Dar es Salaam. Watu sita wakiwamo wafanyabiashara wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni iliyoko Kinondoni, wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kutumia mashine ya kielektroniki ya kutolea risiti (EFD).
Washtakiwa hao ni Stanslaus Mushi, Edwin Mark na Nemence Mushi ambao ni wafanyabiashara, Rose Nanga (mhasibu), Hussein Mlezi, (fundi kompyuta) na Salim Kajiru Salehe, fundi rangi.
Watuhumiwa hao walipandishwa kizimbani mahakamani hapo jana jioni Jumatatu, Januari 6, 2025 na kusomewa mashtaka 68 ya udanganyifu kwa kutumia mashine ya EFD na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh2.16 bilioni za Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Washtakiwa hao walisomewa mashtaka hayo na waendesha mashtaka wakili wa Serikali, Auni Chilamula na Daisy Makakala.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalira aliwaeleza kuwa, hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kisheria kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu.
Mashtaka 64 ni ya udanganyifu wa kutumia mashine ya EFD kwa namna ya kuupotosha mfumo wa TRA, kinyume na kifungu cha 86 (1) (d) na (3) cha Usimamizi wa Kodi, Sura ya 438, Marejeo ya Mwaka 2019.
Katika mashtaka hayo, washtakiwa wote wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati Novemba mosi na 30, 2024 and 30, 2024, katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam.
Wanadaiwa kutumia mashine ya EFD namba 03TZ843058288, mali ya Hadija Songea kutoa risiti za EFD za uwongo na kuupotosha mfumo au Kamishna Mkuu wa TRA.
Mashtaka mengine matatu yaani ya 65, 66 na 67 ni ya kujipatia usajili kwa njia za udanganyifu kinyume na kifungu cha 309 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Marejeo ya mwaka 2022.
Katika shtaka la 65, Stanslaus, Nemence na Rose wanadaiwa kujipatia usajili wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi, namba 171-875-137 kwa jina la Hadija Nassoro Songea wakijua ni utambulisho wa uwongo kitendo ambacho ni kinyume na sheria.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Juni mosi na 30, 2024 katika maeneo tofauto jijini Dar es Salaam.
Shtaka la 66 washtakiwa hao watatu Stanslaus, Nemence na Rose wanadaiwa kujipatia usajili wa VAT kwa njia ya udanganyifu, wakidaiwa kutenda kosa hilo kati ya Oktoba mosi na 31, 2024.
Shtaka la 67 likiwakabili mshtakiwa wa Stanslaus na Rose wanaodaiwa kujipatia usajili wa EFD namba 03TZ843058288 kwa jina la Hadija Nassoro Songea, wakidaiwa kutenda kosa hilo kati ya Juni mosi na 30, 2024.
Shtaka la 68 ni kuisababishia mamlaka hasara kinyume na kifungu cha 284A cha Kanuni ya Adhabu kikisomwa pamoja na aya ya 38 katika jedwali la kwanza na kifungu cha 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhalifu wa Kupanga na Uhujumu Uchumi Sura ya 200 Marejeo ya Mwaka 2022.
Hakimu Rugemalira baada ya kusomwa mashtaka hayo aliwaambia watuhumiwa kuwa, Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, hivyo hawatatakiwa kujibu chochote kuhusu mashtaka hayo. Shauri hilo limeahirishwa Januari 20, 2025.