LICHA ya Mbeya kuendelea kuandika historia kwa kupandisha timu Ligi Kuu Bara miaka ya karibuni, sintofahamu imebaki jinsi Uwanja wa Sokoine uliopo mjini humo unavyokimbiwa.
Mbeya ni miongoni mwa mikoa nchini yenye historia tamu kupandisha timu Ligi Kuu ikiifukuzia Dar es Salaam ambao ni kinara kwa kuwa na idadi kubwa. Kwa sasa Dar es Salaam ina timu nne za Ligi Kuu ikiwa ni Simba, Yanga, Azam na KMC japokuwa iliwahi kuwa na African Lyon, Cosmopolitan na Pan Africans na kuendelea kuwa kinara.
Mbeya ndio inafuata kwa kuingiza timu nyingi Ligi Kuu (ikiwa ni sita) ambapo iliwahi kuwa na Tukuyu Stars ambayo ilibeba ubingwa 1986, Tanzania Prisons, Mbeya City, Mbeya Kwanza, Ihefu na Ken Gold.
Mwanza inafuata kwa kuwa na timu tano zilizowahi kucheza Ligi Kuu ikiwa ni Toto Africans, Mbao FC, Alliance, Gwambina na Pamba FC iliyowahi kutwaa Kombe la Muungano 1990.
Tanga inaingia kwenye historia kwa kuwa na timu tatu zilizowahi kucheza Ligi Kuu ikiwa ni Coastal Union, Mgambo Shooting na African Sports ambazo zilishuka kwa mpigo msimu wa 2018/19 kisha Wagosi wa Kaya (Coastal) wakarejea.
Pamoja na heshima iliyowekwa kwa Mkoa wa Mbeya, lakini ishu imekuwa namna timu zinazopanda kukimbia Uwanja wa Sokoine na historia inaonyesha ni mbili kati ya tano zilitumia uwanja huo muda wote.
Timu ambazo zilitumia Uwanja wa Sokoine kwa mechi zote ni Tukuyu Stars hadi iliposhuka daraja sawa na Mbeya City ambayo ilidumu hapo iliposhuka msimu wa 2022/23.
Kwa upande wa Tanzania Prisons, imekuwa na hamahama katika mikoa flani ikianza na Morogoro kisha Rukwa kabla ya kurejea tena Sokoine kucheza mechi za nyumbani.
Mbeya Kwanza ilianzia Sokoine kwa misimu minne mfululizo ambapo baadaye iliamua kutimkia Mabatini, Kibaha mkoani Pwani ilipopandia Ligi Kuu kisha kurejea Sokoine.
Hata hivyo, haikudumu Sokoine ilipocheza mechi tisa ikiwa ni sare nane na kupoteza moja, ilikimbilia Morogoro kisha Mabatini na baadaye kuweka kambi Songea ilikoshukia daraja.
Timu hiyo licha ya kushuka daraja haikurudi tena jijini Mbeya na kuamua kukimbilia mjini Mtwara ambako hadi msimu huu wa Championship unaisha ilikuwa inatumia Uwanja wa Nangwanda Sijaona.
Kama haitoshi Ihefu nayo licha ya kutumia Sokoine ikiwa Daraja la Kwanza (Championship), ilipopanda Ligi Kuu ilitimkia wilayani Mbarali ikidai kuwapelekea burudani wakazi wa huko.
Kwa sasa Ken Gold nayo baada ya kupanda Ligi Kuu inashinikiza kutumia Uwanja wa Chunya ambao bado haujakamilika ujenzi wake. Uwanja huo ambao unatarajia kugharimu Sh8 bilioni unaweza kutumiwa na watazamaji kati ya 20,000 hadi 30,000 kwa wakati mmoja, ambapo matarajio ya Ken Gold ilikuwa ianze kuutumia mechi kwa mechi za raundi ya pili ya Championship.
Hadi sasa tayari umeshazungushiwa uzio ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Chunya imeelekeza nguvu eneo la kuchezea (pitch) pamoja na vyumba vya wachezaji na waamuzi.
Akizungumza baada ya timu kupanda Ligi Kuu, mkurugenzi wa timu hiyo, Keneth Mwambungu anasema Chunya ina uwezo kwani ni wilaya yenye vyanzo vya mapato ikiwamo uchimbaji madini.
Anasema kiu yao ni kuona wanacheza mechi zao kwenye uwanja huo kuliko kusafiri umbali mrefu kwenda Sokoine, lakini lengo lingine ni kuwasogezea burudani ya Ligi Kuu wakazi wa Chunya.
“Kwa maana hiyo tukipata huo uwanja tutaweza kurahisha safari za kuja Sokoine. Hii ni timu ya Chunya na wakazi wa huko wanatamani kuiona timu yao ikicheza nyumbani. Chunya ni wilaya tajiri yenye vyanzo vya mapato, inachimba madini ambapo inaweza kujitegemea, naomba serikali kupitia halmashauri yetu kutuahidi chochote (kuhusu uwanja),” anasema Mwambungu.
Akizungumza na wachezaji wakati wa pongezi ya kupanda Ligi Kuu na kumaliza kinara wa Championship, mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mmbaraka Batenga anasema lazima Tanzania ipelekwe Chunya.
Anasema kwa heshima waliyoiweka wachezaji wa timu hiyo katika wilaya hiyo, serikali wilayani humo itapambana kukamilisha uwanja huo ili mechi za nyumbani zipigwe palepale.
“Hiki kipo upande wetu serikali, haikuwa bahati mbaya kupanda Ligi Kuu na kuongoza ligi. Tunataka Tanzania tuipeleke Chunya. Niwapongeze wachezaji na viongozi kwa kazi nzuri,” anasema Batenga.
Kila chenye hasara hakikosi faida yake, kwani Ken Gold inapofikiria kutimka Sokoine ni kujitafutia mashabiki na kurejesha fadhila kwa wadau waliowezesha kufika hapo wa wilayani Chunya.
Pia inataka kuweka wigo mpana kusogeza soka nje ya Jiji la Mbeya kwa kuwafikia mashabiki wasiofikiwa na mchezo huo kwa urahisi hususan Ligi Kuu na kuongeza hamasa kwa vijana juu ya soka.
Lakini katika upande mwingine inaweza kujikuta ikipoteza watu ambao ilikuwa nao jijini Mbeya kwa madai ya kusalitiwa na mwisho kujikuta ikipoteana na ispokaza inaweza kushuka daraja kirahisi.
Ilishuhudiwa Mbeya Kwanza ilifanya hivyo hadi sasa haijarejea tena Ligi Kuu kufuatia uamuzi wa kukimbia Uwanja wa Sokoine na kuhamia mikoa kwenye mikoa mingine.
Chama cha soka mkoani Mbeya (Mrefa) kinasema kuhama kwa timu ni imani potofu zikidai kufanyiwa hujuma na wapinzani wao ikieleza kuwa haishauri timu yoyote kuhama nyumbani.
Mwenyekiti wa chama hicho, Sadick Jumbe anasema licha ya kanuni kuziruhusu timu kutumia uwanja wowote, lakini ingekuwa busara hata Ken Gold kubaki Sokoine, kwani mara kadhaa timu zinazohama nyumbani huwa na matokeo mabovu, akizitaja Ihefu na Mbeya Kwanza zilizowahi kufanya hivyo.
“Hizo ni imani potofu kwamba kuna mtu anahujumu na kufanya figisu. Binafsi niwashauri hata Ken Gold wabaki Sokoine japokuwa Chunya ndio kwao lakini hapa ndio wamepandia (daraja),” anasema Jumbe.