MSD YAPONGEZWA KWA MABORESHO YA HUDUMA MKOANI KAGERA

Bohari ya Dawa (MSD) imepongezwa kwa kuimarisha mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya mkoani Kagera, ambao umepunguza malalamiko ya upungufu wa bidhaa za afya mkoani humo.

Pongezi hizo zimetolewa hapo jana tarehe 6/1/2025 na Katibu Tawala wa Mkoa huo Stephen Ndaki, wakati akizungumza na ujumbe maalum kutoka MSD uliomtembelea ofisini kwake, ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MSD Bi. Rosemary Silaa, ikiwa ni ziara maalum ya kuadhimisha miaka 30 ya MSD.

Ndaki amebainisha kuwa maboresho ya huduma za MSD yamesaidia kuondoa kero na malalamiko ya mara kwa mara yaliyokuwepo miongoni mwa jamii na wateja juu ya uhaba wa Dawa vituoni, hivyo kupelekea kuimarika kwa hali utoaji wa huduma za afya Mkoani humo.

Ameongeza kwamba, mbali na kuimarika kwa utoaji huduma, hivi sasa uelewa wa majukumu ya MSD na jinsi inavyofanya kazi zake, umeongezeka miongoni mwa viongozi hivyo kuondoa kasumba ya kutupiana lawama juu ya ununuzi ya bidhaa za afya, baina ya MSD na Wateja wake, kwani viongozi wote ndani ya Mkoa huo wamejengewa uelewa.

“Hapo mwanzo kulikuwa na kelele sana kutoka vituoni kwamba tumelipa lakini MSD hajaleta, hatahivyo kwa siku za hivi karibuni malalamiko hayo yemeondoka, na uelewa juu ya mnyororo wa bidhaa za afya umeongezeka mpaka kwa viongozi, hivyo tuwapongeze kwa maboresho” Alisema Ndaki

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MSD, Bi. Rosemary Silaa, ameeleza namna MSD ilivyopitia katika vipindi tofauti, na jinsi ilivyojizatiti kuboresha huduma zake, ili kupunguza, ama kuondoa kabisa changamoto chache zilizoukabili mnyororo wa bidhaa za afya.

Ameongeza kwamba MSD imeendelea kuboresha mikataba yake na wazalishaji na washitiri, kuajiri kada mbalimbali Ili kukidhi mahitaji ya huduma za MSD kwa wateja, kuboresha na kuimarisha mifumo ya kiutendaji, kuboresha huduma na mawasiliano na wateja wake, Ili kuhakikisha inatatua changamoto chache zilizobakia katika upatikanaji wa bidhaa za afya nchini.

“Katika kipindi cha Miaka 30 ya utendaji wa MSD, hali ya utoaji huduma na upatikanaji wa bidhaa za afya nchini imeendelea kuimarika kwa kiasi kikubwa, huku out of stock zikiendelea kupungua, hivyo tunajivunia kutimiza miaka 30, na tunaahidi kuendelea kutafuta suluhu ya changamoto zilizobaki kwenye mnyororo huu wa bidhaa za afya nchini”. Alisema Silaa

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Dkt.Samuel Laizer ameipongeza MSD kwa kutimiza miaka 30, huku akisema takwimu zinaonyesha mabadiliko makubwa kwenye upatikanaji wa bidhaa za afya na huduma za MSD, ukilinganisha na miaka kadhaa iliyopita.

Ujumbe wa MSD ukiongozwa na Silaa, uko ziarani kutembelea wateja katika mikoa ya Kagera na Geita inayohudumiwa na Kanda ya MSD Kagera, kwa lengo la kupokea mrejesho wa huduma za MSD, ikiwa ni maadhimisho ya Miaka 30, toka ianze kazi zake.

 

Related Posts

en English sw Swahili