Usafiri Moshi bado changamoto | Mwananchi

Moshi. Mamia ya abiria wanaotaka kusafiri kutoka Moshi kwenda maeneo mbalimbali nchini, hususani mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma ambao hawakukata tiketi mapema wanalazimika kusubiri kusafiri hadi Januari 9, mwaka huu kutokana na magari mengi kujaa.

Hali hiyo inatokana na wingi wa abiria wanaorudi makwao, baada ya kumalizika kwa sherehe za mwisho wa mwaka.

Mwananchi Digital leo Jumatatu, Januari 6, 2025 limetembelea maeneo mbalimbali ya stendi kuu ya mabasi Mjini Moshi na kushuhudia abiria wengi waliopo katika stendi hiyo pamoja na kuzungumza na baadhi ya wakata tiketi ambao wamedai magari yamejaa mpaka Januari 9, mwaka huu.

Pamoja na magari ya mikoani kujaa, pia kumekuwepo na changamoto ya usafiri wa ndani, hasa wanaotoka Moshi mjini kwenda Bomang’ombe Wilaya ya Hai, Siha na wale abiria wanaotoka mjini Moshi kwenda Wilaya ya Rombo.

Kutokana na changamoto hiyo ya usafiri, abiria hao wanalazimika kusubiri magari kwa muda mrefu katika stendi hiyo kutokana na abiria wengi waliopo, huku baadhi ya abiria wakigombania magari hayo na wengine kulazimika kupitia dirishani.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo, baadhi ya wasafiri wamesema takribani wiki moja sasa wameshindwa kusafiri kutokana na magari kujaa.

Mmoja wa wasafiri katika stendi hiyo, Devis Minja, amesema usafiri umekuwa changamoto na kwamba wanapokwenda kwenye baadhi ya ofisi za magari kukata tiketi wanaambiwa magari yamejaa hadi Januari 9, mwaka huu.

“Usafiri umekuwa ni changamoto kwa sababu watu waliwahi kushika nafasi kwenye magari, nina wiki sasa natafuta usafiri hakuna nafasi. Naambiwa zimejaa, hivyo nitalazimika kusafiri hiyo tarehe,” amesema Minja.

Abiria mwingine wa Dodoma, Amina Ally amesema wanawalazimu kukaa stendi muda mrefu kusubiri magari, hali inayoleta usumbufu.

“Msimu huu naona abiria ni wengi, watu wanarudi makwao, usafiri hapa umekuwa wa shida, kila ukienda kwenye ofisi unaambiwa magari yamejaa. Nipo hapa stendi na sina uhakika kama nitapata gari,” amesema abiria huyo.

Jully Tesha, mkazi wa Bomang’ombe Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, amesema changamoto ya usafiri imewaathiri kwa kiasi kikubwa, hali inayowalazimu wengi kupanda magari yanayokwenda mkoani Arusha.

Mmoja wa wakata tiketi katika stendi hiyo, Juma Yahaya, amesema nafasi za magari zimejaa mpaka Alhamisi ya Januari 9, mwaka huu kutokana na wingi wa abiria wanaorudi makwao.

“Magari yetu hayana nafasi yamejaa hadi Alhamisi, Januari 9, abiria ni wengi wanaorudi mikoani, “amesema mkata tiketi huyo.

Mmoja wa madereva katika stendi hiyo, Hashim Juma, amesema abiria ni wengi na kwamba wanaotaka kusafiri watalazimika kusubiri au kutumia njia mbadala ya kusafiri.

Katibu mkuu wa stendi ya mabasi Moshi, Godlisten Mushi, amesema changamoto ya usafiri ipo kwa wananchi wanaokwenda mikoa ya Arusha, Dodoma na Dar es Salaam.

“Abiria ni wengi na magari yanaonekana kuwa machache, hali hii imekuwa ikitokea kipindi hiki, baada ya watu kutoka kwenye sikukuu za mwisho wa mwaka,” amesema.

Kwa upande wa Arusha, amesema changamoto kubwa ipo wakati wa jioni, hali inayowafanya abiria kugombania kuingia kwenye magari pindi yanapofika.

Alipotafutwa ofisa mfawidhi wa Mamlaka ya usafiri wa ardhini(Latra) Mkoa wa Kilimanjaro, Paulo Nyello amesema changamoto ya usafiri iliyopo ni kutokana na abiria wengi wanaorudi makwao baada ya kumalizika kwa sikukuu za mwisho wa mwaka na kwamba wametoa vibali kadhaa kwa magari ili kupunguza changamoto hiyo.

“Tulichofanya kwa hiki kipindi chote cha sikukuu ni kutoa vibali vya mabasi yanayotoka nje ya mkoa, kwa mfano Dar es Salaam kulikuwa na mahitaji makubwa, hivyo tulitoa vibali ili kupunguza wingi wa abiria waliopo, na hata ndani ya mkoa nako tumetoa vibali mpaka Januari 18, mwaka huu,” amesema Nyello.

Related Posts