Jeshi la Israel limesema ndege yake ya kivita iliwalenga magaidi katika eneo la Tamun la Bonde la Jordan. Shambulizi hilo la Israel kwenye Ukingo wa Magharibi limetokea baada ya Waisrael watatu kuuawa na watu wengine wanane kujeruhiwa katika shambulizi lililotokea kaskazini mwa Ukingo huo.
Vyombo vya habari viliripoti kuwa mshambuliaji wa Kipalestina alilifyatulia risasi basi akiwa kwenye gari katika eneo la al-Funduq, magharibi ya mji wa Nablus.
Mkuu wa majeshi ya Israel Luteni Jenerali Herzi Halevi alisema alipotembelea eneo la tukio kuwa jeshi litaendeleza msako wake dhidi ya wanamgambo wenye silaha katika Ukingo wa Magharibi. “Tuko katika mapambano makali na makubwa dhidi ya ugaidi huko Yudea na Samaria. Tutazidisha na kuendeleza mapambano haya. Kwa magaidi waliofanya shambulio hili, siku zenu zimeanza kuhesabika. Tutajua ni nani waliofanya shambulizi hili, na tutawafikia.”
Naye waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kuwawajibisha wote waliohusika.
Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani – WFP limeituhumu Israel kwa kuushambulia moja ya misafara yake ya msaada katika Ukanda wa Gaza. Limesema risasi 16 ziliyapiga magari yao yaliokuwa na vibandiko vya utambulisho, lakini hakuna aliyejeruhiwa.
Taarifa ya shirika hilo imesema magari hayo yalilengwa katika kituo cha ukaguzi cha Wadi Gaza. WFP kwa mara nyingine imezitaka pande zote za mzozo kuheshimu sheria ya kimataifa ya kibinaadamu, kuyalinda maisha ya raia, na kuruhusu usafirishwaji salama wa msaada wa kiutu.
Jeshi la Israel limesema limepokea ripoti za msafara kufyatuliwa risasi, lakini halikueleza chanzo cha tukio hilo.
Limesema tukio hilo lilichunguzwa na matokeo yatafanyiwa tathmini. Jeshi hilo limesema Israel inaendelea kupambana na makundi ya kigaidi katika Ukanda wa Gaza na inafanya kila liwezekanalo kupunguza madhara kwa raia wasiohusika.
Israel na Hamas zatofautiana kuhusu mateka
Kwenye uwanja wa kidiplomasia, Israel na Hamaskwa mara nyingine zinaonekana kukaribia kufikia makubaliano ya usitishaji mapigano ambayo yatasimamisha vita vilivyodumu kwa miezi 15 huko Gaza na kuwarejesha nyumbani makumi ya Waisrael wanashikiliwa mateka.
Israel na Hamas wako chini ya shinikizo la rais wa Marekani anayeondoka Joe Biden na Rais mteule Donald Trump kufikia makubaliano kabla ya kuapishwa kwa rais mpya Januari 20.
Duru ya karibuni kabisa ya mazungumzo inajikita zaidi kwenye majina ya mateka wanaopaswa kuachiliwa katika awamu ya kwanza, kwa mujibu wa maafisa wa Israel, Misri na Hamas, ambao walizungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao kwa sababu washiriki kwenye mazungumzo yanayoendelea.
Israel inataka uhakikisho kuwa mateka hao wako hai, wakati Hamas inasema kuwa baada ya miezi mingi ya mapigano makali, haina uhakika kama wako hai au walikufa.