Waziri Mkuu Canada atangaza kujiuzulu, Trump atoa kauli

Canada. Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau ametangaza kujiuzulu wadhfa huo na uongozi wa chama tawala nchini humo huku akisema ataondoka ofisini mara baada chama chake kutangaza mrithi wa nafasi yake.

Trudeau ametangaza uamuzi huo jana Jumatatu Januari 6, 2025, huku akidai amelazimika kufanya hivyo kutokana na mzozo wa kisiasa uliogubika ndani ya utawala wa nchi hiyo.

Tovuti ya The Guardian imeripoti kuwa kutokana na mgogoro huo, Trudeau anadai kushindwa kusimamia shughuli za Serikali jambo linalomkwamisha kukifikisha salama chama chake cha Kiliberali (Liberal Party) katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Ametangaza uamuzi huo akiwa nyumbani kwake Rideau Cottage Jijini Ottawa nchini humo, wiki kadhaa tangu akumbane na msukumo mkubwa wa wafuasi wa Chama chake wakimshinikiza kujiondoa katika wadhfa huo kwa hofu kwamba atakiponza chama chao kwenye uchaguzi ujao.

“Taifa hili linapaswa kupata mtu sahihi kwenye Uchaguzi ujao na imenijia kichwani kwamba kwa jinsi mambo yalivyo hususan migogoro ya ndani inayoendelea sitoweza kuwa mtu sahihi na bora kwenye uchaguzi ujao,” amesema Trudeau.

Uchaguzi Mkuu wa Canada, unatarajiwa kufanyika kabla ya Oktoba 20, mwaka huu.

Kiongozi huyo amesema tayari ameshamuomba Rais wa Canada, kuanzisha mchakato wa kumpata kiongozi mpya wa kujaza nafasi hiyo na kubeba maono ya chama kuelekea uchaguzi huo.

Pia ameagiza kusimamishwa kwa shughuli za Bunge ikiwemo midahalo na upigaji wa kura hadi Machi 24, 2025, wakati ambao huenda msimamizi mkuu wa shughuli za taifa hilo anadhaniwa kuwa huenda akawa amepatikana.

Hadi kufikia leo Jumanne Januari 7, 2025, wabunge wa Bunge la nchi hiyo wako likizo huku wakitarajia kurejea kazini Januari 27, mwaka huu.

Uamuzi huo wa Trudeau unamfanya kuungana na Waziri wa Fedha, na Naibu Waziri wake, Chrystia Freeland, waliotangaza uamuzi wa kuachia ngazi Desemba 16, 2024.

Freeland, ambaye babu yake alikuwa Mnazi ’Nazis’ wa Ukraine wakati wa vita ya pili ya dunia (WWII) alijiuzulu kufuatia kuibuka mzozo uliotokana na uamuzi wa Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump wa kuongeza kodi ya asilimia 25 kwenye kila bidhaa inayoingia Marekani kutoka nchini Canada.

Baada ya Trump kutangaza uamuzi huo, Trudeau alisafiri kwenda Marekani yalipo makazi ya Trump, eneo la Mar-a-Lago akienda kueleza kuwa uamuzi huo wa Trump utaibua vita ya kiuchumi kati ya mataifa hayo.

Hata hivyo, hatua aliyochukua kwenda Marekani iligeuka na kuanza kumtafuna kutokana na kukumbana na upinzani mkubwa nchini Canada.

Trudeau, ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu mstaafu wa taifa hilo, Justin Trudeau aliingia madarakani mwaka 2015 na kukiongoza chama cha Kiliberali kushinda uchaguzi mkuu wa nchi hiyo mara mbili ikiwemo Uchaguzi wa 2019 na 2021.

Katika awamu mbili za uongozi wake, Trudeau alifanya mabadiliko ya baraza la mawaziri, kusaini mkataba mpya wa ushirikiano wa kibiashara kati ya Canada na Marekani.

Pia aliridhia matumizi ya bangi nchini humo, sambamba na kupitisha sheria inayoridhia mauaji ya mgonjwa ambaye anapitia mateso makali.

Taswira na nguvu ya kisiasa ya Trudeau, iliporomoka zaidi kutokana na sera mbalimbali ikiwemo sera ya malipo ya kaboni na kuanzisha Sheria kali ya Uhamiaji kipindi cha Uviko-19 na namna ya kudhibiti maandamano.

Mbali na hayo, Trudeau ameonekana kuwakera wananchi wengi kutokana na msimamo wake wa kuungana mkono mapenzi ya jinsia moja na kubadili jinsia (LGBT).

Katika tatamini ya mwenendo wa kura, Chama cha Kiliberali Liberal nchini humo kinaonekana kuwa nyuma kwa ushawishi ikilinganishwa na chama cha upinzani cha Conservatives, kinachoongozwa na Pierre Poilievre.

Kutokana na ongezeko la gharama ya maisha na bei za bidhaa kuwa juu, wanasiasa wa chama chake na upinzani wamekuwa wakishinikiza Trudeau asigombee awamu ya nne katika uchaguzi ujao.

Wakati Trudeau akitangaza uamuzi huo, Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump amesema wakati umefika kwa Canada kuwa Jimbo la 51 (State) la Kiutawala la Marekani.

“Watu wengi nchini Canada wa atamanı taifa lao liwe Jimbo la 51 la kiutawala la Marekani,” alichapisha Trump kwenye akaunti yake ya Mtandao wa Truth.

“Marekani haitoteseka tena kutokana na changamoto za kibiashara ambazo zinekuwepo zinazosababishwa na bidhaa za Canada. Justin Trudeau alilijua hili na ameamua kujiuzulu,” ameandika Trump.

Rais huyo mteule, alisema endapo Canada itakuwa sehemu ya Marekani hakutokuwa na kodi hizo, badala yake raia wake watatozwa Kodi kiduchu nchini humo na watakuwa salama wanapouza bidhaa zao.

“Sipati picha tutakuwa na taifa la aina gani tukiungana,” ameandika Trump ambaye mbali na siasa, pia ni mfanyabiashara.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts