Fadlu alivyovunja mwiko wa miaka 22

KOCHA wa Simba, Fadlu Davids, ameweka rekodi ndani ya timu hiyo baada ya kupata ushindi wa bao 1-0, juzi dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia. Ushindi huo ni wa kwanza ugenini kwa kikosi hicho kuupata Ukanda wa Kaskazini mwa Afrika kwenye michuano ya CAF.

Bao la Simba lilifungwa na kiungo mshambuliaji, Jean Charles Ahoua dakika ya 34 ukiwa ni mchezo wa Kundi A wa Kombe la Shirikisho Afrika na kuifanya timu hiyo kufikisha pointi tisa, sawa na CS Constantine ya Algeria inayoongoza kundi baada ya michezo minne.

Ushindi huo ni wa kihistoria kwa Fadlu kushinda katika ardhi ya Waarabu tangu mara ya mwisho timu hiyo ilipoitoa Zamalek ya Misri iliyokuwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa mwaka 2003 kwa penalti 3-2, baada ya sare ya bao 1-1 na kutinga hatua ya makundi.

Rekodi hiyo ilishikiliwa na Yanga hivi karibuni ikifanya mara mbili kwa msimu mmoja baada ya kuifunga Club Africain ya Tunisia pia katika hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika, kufuatia mchezo wake wa kwanza uliopigwa jijini Dar es Salaam Novemba 2, 2022 kutoka suluhu.

Mchezo wa marudiano uliopigwa Tunisia, Yanga ikashinda bao 1-0, lililofungwa na kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Stephane Aziz KI, Novemba 9, 2022.

Katika msimu huo wa 2022-2023, Yanga ilifika hadi fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ilipoteza mbele ya USM Alger ya Algeria kwa kanuni ya bao la ugenini, baada ya mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam kuchapwa mabao 2-1, Mei 28, 2023.

Mchezo wa marudiano uliopigwa Algeria, Yanga ikashinda bao 1-0, Juni 3, 2023, ukiwa ni ushindi wa pili kwa Waarabu ugenini ndani ya msimu mmoja.

Hata hivyo, Simba imekuwa ni timu ya kwanza nchini tangu tupate Uhuru mwaka 1961 kuifunga klabu kutoka Kaskazini mwa Afrika nje ndani, baada ya kuichapa Sfaxien mabao 2-1, jijini Dar es Salaam Novemba 27 mwaka jana, kisha juzi kushinda bao 1-0.

“Sio rahisi kwa sababu unapocheza na timu za aina hii ni lazima ujipange kiakili, kimwili na kisaikolojia kutokana na jinsi ambavyo wanajua kutafuta matokeo chanya wakiwa kwao, mchezo umeisha na sasa tunaangalia kilichokuwa mbele yetu.”

Fadlu aliongeza ushindi huo umewapa matumaini makubwa ya kupambana tena ugenini na Bravos do Maquis ya Angola Januari 12, huku akiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda pia bao 1-0, la Jean Charles Ahoua Novemba 27, mwaka jana jijini Dar es Salaam.

Ushindi wa Simba dhidi ya Bravos utaifanya kufikisha pointi 12 na kufuzu robo fainali ya michuano hiyo baada ya kufanya hivyo msimu wa 2021-2022, huku ikikamilisha tu ratiba kwa kucheza na CS Constantine Januari 19, jijini Dar es Salaam.  Katika msimu wa 2021-2022, Simba ilifika robo fainali ya Kombe la Shirikisho, ikatolewa kwa penalti 4-3 na Orlando Pirates ya Afrika Kusini, baada ya kushinda nyumbani bao 1-0, Aprili 17, 2022, kisha kuchapwa ugenini pia 1-0 Aprili 24, 2022.

Rekodi hiyo ya Fadlu ni ya pili kwake tangu ajiunge na timu hiyo ya Simba Julai 5, 2024, akichukua nafasi ya Mualgeria Abdelhak Benchikha baada ya kushinda pia michezo minne mfululizo ya Ligi Kuu Bara kwa msimu huu bila ya kuruhusu bao.

Tangu msimu wa 2020-2021, hadi sasa ilikuwa ni Yanga pekee iliyoshinda michezo minne mfululizo ya mwanzo wa Ligi Kuu Bara bila kuruhusu bao, ikifanya hivyo msimu wa 2021-2022 kwa kuzichapa Kagera Sugar na Geita Gold bao 1-0, kila mmoja wao.

Baada ya hapo Yanga ikacheza mchezo wa tatu na wa nne kwa kuzichapa KMC na Azam FC mabao 2-0 kila mmoja wao na kuanzia hapo hakuna timu nyingine iliyofanya hivyo, hadi Simba msimu huu chini ya Fadlu ilipojiandikia pia rekodi hiyo.

Simba msimu huu ilianza Ligi Kuu Bara kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United, ikashinda 4-0 mbele ya Fountain Gate yote ikicheza Uwanja wa KMC, ikaifunga Azam FC 2-0 kwenye Uwanja wa New Amaan Zanzibar kisha kuichapa Dodoma Jiji bao 1-0 pale Jamhuri, Dodoma.

Related Posts