Majaliwa: Ubora wa miradi uwiane na thamani ya fedha zinazotolewa

Zanzibar. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wasimamizi wa miradi inayotekelezwa na Serikali, ikiwemo ya elimu kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaolingana na thamani ya fedha iliyotolewa.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Januari 6, 2025 wakati wa ufunguzi wa Skuli ya Sekondari ya Makoba iliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar. Ufunguzi wa skuli hiyo ni sehemu ya shamrashamra kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema Serikali imeendelea kutenga rasilimali fedha kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya elimu ambayo kwa kiasi kikubwa imewezesha kuweka mazingira bora ya upatikanaji wa elimu, ikiwemo ujenzi wa miundombinu.

Aidha, amesema katika kipindi cha miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi ameendelea kuipa hadhi sekta ya elimu kwa kuhakikisha kunakuwa na ufanisi wa utoaji wa huduma za elimu.

“Sina shaka leo hii chini ya Jemedari Dk Mwinyi sote tunashuhudia mwendelezo wa hatua kubwa ya kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu nchini. Suala hili ni la kujivunia kwa kuwa ni matunda ya Mapinduzi ambayo sasa yanafikisha miaka 61 tangu kuasisiwa kwake,” Amesema.

Kadhalika, Majaliwa amesema Serikali inayoongozwa na Rais Mwinyi, imeendelea kufanya mageuzi makubwa ya elimu katika kuhakikisha kunakuwa na ufanisi wa utoaji wa huduma za elimu nchini.

“Mageuzi hayo ni pamoja na kutekeleza mtaala mpya wa umahiri utakaomwezesha mtoto kujifunza kwa vitendo na kumudu kasi kubwa ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia”.

Ameongeza Serikali imeendelea kutekeleza mipango, mikakati na kufanya jitihada za makusudi za kuhakikisha kunakuwa na maendeleo kwenye sekta zote za kijamii, ili kuleta tija inayotarajiwa kwa wananchi bila ubaguzi wa aina yoyote.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa, amesema Rais Mwinyi ameendeleza ari ya waasisi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha analeta mageuzi katika sekta ya elimu.

“Serikali hii iliahidi kuboresha miundombinu ya madarasa kwa shule za msingi kwa kujenga madarasa 1,000 na 500 kwa ngazi ya sekondari na mpaka sasa kwa ngazi ya msingi imejenga madarasa 2,893 na sekondari imejenga madarasa 1,917” amebainisha.

Ujenzi wa shule hiyo ambao umefikia asilimia 100 umegharimu Sh6.1 bilioni ambazo zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Related Posts