Moscow. Vikosi vya Russia vimedai kukiteka Kijiji cha Kibiashara cha Kurakhovo kilichopo Jijini Donetsk nchini Ukraine na kulifanya eneo hilo kuwa chini ya Utawala wa Russia.
Taarifa ya kukamatwa kwa Kijiji hicho cha Kurakhovo imetolewa jana Jumatatu Januari 6, 2025 na Wizara ya Ulinzi ya Russia.
Kwa mujibu wa Wizara hiyo, Kurakhovo ni Kijiji ambacho ndiyo Makao Makuu ya Mji wa Donbass. Kinategemewa kwa shughuli za usafirishaji majini na biashara nchini humo.
Tovuti ya Russia Today imeripoti kuwa kabla ya Russia kuanza operesheni zake nchini Ukraine, Februari 2022, Kijiji hicho kilikadiriwa kuwa na wakazi wanaofikia 19,000.
“Katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita, Utawala wa Ukraine ulipafanya Kurakhovo kuwa eneo la kibiashara lenye Ulinzi wa hali ya juu. Kuanzia Kaskazini kwake lilikuwa limeimarishiwa Ulinzi mkali jambo lililotupatia ugumu kuukamata,” ilisema taarifa ya Wizara hiyo.
Kwa mujibu wa Wizara hiyo, Ukraine ilipeleka wanajeshi takriban 15,000 katika Kijiji hicho wakiwemo wanajeshi wa kukodi (marcenaries) kutoka nje ya nchi.
Wanajeshi hao wanadaiwa kuwa walikuwa wamekabidhiwa vifaa ikiwemo vifaru na makombora kwa ajili ya kulinda Kijiji hicho.
“Kutokana na weledi wa vikosi vya Russia wakati wa mapigano ya kukikomboa kijiji hicho, Ukraine ilipoteza takriban asilimia 80 ya wanajeshi wake yaani wanajeshi 12,000 wakiwemo 3,000 waliokuwa kwenye vitengo vya silaha na vifaru 40,” ilisema taarifa hiyo.
Kabla ya mapigano ya jana, Wizara hiyo imesema kwenye mapigano yaliyodumu kwa wiki mbili zilizopita katika kijiji hicho kati ya Russia na Ukriane, inakadiriwa kuwa wanajeshi kati ya 150 hadi 180 walifariki ama kujeruhiwa wa kutokana na mapigano katika pande hizo.
Wizara hiyo ilidai kitendo cha kukiteka na kutwaa kijiji hicho, cha Kurakhovo kitakwamisha usafirishaji wa silaha na vikosi vya wanajeshi wa Ukraine kwenda maeneo mengine ya taifa hilo.
Pia imesema kitendo hicho kinavikwamisha vikosi vya Ukraine kufika katika Mkoa wa Donetsk ambapo Russia imeshauteka kwa kiwango kikubwa baada ya kuanza Operesheni zake nchini humo Februari 2022.
“Baada ya kukikamata kijiji cha Kurakhovo, sasa vikosi vya Russia vitakuwa na uwezo wa kubadilisha mapigo kwa Ukraine. Pia itaongeza kasi ya kusonga mbele katika Mkoa wa Donetsk,” imesema.
Wakati Russia ikidai kuiteka Kurakhovo, mapigano katika Mkoa wa Kursk yanatajwa kushika kasi huku Tovuti ya BBC ikiripoti kuwa majeshi ya Russia yalifanyiwa shambulizi la kushtukiza.
Baada ya kufanyiwa mashambulizi ya kushtukizwa, Vikosi vya Russia vilijibu mapigo kwa kulipua vifaru vilivyokuwa na wanajeshi wa Ukraine, huku zaidi ya vifaru 10 vikiharibiwa.
Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Russia, pamoja na kukiri kuwepo uvamizi huo wa kushtukiza wa vikosi vya Ukraine, pia imesema jitihada za kuvirudisha nyuma zinaendelea.
Kwa mujibu wa Wizara hiyo, Vikosi vya Ukraine vililenga kutwaa Mji wa Bolshoye na Soldatskoye na kusema jaribio hilo limedhibitiwa.
Pia ilisema kupitia mashambulizi hayo, Russia imewaua wanajeshi 485 wa Ukraine eneo la Kursk, kuharibu vifaru 10, gari moja ya kurusha makombora, na magari kadhaa ya kubebea wanajeshi.
Mwandishi wa BBC, Will Vernon anayeripoti kutokea Ukraine amesema ni vigumu kueleza madhara yaliyosababishwa na uvamizi wa Ukraine kwenye vikosi vya Russia kutokana na usiri mkubwa kugubika utoaji wa taarifa za madhara ya vita hiyo nchini Russia.
Hata hivyo, Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine amesema anaamini Ukraine itashinda vita hiyo endapo utawala mpya wa Marekani chini ya Rais Donald Trump utaliunga mkono taifa hilo.
Vikosi vya Ukraine vimekuwa moto wa kuotea mbali, vinapofanya mashambulizi eneo la Kursk jambo lililoilazimu Russia kupeleka wanajeshi wa ziada kutoka Korea Kaskazini katika eneo hilo mwishoni mwa Oktoba 2024.
Wakati wa Kikao chake cha Mwisho wa mwaka na vyombo vya habari, Rais wa Russia Vladimir Putin alitamka wazi kuwa hana hofu kuwa vikosi vya Ukraine vilivyopo eneo la Kursk vitashambuliwa na kuondolewa eneo la Mkoa huo.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.