi nchini Kenya kilitangazwa na Rais wa Kenya, William Ruto.
Taarifa za kituo cha habari cha Citizen Digital nchini Kenya jana Aprili 19, 2024 kilimnukuu Hezekiah akisema maziko ya kaka yake yatafanyika Aprili 21, 2024 na yatakuwa rahisi, kwani mdogo wake alitaka kuzikwa ndani ya saa 72 baada ya kufariki dunia.
Amefafanua Jenerali Ogalla alimuonyesha eneo ambalo atazikwa jirani na nyumba yake katika kijiji cha Mor, kaunti ya Siaya.
Japo kiongozi huyo alikuwa Mkristo, alichagua kuzikwa pasipo mwili wake kuwekwa kwenye jeneza kwa mujibu wa kaka yake, ili kupunguza gharama kwa familia.
Hata hivyo, amesema taratibu za mila na desturi za kabila la Wajaluo zitazingatiwa.
Peris Onyango, dada wa CDF Ogalla amefichua kuwa kaka yake alijiandaa kwa kifo.
Amesema wakati wote alipomtembelea alimweleza jinsi maziko yake yanapaswa kuonekana, licha ya yeye kumzuia na kumtaka kuondokana na mawazo ya kifo.
Amesema Ogalla alimweleza kifo kipo hasa kwao askari ambao kazi yao ni kwenda mstari wa mbele vitani.
“Kifo hicho cha ghafla kimetia jamii nzima katika hali ya simamzi kwa kuwa kaka alikuwa msaada kwenye jamii,” amesema Peris.
Amesema alikuwa mkarimu, aliyesikiliza matatizo yanayowakabili wananchi kijijini kwake.
“Alisaidia kanisa na kuhakikisha linakamilika, akatoa kisima cha maji, na kutoa misaada kwenye shule alizosoma,” amesema.
“Ndiyo maana taarifa za kifo chake zilipotangazwa watu walikuja kwa wingi kumuomboleza kwa sababu hakuwa na mipaka,” amesema.