NA WILLIUM PAUL, SAME.
WANANCHI wa vitongoji vya Mahuu na Kavambughu kata ya Same wilayani Same mkoani Kilimanjaro wameingia katika historia mpya tangu kupatikana kwa Uhuru wa Taifa baada ya Serikali kufikisha huduma ya maji safi kupitia mradi wa Same – Mwanga – Korogwe.
Shangwe nderemo na vifijo vilisikika kutoka kwa wananchi hao waliokuwa wakitembea umbali wa kilomita 8 kufuata huduma ya maji baada ya jana Mkuu wa wilaya ya Same, Kasilda Mgeni kufika katika maeneo hayo na kushuhudia kwa mara ya kwanza maji yakitoka katika vituo ambavyo vimejengwa huku wananchi hao wakilitaja jina la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kama mkombozi kwao.
Kasilda alisema kuwa, wananchi wa vitongoji hivo viwili wameangaika kwa muda mrefu kutokana na tatizo la maji ambalo kwao lilikuwa tatizo kubwa lakini Rais Dkt. Samia Suluhu amejidhihirisha kuwa ni kiongozi shupavu baada ya kufikisha maji katika wilaya ya Same.
“Nimekuja kujihakikisha mwenyewe kama maji yanatoka hapa Mahuu na Kavambughu kweli wiki mbili zilizopita alikuja Naibu Waziri wa maji ambapo alitoa maagizo ndani ya wiki mbili maji yawe yanatoka hapa na mimi nimekuja kuhakikisha na nimeona leo hii maji yameanza kutoka hili ni ukombozi kwa wananchi wa Mahuu na Kavambughu” alisema Kasilda.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa, jukumu la wananchi kwa sasa ni kuhakikisha mradi huo unalindwa na kuwataka kuwa walinzi kuhakikisha mradi huo hauujumiwi na mtu yoyote mwenye nia hovu.
Alisema kuwa, wakinamama ndio walikuwa waathirika wakubwa wa tatizo la maji ambapo wamekuwa wakiangaika umbali mrefu kutafuta maji na kuwataka kuwa mstari wa mbele kulinda mradi huoi.
Kasilda alisema kuwa, ili huduma yam aji iendelee kupatikana katika vitongoji hivyo amewataka wananchi wawe wanalipa bili za maji pindi watakapopelekewa kwani sera ya maji ni wananchi kulipia ambapo fedha hizo zitasaidia kukarabati miundombinu pindi itakapoharibika.
Akisoma taarifa ya mradi wa maji Mahuu na Kavambughu, Mkurugenzi wa mamlaka ya maji Samwasa, Mhandisi Rashidi Mwinjuma alisema kuwa, serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuboresha hali ya huduma ya maji kwa wananchi wapatao 35220 wakazi wa same.
Mhandisi Mwinjuma alisema kuwa, serikali imetekeleza mradi wa maji awamu ya kwanza kwa kutoa maji katika Bwawa la Nyumba ya Mungu na kusambaza katika miji ya Mwanga na Same na vijiji vyote vilivyopitiwa na mradi huo.
Alisema kuwa, kukamilika kwa mradi huo kumewezesha uwepo wa maji ya uhakika katika miji hiyo ambapo kwa sasa wanaendelea na zoezi la kuendeleza mitandao yam aji ili kuwasogezea wananchi huduma karibu.
“Wananchi hawa walikuwa wanalazimika kutembea umbali mrefu wa kilomita 8 kufuata huduma ya maji ambapo walikuwa wakinunua ndoo ya maji shilingi 300 mpaka 500 ambapo sasa kukamilika kwa mradi huo kutaondoa hadha hiyo” alisema Mhandisi Mwinjuma.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa, mamlaka yam aji Same Mwanga (SAMWASA), walisanifu mradi wenye thamani ya zaidi ya milioni 40.8 ambao unalenga kuwasaidia wakazi wa vitongoji vya Mahuu na Kavambughu vyenye watu 5600.
Aliongeza kuwa, kwa sasa mamlaka hiyo inaendelea kutekeleza miradi mingine zaidi ya 8 ndani yam ji wa Same yenye thamani ya milioni 219.179 ili kusogeza huduma karibu kwa wakazi na kuwezesha wakazi hao kuunganishiwa huduma katika kaya zao.