DKT. BITEKO AKAGUA UJENZI WA OFISI YA WAZIRI MKUU NA JENGO LA WIZARA YA NISHATI

*Aagiza ujenzi ukamilishwe haraka

*Majengo yakamilika kwa asilimia 88

*Wakandarasi waomba nyongeza siku 90

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amefanya ziara katika Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma kukagua maendeleo ya ujenzi majengo ya Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu pamoja na Wizara ya Nishati ambayo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 88. 

Akizungumza baada ya kukagua na kupata maelezo ya wataalam na wasimamizi wa majengo hayo, Naibu Waziri Mkuu Biteko amewapongeza wakandarasi kwa hatua iliyofikiwa na kuagiza majengo yakamilishwe kabla ya mwezi Aprili, 2025.

“Serikali chini ya Rais Samia imefanya kazi kubwa, tayari imetoa zaidi ya asilimia 90 ya malipo kwa wakandarasi kwa maana ya kwamba ni kiasi kikubwa zaidi ya ukamilifu wa jengo, Najua SUMA JKT mkifanya kazi kwa operesheni mnaweza kukamilisha ujenzi wa jengo hili hata kabla ya muda uliopangwa” amesema Dkt. Biteko

Msimamizi wa Ujenzi Jengo la Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, kutoka SUMA JKT Kanali Mbaraka Magogo ameomba Serikali iwaongezee muda wa miezi mitatu kuanzia sasa ili kukamilisha ujenzi na majengo yatumike ifikapo mwezi Aprili, 2025.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametembelea jengo la Wizara ya Nishati ambapo amemtaka mkandarasi ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuharakisha ukamilishaji ujenzi wa jengo hilo na lianze kutumika kabla ya mwezi Aprili, mmwaka huu.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu, Mhe. Ummy Nderiananga amemshukuru Naibu Waziri Mkuu kwa maelekezo yake na kusema Ofisi itaendelea kusimamia kwa karibu ili kuhakikisha kwamba malengo yanafikiwa kama ilivyopangwa.

“Kwa niaba ya Waziri Nchi Mhe. Lukuvi (William Lukuvi) namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwa ziara hii ambayo ni chagizo kwetu kuhakikisha kwamba ujenzi wa majengo haya unakamilika kwa wakati kama walivyoomba wakandarasi, kwa kuwa sisi ni waratibu inabidi tuwe mfano kwa wengine.” Amesema Mhe. Ummy.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felichesmi Mramba amemhakikishia Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kuwa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa Wizara hiyo ziko katika hatua nzuri na amekuwa akiwasiliana na HAZINA kwa ajili ya upatikanaji wake.

“Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, tuko katika hatua nzuri hata leo asubuhi nimezungumza na PST (Katibu Mkuu Wizara ya Fedha) na nimehakikishiwa kwamba fedha hizo zitapatikana,” amesema Katibu Mkuu Mramba.         

Related Posts