Dakika chache za kwanza tunapokutana na wapenzi wetu baada ya kuachana kwa kitambo kifupi zina umuhimu.
Kitambo hiki ni kile ambacho labda mpenzi wako alikuwa kazini au safarini, umepita muda fulani hamjaonana, yamkini moyoni ulitamani kumwona au hata kule kutamani (kummiss) kulisha poa, jiulize mara utakapomwona, labda ni uwanja wa ndege, kituo cha basi, au amefungua mlango kuingia nyumbani. Je, unafanya nini.
Kile utakacho kifanya hapa kina nafasi kubwa katika kuharibu penzi na ukaribu wenu (intimacy) au kulijenga kwa kasi kubwa, ni uchaguzi wako, ingawa unashauriwa kufanya haya yafuatayo:
1. Jiandae wewe mwenyewe kiakili
Kabla hamjaonana uso kwa uso andaa vema akili yako kumlaki mpenzi wako. Fikiri mawazo mazuri siyo yale mabaya yake. Usiwaze kummwagia lawama mara tu utakapomwona. Panga nafsini mwako kitu au tukio la kufurahisha utakalomfanyia mara ukimwona, mara nyingine unaweza kumuuliza kwa simu muda atakapowasili ili uweze kujiandaa vile unavyodhani.
2. Jiangalie mwonekano wako
Dakika ya kwanza tu mnapotazamana yaweza kuathiri mwendelezo mzima wa siku yenu. Sura yako ya uso, tabasamu lako, harufu yako (nzuri au mbaya) vyaweza kumdaka au kumkimbiza mpenzi wako, haswa yule wa kiume. Wanaume pia nao wana cha kufanya, haupaswi kupokewa ukiwa rafu, mchafu, unatoa harufu mbaya ya mwili au viatu.
Jiangalie, nywele na ndevu zako zikoje, meno yako yanaonekanaje na hata ngozi yako, hususan ya usoni. Mwonekano wako kuzungumza zaidi vile unavyojiona wewe mwenyewe. Huhitaji kusema mimi sijipendi, bali kuonekana kwako kutatoa ujumbe. Jaribu uwezavyo kuwa mwenye mvuto mara utakapokuwa na umpendaye.
3. Onyesha tabasamu la pendo kwa mpenzi wako
Panga muda wako ili uweze kumsalimu mpenzi wako kwa tabasamu. Acha mpenzi wako ajue kuwa yeye ni wa kipaumbele, ni muhimu kwako, usimpokee kwa staili ya kumwonyesha humjali. Tabasamu linaweza kusema “I love you” kuliko hata maneno au zawadi. Tabasamu halina gharama yoyote, ni la bure na lipo wakati wowote, kinacho kushinda ni nini?
Hata kama hujisikii kutabasamu, jitahidi kwa namna yoyote kuonyesha kuwa unaweza pia kutabasamu. Jifanyishe pale mazingira yanapokuwa magumu, hususani katika dakika nne za mwanzo. Ikiwa utajifanyisha vizuri, hisia njema zaweza kuibuka na yale maumivu ya moyo ya ndani yaweza kutoweka taratibu.
4. Salimianeni kwa kukumbatiana na kwa busu
Kuwa na mtu anayetusubiri mara tutakapofika sehemu au mara tutakapofungua mlango ni jambo ambalo wengi wetu tunalipenda, kama kubusu sio mtindo au pendeleo lako basi tafuta njia nyingine ya miili yenu kugusana mara mnapoonana. Mfano kushikana mkono, kumshika mwenzako nywele au kichwa, nk. Mgusano wa mwili ni muhimu na unashauriwa kwa afya ya penzi lenu.
5. Tengeneza mazingra mwanana
Jipeni muda wa kupumzika na kupumzisha akili kabla ya kuanza kuzungumzia matatizo. Kila anayeingia nyumbani na kukuta anapokelewa na makelele na mikikimikiki hutamani kuondoka.
Kila anayekuwa nyumbani kwanza kabla ya mwenzake anawajibika kutengeneza mazingira ya hisia nzuri, ingawa baada ya hapo wote wawili pia mna wajibu wa kuendeleza hisia njema na mazingira ya amani yaliyopo.
Wale ambao wanafanya kazi nje ya nyumbani huhitaji utulivu kidogo mara wanaporudi ili kutuliza akili na hisia zao, wengine watataka dakika 15, wengine 20, wanataka kujinyoosha kidogo, au kusikiliza muziki fulani bila maongezi mengi, ingawa pia wapo wanaotaka kucheza na watoto mara wanapofika nyumbani.
Chochote na kwa hali yoyote uipendayo, jaribu kujielezea, na mueleze mwenzako aelewe, hii itawasaidia sana.